Cerca

Vatican News
Ufaransa imeanza kutekeleza Makubaliano ya Mkutano wa COP21 kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kutokana na athari kubwa zinazoendelea kujitokeza duniani! Ufaransa imeanza kutekeleza Makubaliano ya Mkutano wa COP21 kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi kutokana na athari kubwa zinazoendelea kujitokeza duniani!  (AFP or licensors)

Ufaransa yaanza utekelezaji wa Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi

Makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika nchini Ufaransa yanapaswa kutekelezwa kwa dhati, ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na kuongezeka kwa hewa ya ukaa na joto duniani. Ufaransa imeanza kutekeleza makubaliano hayo kwa kupunguza hewa ya ukaa, ifikapo mwaka 2020.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani linalohatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ni kati ya changamoto kubwa zinazovaliwa njuga kwa sasa na Umoja wa Mataifa. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatishia sana maisha ya watu wengi duniani: magonjwa ya mlipuko, umaskini na maafa makubwa kwa watu na mali zao.  Kumbe, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015.

Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha mkataba mpya wa Paris ambao umeweka historia mpya kwa nchi 195 kukubali kushirikiana katika kushughulikia athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kupitisha mkataba mpya wa kisheria unaozijumuisha nchi zote katika kupunguza gesi joto duniani. Makubaliano haya yanatoa taswira, mwelekeo, na malengo ambayo nchi zote duniani zitashiriki katika kupunguza gesi joto ili kufikia lengo la dunia la kutokuongezeka kwa wastani wa joto la dunia kwa zaidi ya nyuzi 20C au 1.50C. Hatua hii ni muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri nchi changa duniani hasa katika sekta muhimu zinazochangia ukuaji wa uchumi, ustawi na maendeleo ya wengi kama vile: kilimo, mifugo, uvuvi na utalii.

Greta Thunberg ni msichana mwenye umri wa miaka 16 ambaye  kwa siku za hivi karibuni ameibuka kuwa kweli ni mwanaharakati mahiri wa mazingira kutoka Sweden anaendelea kujipambanua katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwa kuwahamasisha vijana wa kizazi kipya, kusimama kidete, ili kuwashinikiza wanasayansi, wanasiasa na watunga sera za kitaifa na kimataifa kutoa kipaumbele cha kwanza katika utunzaji bora wa mazingira. Bado kuna uwezekano wa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa kama kutakuwepo na utashi wa kisiasa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yakipewa kipaumbele cha kwanza badala ya kujikita katika utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko!

Harakari za utunzaji bora wa mazingira zinazofanywa na mtandao wa vijana wa kizazi kipya zimekwisha kutikisa mataifa kadhaa duniani. Ni katika muktadha huu, Cèlia Blauel, Mkurugenzi wa Mazingira nchini Ufaransa ametamka kwamba, makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi, Cop21 uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa yanapaswa kutekelezwa kwa dhati, ili kupambana kufa na kupona na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazotokana na kuongezeka kwa hewa ya ukaa na joto duniani. Serikali ya Ufaransa imeanza kutekeleza makubaliano hayo kwa kuhakikisha kwamba, inapunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kutoka katika vyombo vya usafiri na kwamba, kuanzia mwaka 2020 Makampuni ya Ndege yatakuwa yanalipia kodi ya mazingira!

Mazingira

 

11 July 2019, 14:54