Tafuta

Wizara ya Kilimo Tanzania imetoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2018/2019 na upatikanaji wake kwa mwaka 2019/2020 Wizara ya Kilimo Tanzania imetoa taarifa ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa mwaka 2018/2019 na upatikanaji wake kwa mwaka 2019/2020 

Hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula 2018/2019 na Upatikanaji wake

Wizara ya Kilimo nchini Tanzania katika taarifa yake inasema, Hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini Tanzania imeendelea kuwa nzuri katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula kuanzia msimu wa kilimo wa 2013/2014 hadi 2017/2018 ambapo kwa msimu wa 2018/2019 nchi imejitosheleza ikilinganishwa na mahitaji.

Na Japhet Ngailonga Hasunga (Mb), Dar Es Salaam.

Ifuatayo ni taarifa iliyotolewa na Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Japhet Hasunga (Mb) wakati akizungumza na waandishi wa habari tarehe 18 Julai 2019 kuhusu taarifa ya hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kwa msimu wa 2018/2019 na upatikanaji wake kwa mwaka 2019/2020. Kila mwaka kati ya mwezi Mei na Juni, Wizara ya Kilimo kwa kushirikiana na Wadau mbalimbali hufanya tathmini ya hali ya uzalishaji wa chakula na upatikanaji ili kujua; Mosi, hali ya kiujumla ya uzalishaji wa mazao na upatikanaji wa chakula kwa Mikoa na Halmashauri zote. Pili, ni kuangalia uzalishaji wa mazao ya chakula na utekelezaji wa malengo ya uzalishaji hadi tarehe 31 Mei kila mwaka. Tatu, ni athari za visumbufu katika uzalishaji wa mazao. Nne ni bei ya mazao ya chakula na hali ya upatikanaji wa chakula sokoni katika Halmashauri zote na kuainisha maeneo yenye dalili ya uhaba. Tano ni hali ya unyeshaji wa mvua na mwenendo wa uzalishaji wa mazao mashambani

Hali ya uzalishaji na upatikanaji wa mazao ya chakula nchini Tanzania imeendelea kuwa nzuri katika kipindi cha miaka mitano mfululizo kufuatia uzalishaji wa ziada wa mazao ya chakula kuanzia msimu wa kilimo wa 2013/2014 hadi 2017/2018 ambapo kwa msimu wa 2018/2019 nchi imejitosheleza ikilinganishwa na mahitaji. Katika kufanya tathmini ya hali ya chakula, hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula na usalama wa chakula tunaangalia baadhi ya mazao muhimu yanayohitajika zaidi kama vile mahindi, mtama na ulezi, mchele, mikunde, ngano, ndizi, muhogo na viazi. Katika kipindi hicho, nchi imekuwa na kiwango cha utoshelevu kati ya asilimia 120 hadi 125 na imekuwa ikizalisha ziada kati ya tani 2,582,717 hadi 3,322,689. Mafanikio hayo yanatokana na sababu mbalimbali ikiwemo hali ya hewa nzuri, pamoja na usimamizi na utekelezaji mzuri wa sera na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Serikali pamoja na Wadau wengine wa masuala ya kilimo ili kuongeza tija na uzalishaji. Wizara ya Kilimo mwezi Mei hadi Juni 2019 ilifanya Tathmini ya Hali ya Uzalishaji wa Mazao ya Chakula kwa msimu wa 2018/2019 na Upatikanaji wa Chakula kwa mwaka 2019/2020 katika mikoa yote 26 Tanzania Bara kwa lengo kubaini uzalishaji na mahitaji.

Matokeo yanaonesha kuwa hali ya uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa katika msimu wa 2018/2019 utafikia tani 16,408,309 kwa mlinganisho wa nafaka (Grain Equivalent) ambapo nafaka ni tani 9,007,909 na siyo nafaka tani 7,400,400. Ikilinganishwa na msimu uliopitauzalishaji wa mazao ya chakula umeshuka kwa tani 483,665 ambapo nafaka hususan mahindi yameshuka kwa tani 455,642 na mchele kwa tani 210,454. Aidha, uzalishaji wa mazao siyonafaka (non cereals) umeongezeka kwa tani 46,283. Uzalishaji wa mazao ya nafaka ulifikia asilimia 103 na mazao yasiyo ya nafaka yalifikia asilimia 145. Hivyo, uzalishaji wa jumla wa mazao ya nafaka na yasiyo ya nafaka ulifikia asilimi 119. Aidha mchango wa uzalishaji wa mazao ya chakula kitaifa katika msimu wa 2018/2019 unaonesha kuwa mahindi yamechangia kwa asilimia 35, muhogo kwa asilimia 17, mchele kwa asilimia 12, viazi kwa asilimia 10 na mazao mengine. Pamoja na hali hiyo, utengamano wa usalama wa chakula unatarajiwa kuwa wa viwango tofauti kimkoa. Aidha, hali ya uwepo na upatikanaji wa chakula kwa sasa ni nzuri kutokana na uzalishaji mzuri wa msimu wa 2017/2018.

