Tafuta

Vatican News
Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela tarehe 18 Julai 2019: Haki, ustawi na maendeleo ya wengi! Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela tarehe 18 Julai 2019: Haki, ustawi na maendeleo ya wengi! 

Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela, 18 Julai 2019

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa mwaka 2019 yamekwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka 101 tangu alipozaliwa. Ni kiongozi anayeheshimika sana duniani kutokana na moyo wake wa kusamehe na kusahau. Alikuwa mstari wa mbele kukuza: umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu wote pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela yalianzishwa na Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2009 na kuanza kuadhimishwa rasmi tarehe 18 Julai 2010 kama njia ya kumuenzi Mzee Nelson Mandela aliyejisadaka kwa ajili ya kupigania uhuru, utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kukoleza na kudumisha demokrasia ya kweli inayowaambata wananchi wote wa Afrika ya Kusini. Ni kiongozi aliyesimama kidete, kupambana na utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini, vitendo ambavyo vilidhalilisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa mfano na sura ya Mwenyezi Mungu kwa muda wa miaka 67.Ndiyo maana kama sehemu ya kumbu kumbu ya mchango wake, watu wanahimizwa kutekeleza walau mambo mbali mbali kwa muda wa dakika 67 ili kusaidia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kwa mwaka 2019  yamekwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka 101 tangu alipozaliwa. Ni kiongozi anayeheshimika sana duniani kutokana na moyo wake wa kusamehe na kusahau, ili kuandika ukurasa wa umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu wote pasi na ubaguzi wa aina yoyote ile. Umoja, mshikamano na mafungamano ya kitaifa ni kati ya vipaumbele vya Mzee Madiba. Itakumbukwa kwamba, Mzee Nelson Mandela alizaliwa tarehe 18 Julai 1918. Aliwahi kufungwa kizuizini kwa muda wa miaka 27 na Utawala wa ubaguzi wa rangi Afrika ya Kusini.

Maadhimisho ya Mwaka 2019 yanahimiza zaidi haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Frsancisko katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kunako mwaka 2017 alisema, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuvuka mifumo yote ya ubaguzi, hali zote za kutovumiliana pamoja na udhalilishaji wa utu na heshima ya binadamu! Mfano wa Mzee Nelson Mandela usaidie kuleta ari na mwamko mpya kwa vijana wa kizazi kipya nchini Afrika ya Kusini, ili waweze kujikita zaidi katika kukuza na kudumisha, misingi ya haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama sera na mikakati yao ya kisiasa.

Nelson Mandela
19 July 2019, 11:25