Tafuta

Ajali ya moto Msamvu, Morogoro Tanzania. hadi kufikia Jumapili jioni watu waliofariki dunia walikuwa ni 71 huku wengine 59 wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Kifo hakizoeleki hata kidogo! Ajali ya moto Msamvu, Morogoro Tanzania. hadi kufikia Jumapili jioni watu waliofariki dunia walikuwa ni 71 huku wengine 59 wakiwa wamejeruhiwa vibaya. Kifo hakizoeleki hata kidogo! 

Ajali ya moto Msamvu Morogoro: Kutoguswa na mateso ya wengine ni upagani mamboleo!

Taarifa rasmi inaonesha kwamba, hadi kufikia Jumapili jioni, watu 71 walikuwa wamefariki dunia kutokana na ajali ya moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori kupinduka. Kuna watu 59 ambao wamejeruhiwa. Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa, Jumapili tarehe 11 Agosti 2019 ameongoza umati wa watanzania katika maziko ya watu waliofariki dunia.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.- Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Romania hivi karibuni, aligusia pia kuhusu ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayoendelea kukuza na kudumisha ubinafsi na choyo, kiasi cha watu kujifikiri na kujitafuta wenyewe, na hivyo kushindwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao. Hiki ni kielelezo cha upagani mamboleo. Kuna wakimbizi na wahamiaji wanaokufa maji kwenye Bahari ya Mediterrania; wanaoteseka kwa njaa na kiu ya kutisha kwenye Jangwa la Sahara; kuna watu wanaokufa kwa baa la njaa na utapiamlo, lakini kuna watu wanaokula na kusaza, kiasi hata cha kufanya kufuru. Matukio ya majanga na maafa sehemu mbali mbali za dunia, yanaanza kuzoeleka na kuwa si tena sehemu ya habari inayovuta hisia za huruma, upendo na mshikamano na watu kama hawa!

Hizi ni dalili za upagani mamboleo. Badala ya kuthamini, utu, heshima na haki msingi za binadamu, watu wanavutwa na tamaa ya vitu; badala ya kuokoa, watu wanataka kufaidika na majanga yanayowakumba watu. Kuna haja ya kuendelea kuwaelimisha watu umuhimu wa kuheshimu utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huzuni, simanzi, majonzi na vilio vilitawala mjini Morogoro, Jumapili tarehe 11 Agosti 2019 wakati Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akiongoza umati wa wananchi wa Manispaa ya Morogoro, mkoani Morogoro katika mazishi ya wananchi waliofariki dunia kutokana na ajali ya moto wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 71 huku wengine 59 wakijeruhiwa. Mazishi hayo yameanza kufanyika Jumapili, Agosti 11, 2019) katika eneo la makaburi la Kilima cha Kola, mjini Morogoro ambapo Waziri Mkuu amemwakilisha Rais, Dkt. John Pombe Magufuli.

Waziri Mkuu ametoa pole kwa wafiwa wote na amewaomba wananchi wawe watulivu katika kipindi hiki cha maombolezo. Akizungumza na wananchi katika ibada ya kuwaombea marehemu waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea katika eneo la Msamvu mjini Morogoro iliyofanyika kwenye viwanja vya Hospitali ya Mkoa wa Morogoro, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano waliouonesha wakati huu wa majonzi. Kufuatia ajali hiyo iliyotokea Jumamosi saa 2 asubuhi baada ya lori lenye shehena ya mafuta ya petrol kupinduka jirani na Kituo Kikuu cha Mabasi cha Msamvu mjini Morogoro, wakati dereva alipokuwa akijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki. Rais Dkt, Magufuli ametangaza siku tatu za maombolezo ya Kitaifa kuanzia Jumamosi Agosti 10, 2019 na bendera zote zipeperushwe nusu mlingoti.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameunda Tume maalumu kwa ajili ya kufanya uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali ya moto iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 69 hadi mchana huu na wengine 70 kujeruhiwa wakati wakichota mafuta yaliyokuwa yakimwagika baada ya lori la mafuta kupinduka, mjini Morogoro. “Hii tume inaanza kazi Jumapili, Agosti 11, 2019, Hadi ijumaa inipe taarifa yake na hata kama mimi sijawajibika initaje. Ajali ya namna hii si mara ya kwanza ilitokea Mbeya eneo la Mbalizi. Naomba niwasihi Watanzani pale gari linapoanguka tusitumie kama fursa twende tukaokoe binadamu waliopo pale”. Waziri Mkuu ameunda tume hiyo Jumapili, Agosti 11, 2019, wakati akizungumza na waombolezaji waliofika katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa ajili ya kutambua miili ya ndugu zao. Niko mbele yenu nikimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli aliyenituma kuja kuungana nanyi kwenye siku hii ya huzuni”.