Kwa kuzingatia Kigezo cha Upimaji wa Kiwango cha Utoshelevu (Self Sufficiency Ratio – SSR), matokeo yanaonesha kuwa kwa mwaka wa chakula 2019/2020, nchi itakuwa na kiwango cha Utoshelevu cha asilimia 119. Tathmini imeonesha, hali ya chakula inatarajiwa kuwa ya kiwango chaZiada kwenye mikoa 11 ya Rukwa, Ruvuma, Songwe, Katavi, Njombe, Mbeya, Kigoma, Iringa, Kagera, Morogoro, na Mtwara kwa asilimia 128 hadi 227. Aidha, kutakuwa na hali ya Utoshelevu kwenye mikoa 7 ya Geita, Simiyu, Pwani, Lindi, Manyara, Singida na Tanga kwa asilimia 109 hadi 119 na Upungufu kwenye mikoa 8 ya Dodoma, Mara, Mwanza, Arusha, Tabora, Shinyanga na Kilimanjaro kwa asilimia kati ya 98 hadi 99. Mkoa Dar es Salaam si miongoni mwa mikoa ya uzalishaji wa mazao na hivyo kujitosheleza kwa asilimia 3 tu kutokana na eneo dogo linalolimwa lisilokidhi mahitaji ya chakula ya wakaazi wake. Ingawa mkoa huu unawekwa kwenye upungufu wa chakula kwa maana ya uzalishaji katika mashamba, mkoa huu una vyakula vingi vinavyoingia sokoni kutoka katika mikoa 25 ya Tanzania bara na hivyo kuwa na Utoshelevu kwa vipindi vyote.  

Tathmini imebainisha kuwa uwepo wa maeneo (pockets) yenye dalili za upungufu wa chakula kwenye Halmashauri 46 katika mikoa 13kama ifuatavyo; Mkoa wa Dodoma katika Halmashauri 7 za Bahi, Chamwino, Chemba, Kondoa, Kongwa na Mpwapwa. Mkoa wa Mara katika Halmashauri 5 za Bunda DC, Bunda TC, Musoma DC, Musoma MC na Rorya. Mkoa wa Tabora katika Halmashauri 5 za Uyuyi, Igunga, Nzega DC, Nzega TC na Kaliua. Mkoa wa Shinyanga katika Halmashauri 4 za Kishapu, Shinyanga DC, Shinyanga MC na Msalala. Mkoa wa Kilimanjaro katika Halmashauri 4 za Mwanga, Same, Siha na Hai. Mkoa wa Mwaza katika Halmashauri 4 za Misungwi, Ukerewe, Kwimba na Sengerema. Mkoa wa Manyara katika Halmashauri 4 za Simanjiro, Kiteto, Hanang na Mbulu TC. Mkoa wa Simiyu katika Halamshauri 4 za Itilima, Maswa, Meatu na Busega. Mkoa wa Arusha katika Halamshauri 3 za Longido, Ngorongoro na Monduli. Mkoa wa Singida katika Halmashauri 3 za Ikungi, Manyoni na Singida DC. Mkoa wa Tanga katika Halmshauri 1 ya Tanga jiji. Mkoa wa Lindi katika Halmashauri 1 ya Lindi DC na Mkoa wa Iringa katika Halmashauri 1 ya Iringa DC.

Ndugu Wanahabari Msimu wa uzalishaji wa 2018/2019 ulikabiliwa na changamoto mbalimbali katika baadhi ya maeneo zilizoathiri uzalishaji wa mazao kwa viwango tofauti na kusababisha kushuka kwa uzalishaji wa mazao hususan zao la mahindi. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na: Katika maeneo yanayopata mvua misimu miwili (Bimodal Areas) mvua za vuli katika maeneo mengi hazikufanya vizuri. Aidha, mvua za masika zilichelewa sana kuanza na hivyo kuathiri shughuli za kilimo katika maeneo hayo. Pili, kuchelewa kuanza kunyesha kwa mvua na mtawanyiko usioridhisha kwenye baadhi ya maeneo ya nchi yanayopata mvua msimu mmoja (Unimodal Areas) hususan katika mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, na baadhi ya maeneo ya mikoa ya Morogoro, Mwanza, Mara, Simiyu na Manyara. Tatu ni visumbufu hususan viwavijeshi vamizi (Fall Army Worm - FAW), panya na Kweleakwelea.

Kufuatia matokeo ya Tathmini hii, Serikali inachukua / itachukua hatua zifuatazo; Kuimarisha Mfumo wa ukusanyaji taarifa za usalama wa chakula nchini ili kuweza kuchukua hatua stahiki pindi inapobidi. Kufanya Tathmini ya Kina ya Hali ya Chakula na Lishe mapema katika Halmashauri zilizobainika kuwa na maeneo yenye viashiria vinavyoweza kusababisha upungufu wa chakula. Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko wanatarajia kuanza ununuzi wa mazao ya chakula kutoka kwenye maeneo yenye ziada. Kuimarisha mfumo wa upatikanaji na usambazaji wa pembejeo za kilimo ikiwemo viuatilifu, mbegu na mbolea. TRA pamoja na Wataalam wa kilimo katika vituo vya mipaka ya nchi kusimamia kikamilifu usafirishaji wa mazao yanayokwenda nje ya nchi ili kusaidia upatikanaji wa takwimu sahihi za kiasi kinachosafirishwa nje ya nchi.

Ndugu Wanahabari Niwatake wananchi wote nchini kuzalisha mazao ya chakula kwa kuzingatia kanda za kiekolojia, kuwa na hulka ya kuhifadhi chakula kulingana na mahitaji ya kaya pamoja kutumia mazao ya chakula kilichopatikana vizuri kiweze kutumika hadi kufikia msimu mwingine wa uzalishaji. Aidha, Wakulima waliopata chakula cha ziada wanashauriwa wasiharakishe kuuza mazao yao mapema bali wasubiri hadi bei zitakapokuwa nzuri ndipo wauze na kwa wale wenye waliopata utoshelevu kidogo wa chakula watumie vizuri mazao hayo kwa ajili ya chakula na si vinginevyo.

ASANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

Japhet Ngailonga Hasunga (Mb)

WAZIRI WA KILIMO

18 Julai 2019

20 July 2019, 15:16