Ajali ya Msamvu, Morogoro 10.8.2019: Watu zaidi ya 60 wamefariki dunia, na wengine 70 kujeruhiwa vibaya. Rais Magufuli aitaka Serikali kuwahudumia majeruhi ili kuokoa maisha yao! Ajali ya Msamvu, Morogoro 10.8.2019: Watu zaidi ya 60 wamefariki dunia, na wengine 70 kujeruhiwa vibaya. Rais Magufuli aitaka Serikali kuwahudumia majeruhi ili kuokoa maisha yao! 

Ajali ya moto Msamvu Morogoro: Watu zaidi ya 60 wamefariki dunia

Rais John Pombe Magufuli amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 60 na majeruhi takribani 70 walioungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kulipuka moto mjini Morogoro, Jumamosi tarehe 10 Agosti 2019 baada ya lori hili kupinduka wakati likijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta kumwagika na kushika moto.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ya Mungu nchini Tanzania imekumbwa na majonzi makubwa, baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta kupinduka eneo la Msamvu, Manisapaa ya Morogoro na kuwaka moto uliopelekea zaidi ya watu 60 kupoteza maisha kwa kuteketea kwa moto! Taarifa za vyombo vya ulinzi na usalama vimebaini kwamba, katika eneo la tukio piki piki 10 maarufu kama “Bodaboda” zimeungua moto na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa ajali hii. Maiti zimehifadhiwa kwenye Hospitali ya Mkoa wa Morogoro na utambuzi unaendelea kufanyika. Pengine idadi ya watu waliofariki katika ajali hii ikaongezeka maradufu kwa sababu kuna baadhi ya watu wameteketea kabisa na wala hakuna alama yoyote iliyobakia kutokana na ukali wa moto! Mashuhuda waliokuwa kwenye eneo la tukio wanasema, mara baada ya lori lililokuwa limebeba mafuta aina ya petroli kupinduka na mafuta hayo kuanza kumwagika, baadhi ya watu walikimbilia kwenye eneo la tukio na kuanza kuchota mafuta haya na baada ya muda mfupi, moto mkubwa ukalipuka na huo ukawa ni mwanzo wa maafa makubwa kwa watu na mali zao Manispaa ya mji wa Morogoro.

Wachunguzi wa mambo wanasema, bado kunahitajika elimu makini na endelevu kwa ajili ya watu kujiokoa na majanga kama haya! Mara nyingi watu wengi wameponzwa na uchu wa kutaka kufaidika na mafuta yanayomwagika wakati wa ajali kama hizi, lakini matokeo yake ni maafa makubwa kama ambavyo pia imetokea katika historia ya matukio kama haya ndani na nje ya Tanzania. Jambo la pili ni kuheshimu na kuthamini utu wa watu waliopoteza maisha katika matukio kama haya! Kumezuka utamaduni wa ovyo wa watu kusambaza picha za watu waliofariki katika ajali mbaya kama hizi, hali ambayo inakwenda kinyume kabisa cha maadili, utu, heshima na haki msingi za binadamu! Wakati huo huo, Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa ya vifo vya watu 60 na majeruhi takribani 70 walioungua kwa moto baada ya lori lililokuwa na shehena ya mafuta kupata ajali na kisha kulipuka moto mjini Morogoro. Ajali hiyo imetokea Jumamosi tarehe 10 Agosti 2019 majira ya saa 2 asubuhi baada ya lori hili kupinduka wakati likijaribu kumkwepa mwendesha pikipiki na kisha mafuta yaliyokuwa yakimwagika kushika moto na kuunguza watu waliokuwa wanayachota.

Rais Magufuli ametoa rambi rambi kwa wote walioguswa na msiba huu mzito na anawaombea majeruhi ili wapone haraka. Rais Magufuli ameagiza Wizara zote zinazohusika kushughulikia ajali hi ina ametaka Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuhakikisha majeruhi wote wanapatiwa matibabu na kuokoa maisha yao. Aidha Rais Magufuli amesikitishwa na vitendo vya watu kuvamia magari yanayopata ajali kwa lengo la kujipatia bidhaa mbali mbali zilizobebwa na magari hayo na ametaka vitendo hivyo vikome. Kwa sababu kuna magari yanayobeba kemikali za sum una milipuko, kumbe hii si tabia ya kuendekezwa hata kidogo!

 

10 August 2019, 14:00