Tafuta

Vatican News
Taarifa ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani kwa Mwaka 2019: Kuna watu zaidi ya milioni 820 wanashambuliwa na baa la njaa duniani pamoja na utapiamlo wa kutisha! Taarifa ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani kwa Mwaka 2019: Kuna watu zaidi ya milioni 820 wanashambuliwa na baa la njaa duniani pamoja na utapiamlo wa kutisha!  (AFP or licensors)

UN: Hali ya Usalama wa Chakula & Lishe Duniani 2019: Baa la njaa

Taarifa ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani kwa Mwaka 2019 iliyotolewa kwa pamoja na Mashirika ya UN inaonesha kwamba, kwa muda wa miaka mitatu mfululizo baa la njaa duniani inaendelea kupekenya watu zaidi ya milioni 820, ambao hawana uhakika wa usalama wa chakula na lishe bora. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wenye unene wa kupindukia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa imejiwekea Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Malengo hayo ni pamoja na: 1. Kutokomeza umaskini, 2. Kukomesha baa la njaa, 3. Kuboresha afya njema na ustawi, 4. Elimu bora, 5. Usawa wa kijinsia, 6. Maji safi na salama. 7. Nishati mbadala kwa gharama nafuu, 8. Kazi zenye staha na ukuzaji uchumi, 9. Viwanda, ubunifu na miundombinu, 10. Kupunguza tofauti, 11. Miji na jamii endelevu, 12. Matumizi na uzalishaji wenye uwajibikaji, 13. Kuchukua hatua madhubuti dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, 14. Kuendeleza uhai katika maji, 15. Kulinda uhai katika ardhi, 16. Amani, haki na taasisi madhubuti, na hatimaye, 17. Ushirikiano ili kufanikisha malengo haya yaliyobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa. Lengo la Pili linapania pamoja na mambo mengine kupambana na baa la njaa, kuwa na Usalama wa Chakula, kuboresha hali ya lishe na kukuza kilimo endelevu.

Lengo hili linadhamiria kutokomeza na kumaliza kabisa baa la njaa kwa kusisitiza upatikanaji wa chakula cha uhakika, utolewaji wa lishe bora, huku likihimiza kukuza kilimo endelevu. Linaendelea kubainisha njaa kama tatizo linalopaswa kuondolewa kwa kushughulikiwa kikamilifu ili kuhakikisha kila kaya inakuwa na uhakika wa kupata chakula salama na cha kutosha ambacho kina virutubisho vyote. Lengo hili linadhamiria pia hadi kufikia mwaka 2030, kilimo kiwe kimeboreshwa kwa kuhakikisha wakulima wanatumia zana za kisasa na bora, urutubishaji wa ardhi inayotumika kwa ajili ya kilimo, na kuongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi na majanga asilia kama vile: mafuriko, ukame, na ndege waharibifu. Hii itasaidia kukuza uzalishaji wa mazao na hivyo kutokomeza kabisa balaa la njaa duniani.

Ili kuhakikisha lengo hili linafanikiwa kikamilifu, ni wajibu wa serikali na mamlaka zote zinazohusika kuhakikisha wanaweka jitihada kwenye kuongeza uzalishaji katika sekta ya kilimo kwa kuhakikisha zana za kilimo ikiwa ni pamoja na pembejeo za kilimo, na viuatilifu vya wadudu wanaoshambulia mazao zinapatika kwa urahisi zaidi kwa wakulima. Taarifa ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani kwa Mwaka 2019 iliyotolewa kwa pamoja na Mashirika ya Umoja wa Mataifa yaani: Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, WHO, Shirika la Afya Duniani, WHO, Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani, WFP, pamoja na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo, (IFAD) inaonesha kwamba, kwa muda wa miaka mitatu mfululizo baa la njaa duniani linaendelea kupekenya watu zaidi ya milioni 820, ambao hawana uhakika wa usalama wa chakula na lishe bora.

Kwa upande mwingine, kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wenye unene wa kupindukia. Takwimu zinaonesha kwamba, watoto wanaozaliwa wakiwa na uzito mdogo wamefikia milioni 20. 5 sawa na mtoto mmoja kati ya watoto 7 wanaozaliwa duniani. Kuna watoto milioni 148.9 sawa na asilimia 21.9% ya watoto wote wenye umri chini ya miaka 5 wanaokabiliwa na kashfa ya utapiamlo wa kutisha. Hali hii inaonesha kwamba, jitihada za Umoja wa Mataifa kupambana na baa la njaa, kuwa na Usalama wa Chakula, kuboresha hali ya lishe na kukuza kilimo endelevu ifikapo mwaka 2030 zinaonekana kugonga mwamba. Kashfa ya baa la njaa duniani inaendelea pia kuchangiwa na changamoto kubwa ya ongezeko la watoto wenye uzito wa kupindukia, hali inayohitaji ushirikiano na mshikamano wa dhati kabisa kutoka kwenye Jumuiya ya Kimataifa ili kuweza kudhibiti hali hii.

Baa la njaa linongezeka sana duniani na hali ya uchumi kimataifa inaendelea kudidimia kila kukicha! Hali hii ni hatari sana kwani kumekuwepo na ongezeko la matabaka ya watu kulingana na kipato chao; kwani maskini wanaendelea kutopea katika umaskini wao, kiasi hata cha kushindwa kujikwamua kupata chakula na lishe bora! Sera na mbinu mkakati wa kupambana na baa la njaa duniani, ukosefu wa usalama wa chakula pamoja na lishe duni, walengwa wakuu wawe ni maskini na “akina yakhe, pangu pakavu tia mchuzi”. Mapambano ya baa la njaa Barani Afrika yanaendelea kidogo kidogo, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa kwa mwaka 2011. Kwa ufupi kabisa, Barani Afrika kuna watu milioni 256.1 wanaoteseka kwa baa la njaa. Barani Asia ni watu milioni 513.9, Amerika ya Kusini na Visiwa vyake kuna jumla ya watu milioni 42.5 . Idadi ya watu wasiokuwa na uhakika wa usalama wa chakula ni bilioni 2, sawa na asilimia 26%. Watoto wanaozaliwa wakiwa na uzito wa chini duniani wamefikia kiasi cha milioni 20.5 sawa na mtoto mmoja kati ya watoto saba duniani!

Baa la Njaa
16 July 2019, 09:54