Waziri Mkuu amesema lazima wajiridhishe kama Serikali ilitekeleza vizuri jukumu lake kwa sababu ajali imetokea saa mbili asubuhi katikati ya mji, hivyo tunataka kujua ajali ilipotokea kila mmoja alitumiza jukumu lake. Amesema ajali imetokea karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi na kuna Polisi.  Sasa Je, hawa wananchi waliopata ajali walienda na madumu ya kuchotea mafuta ina maana waliamka asubuhi wakijua ajali itatokea. “Najua pale ajali inapotokea Trafiki wana wahi haraka hata kama kwa gari la kukodi. Watu walikuja na madumu, wengine kuchomoa betri nani aliwazuia. Je, lilipoanza kuungua gari la zima moto lilikuja kwa wakati gani”. Waziri Mkuu amesema lazima wajiridhishe ndani ya Serikali kama wamewajibika. “Kuna vitu vingi lazima tuviangalie tujue nani hakutimiza majukumu yake. Nadhani ujumbe mnaupata si vyema tutakimbilia vitu badala ya watu. Tunasikitika sana kwa yaliyotukuta hata upande wa Serikali tunasikitika kuwapoteza Watanzania”.

Pia, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu jitihada za kuokoa waliopata majeraha kwamba, zinaendelea vizuri na jukumu lao kubwa kuwaombea marehemu wapumzike kwa amani na pia wawaombee wajeruhi waweze kupona. Waziri Mkuu ameongeza kuwa, Rais Dkt. Magufuli tayari ameshatoa kibali cha kutolewa fedha kwa ajili ya kununuliwa vifaa tiba na dawa zinazohitajika. Akizungumzia kuhusu idadi ya vifo na majeruhi waliotokana na ajali hiyo ambayo inatangazwa kupitia vyombo mbali mbali vya habari, Waziri Mkuu amesema ni vema takwimu hizo wakaacha zikatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Bw. Stephen Kebwe. “Kwenye vyombo vya habari tuelewane kwenye takwimu za vifo na majeruhi. Msiseme suala la takwimu anayetoa ni Mkuu wa Mkoa na matukio haya yapo chini yake. Nimeamua kusema hivi hizi takwimu zikitajwa nyingi nyingi mnajenga hofu na taharuki kwa wananchi. Hili halikubaliki mkitaka taarifa mtafuteni mkuu wa mkoa”.

Habari zaidi zinasema, Rais Dkt. Magufuli alipokea taarifa mapema ya ajali ya lori la mafuta na kusababisha vifo vya Watanzania 69, ambapo alimtaka aende mkoani Morogoro kwa ajili ya kuwasilisha salamu za pole kwa wananchi wa Morogoro na Tanzania kwa ujumla kufuati tukio hilo la kuhuzunisha. Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawaombea marehemu na majeruhi lakini pia amawataka wafiwa na wananchi wote wawe watulivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na wapendwa wao. “Mheshimiwa Rais amehuzunishwa sana na msiba huu ndio maana amenituma nilete ujumbe huu kwenu.Lakini pia nimekuja na salamu za pole kutoka kwa Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan. Jambo hili si dogo ni kubwa kwani tumepoteza ndugu zetu wengi. Kwa idadi hii kubwa ya ndugu zetu waliotangulia mbele za haki na wale waliopo kwenye maumivu si jambo la faraja”.

Waziri Mkuu amesema wananchi wasipeleke miili kwanza makaburini ili waweze kupitia na kutambua ndugu na rafiki kwa ajili ya kuwa na kumbukumbu ya kudumu. “Hali si nzuri ndugu zetu wameungua sana wapo wengine mnaweza msiwatambue lakini mnaweza kutambua kwa alama. Wapo wengine walivaa bangili, heleni, mkanda havijaungua”. Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kama hawajawatambua Serikali imeweka utaratibu wa vipomo vya vinasaba, ambapo kumbukumbu hizo zimechukuliwa na wataalamu wetu wa afya. “Kama ukipita ukishindwa kumuona bado tunakuruhusu kukupima vinasaba na kulinganisha na vya kwako. Bado haki ya kumpata ndugu yako iko pale pale madaktari wapo, mitambo ipo tutachukua vinasaba na kuainisha tutatoa nafasi leo hadi saa 10 kufanya utambuzi”.

Amesema Serikali inaratibu vizuri jambo hilo lakini kuanzia saa 10 imeruhusu wale waliotambuliwa kuchukua mwili lakini kama hawajajipanga vizuri itauzika na kama kuna jina litaliandika na kama hakuna jina wataandika namba ya vinasaba ili kutoa fursa kwa ndugu siku nyingine waende wakapimwe na kuoneshwa kaburi la ndugu yao. Mazishi hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI, Selemani Jafo, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isac Kamwelwe, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. Wengine ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba, Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Ashatu Kijaji pamoja na wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wabunge, viongozi wa dini na wananchi wa mkoa wa Morogoro.

12 August 2019, 12:13