Serikali ya Tanzania imewataka viongozi wa kidini kuendelea kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa! Serikali ya Tanzania imewataka viongozi wa kidini kuendelea kuwekeza zaidi katika malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya ili kudumisha haki, amani, utulivu na umoja wa kitaifa! 

Serikali ya Tanzania: Viongozi wa kidini imarisheni malezi ya vijana

Viongozi wa dini waendelee kuimarisha. Malezi na mafundisho ya kiroho kwa vijana na kuepusha mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema, ili Taifa la Tanzania liendelee kung’ara, kuheshimika na kusifika kwa utulivu, amani na umoja na mshikamano wa kitaifa! Serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo CCT kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Na Mwandishi Maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Dodoma.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini waendelee kuimarisha:Makuzi, malezi na mafundisho ya kiroho kwa vijana na kuepusha mmong’onyoko wa kanuni maadili na utu wema, ili Taifa la Tanzania liendelee kung’ara, kuheshimika na kusifika duniani kwa utulivu, amani na umoja na mshikamano wa kitaifa! Amesema Serikali inatambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) katika kutengeneza mustakabali mwema na ustawi wa familia kupitia mahubiri ya Habari Njema ya Wokovu na malezi ya kiroho kwa waamini wao, ili kujenga na kudumisha familia imara na thabiti, zinazoweza kutangaza na kushuhudia wema na ukuu wa Mungu katika maisha yao.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Ijumaa, Julai 5, 2019, wakati alipomwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye Mkutano wa Halmashauri Kuu ya 53 ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) ulioambatana na harambee ya kukusanya fedha kwa ajili ya ujenzi wa kitegauchumi cha Jumuiya hiyo. Mkutano ambao umefanyika Jijini Dodoma. Amesema Serikali inatambua mchango wa malezi ya kiroho katika ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla, na mafundisho yake kwani yamesaidia kujenga watumishi wa umma ambao wamelelewa katika misingi bora ya kumcha Mwenyezi Mungu. Waziri Mkuu amesema Serikali inaamini kwamba watumishi wa namna hiyo watachapa kazi kwa bidii, uadilifu, uaminifu na kupiga vita vitendo vyote vya rushwa na ubadhilifu wa mali za umma.

Serikali itaendelea kushirikiana na Taasisi za kidini kwa ajili ya maendeleo, ustawi na mafao ya watanzania wengi. Akizungumzia kuhusu harambee hiyo ambayo jumla ya sh. milioni 357.35 zilipatikana, Waziri Mkuu amesema ni sehemu ya utekelezaji wa Mkakati wa CCT wa miaka mitano (2017 – 2022) wenye lengo la kuiwezesha CCT kujitegemea kwa kuwa na vitega uchumi vyake ambavyo vitawawezesha kujiendesha kwa asilimia 80%. Waziri Mkuu ameipongeza CCT kwa kuanza kuchukua hatua za kujenga uwezo wa ndani wa kujitegemea kiuchumi kwani zinahitajika nguvu za pamoja katika kuhakikisha wanawahudumia Watanzania na kuwaletea maendeleo endelevu na fungamani. Kujizatiti kwa CCT katika kufikia malengo yake ya kujitegemea kiuchumi ni muhimu katika kutimiza kusudio na agizo la Mungu la kuwahudumia wahitaji ambao ni Watanzania, lakini pia wanajaziliza juhudi za Serikali katika wajibu wake wa kuwahudumia watanzania.

Waziri Mkuu amesema kwa msingi huo, Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za CCT na madhehebu mengine ya dini katika kuwahudumia Watanzania kupitia sekta za elimu, maji, afya na shughuli za ujasiriamali. Amesema suala la kujitegemea ndiyo msingi wa uongozi wa Rais Dkt. Magufuli wa kujenga uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025 na katika kufanikisha hilo, Serikali imeendelea kupunguza kiwango cha utegemezi. Amesema kiwango cha utegemezi kutoka kwa Washirika wa Maendeleo katika bajeti kimepungua kutoka asilimia 12.5% mwaka 2017/2018 hadi asilimia nane 2019/2020. Kuimarika huko kwa bajeti ya Tanzania kunakwenda sanjari na kuimarika kwa huduma za kijamii kama vile elimu, maji na kupungua kwa umaskini wa mahitaji muhimu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Canon Moses Matonya, amesema jumuiya hiyo imeanzisha mkakati wa kuwa na vitegauchumu vyake, kwa lengo la kuondokana na utegemezi wa fedha za ufadhili ambazo zimekuwa zikipungua mwaka hadi mwaka.

Waziri Mkuu Majaliwa

 

06 July 2019, 14:25