Rais John Pombe Magufuli amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kuonesha uaminifu, uadilifu na uchaji wa Mungu kwa kurejesha dhahabu kg 35.34 na fedha taslimu! Rais John Pombe Magufuli amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kuonesha uaminifu, uadilifu na uchaji wa Mungu kwa kurejesha dhahabu kg 35.34 na fedha taslimu! 

Serikali ya Kenya yarejesha dhahabu kg 35.34 kwa Tanzania!

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, Jumatano tarehe 24 Julai 2019 amevipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya kwa kufanikiwa kukamata kilo 35.34 za dhahabu iliyokuwa imeibwa nchini Tanzania na hatimaye, kuirejesha tena kwa Serikali ya Tanzania. Serikali ya Kenya pia imerejesha fedha ya Tanzania iliyoibwa kunako mwaka 2004! Bado kuna watu waaminifu duniani!

Na Mwandishi maalum, Dar es Salaam.

Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania ameipongeza Serikali ya Kenya kwa maamuzi yake ya kuirejeshea dhahabu yenye uzito wa kilo 35.34 zilizotoroshwa kutoka nchini Tanzania na Wafanyabiashara wasio waaminifu kwa njia ya magendo kunako mwaka 2018. Akizungumza katika hafla ya kukabidhi dhahabu pamoja na fedha taslimu akiwa pamoja na ujumbe wa Mawaziri na Watendaji wa Serikali ya Kenya Jumatano, 24 Julai 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli amesema kitendo kilichofanywa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ni cha kizalendo na kimedhirisha urafiki na udugu wa kweli baina yake na Tanzania. Amesema kuwa Serikali ya Kenya kupitia vya vyombo ulinzi na usalama vimefanya kazi nzuri inayodhirisha ushirikiano uliopo  kati ya Tanzania na Kenya,  na ameeleza kuwa kama kusingekuwepo na ushirikiano huo dhahabu na pesa  hizo zilizokamatwa kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jommo Kenyatta nchini humo visingelejeshwa Tanzania.

“Tunaipongeza Serikali ya Kenya kupitia vyombo vya vyake vya ulinzi na usalama vilivyofanya kazi nzuri ya kukamata dhahabu kilo 35.34 iliyokuwa imeshavuka kwenye mipaka yetu, na tuwapongeze pia kwa kutunza pesa yetu ambayo ilibiwa Tanzania kwenye Benki ya NMB mwaka 2004, kwa kweli huu ni uaminifu mkubwa” amesema Rais Magufuli. Licha ya kuipongeza vyombo vya ulinzi na usalama vya Kenya, Rais Magufuli ameshangazwa na ukimya kutoka vyombo vya ulinzi na usalama vya Tanzania na hivyo kuvitaka kujitafakari kwa namna dhahabu hiyo ilivyoweza kukamatiwa nchini Kenya na sio Kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwanza ambapo watuhumiwa walitumia ndege ya Shirika la Ndege la ‘Precision Air’ kusafirishia mzigo huo. “Vyombo vyetu vya ulinzi vipo hapa lazima niviseme, dhahabu iliwezaje kufika Kenya tukashindwa kuwakamata watumiwa wakiwa bado kwenye uwanja wa Mwanza?

"Hapa lazima vyombo vyetu mjitafakari japo mnafanya kazi kubwa lakini ikiwezekana mkajifunze kwa wenzenu wawape mbinu walizozitumia katika hili” amesema Rais Magufuli. Katika hafla hiyo, Rais Magufuli pia alimpigia simu ya moja kwa moja Rais Uhuru Kenyatta na kutoa shukrani zake na kumdhibitishia kuwa amepokea mzigo huo na kumpongeza kwa ushirikiano wa Serikali yake kwa Watanzania, ambapo Rais Kenyatta akimuhakikishia Rais Magufuli ushirikiano wa kudumu ambao utachochea zaidi maendeleo kama walivyoahidi na kupewa mamlaka na wananchi. Naye mjumbe maalumu aliyemwakilisha Rais Kenyatta, Monica Juma ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Serikali ya Kenya amesema Serikali ya Kenya itaendeleza ushirikiano wake na Tanzania katika masuala ya ulinzi na usalama kwa kuwa ushirikiano huo utasaidia kukuza uchumi wa pande zote mbili.

Na kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Professa Palamagamba Kabudi amesema Kenya na Tanzania ni ndugu tokea enzi na enzi, hivyo Serikali Tanzania itahakikisha kuwa inaendelea kushirikiana na Kenya ili kufanya ushirikiano huo unaleta ustawi, maendeleo na manufaa kwa wananchi wa nchi hizi mbili!

25 July 2019, 11:46