Tafuta

Umoja wa Mataifa unasema, katika kipindi cha Mwaka 2018 watoto 12, 000 wamefariki dunia katika vita na kinzani sehemu mbali mbali za dunia! Umoja wa Mataifa unasema, katika kipindi cha Mwaka 2018 watoto 12, 000 wamefariki dunia katika vita na kinzani sehemu mbali mbali za dunia! 

Umoja wa Mataifa: Watoto 12, 000 wamefariki dunia kwa vita & kinzani

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2018 watoto zaidi ya 12, 000 wameuwawa na wengine kupata ulemavu na majeraha ya kutisha kutokana na vita, kinzani na misigano ya kijamii na kisiasa sehemu mbali mbali za dunia. Lakini maeneo yaliyoathirika zaidi ni Afghanstan, Palestina, Siria na Yemen. Taarifa ya Usalama wa watoto katika maeneo ya vita!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, hivi karibuni aliyaelekeza mawazo yake nchini Yemen ambako watu wanateseka kutokana na vita, njaa, magonjwa na umaskini wa hali na kipato. Kilio cha watoto na wazazi wao, kinamfikia Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa mwaliko kwa viongozi wanaohusika pamoja na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kusimama kidete, ili kutekeleza mikataba ya kimataifa iliyotiwa sahihi pamoja na kuhakikisha kwamba, wananchi wanagawiwa chakula pamoja na kuendelea kujikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu katika sala iliyoungwa mkono na waamini waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, mjini Vatican wamewaombea watoto ambao wanateseka na kufa kwa baa la njaa na kiu ya kutisha; watoto wanaofariki mikononi mwa mama zao pasi na huduma bora ya afya; hawa ni watoto wanaonyemelewa na kifo wakati wowote ule! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka katika sala watoto hawa! Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2018 watoto zaidi ya 12, 000 wameuwawa na wengine kupata ulemavu na majeraha ya kutisha kutokana na vita, kinzani na misigano ya kijamii na kisiasa sehemu mbali mbali za dunia.

Lakini maeneo yaliyoathirika zaidi ni Afghanstan, Palestina, Siria na Yemen. Takwimu hizi zimetolewa hivi karibuni wakati Umoja wa Mataifa ulipokuwa unajadili kuhusu usalama wa watoto wadogo katika maeneo ya vita sehemu mbali mbali za dunia. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antònio Guterres ameonesha masikitiko yake makubwa kutokana na vifo vya watoto wadogo katika maeneo ya vita. Idadi ya watoto waliofariki dunia kutokana na vita kwa Mwaka 2018 imeonesha kiwango cha juu kabisa kuwahi kutokea tangu mwaka 2005, mwanzo wa Umoja wa Mataifa kuanza kukusanya taarifa za ulinzi na usalama wa watoto katika maeneo ya vita.

Umoja wa Mataifa unasikitika kusema kwamba, kuna idadi kubwa ya watoto wadogo wanaopelekwa mstari wa mbele kama chambo wakati wa vita na mipasuko ya kijamii. Baadhi ya watoto wametumbukizwa katika nyanyaso na dhuluma za kijinsia. Baadhi ya watoto wametekwa nyara na wengine kupotea katika mazingira tatanishi. Afghanstan inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya watoto waliouwawa kutokana na mashambulizi ya kivita. Mashambulizi ya kivita nchini Siria yamepelekea watoto zaidi ya 1, 854 kufariki dunia na wengine kupata vilema na majeraha ya kudumu.

Umoja wa Mataifa
31 July 2019, 11:30