Chombo kiichatwacho Apollo 11 kilitua mwezini pamoja na Neil Armstrong na wenzake Buzz Aldrin na Michael Collins kunako mwaka 1969 Chombo kiichatwacho Apollo 11 kilitua mwezini pamoja na Neil Armstrong na wenzake Buzz Aldrin na Michael Collins kunako mwaka 1969 

Miaka 50 tangu wanaanga na chombo Apollo-11 kutua mwezini!

Neil Armstrong,binadamu wa kwanza kufika mwezini alisema,sisi wakazi wa dunia ambao tunaweza kutatua matatizo ya sayari hii,tunaweza kutatua matatizo yatokanayo na kuishi kwenye sayari hii.Alitamka hayo mara baada ya kutembelea Umoja wa Mataifa wiki tatu baada ya safari yao hiyo ya kipekee.Jumamosi 20 Julai,Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 50 tangu wanaanga hao kutua mwezini 1969.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Jumamosi tarehe 20  Julai 2019 dunia inakumbuka miaka 50 tangu binadamu alipotua mwezini, ziara ilifanywa na wanaanga Neil Armstrong na wenzake Buzz Aldrin na Michael Collins. “Sisi wakazi wa dunia, ambao tunaweza kutatua matatizo ya sayari hii, tunaweza kutatua matatizo yatokanayo na kuishi kwenye sayari hii,” hii  ni kauli yake Neil Armstrong, binadamu wa kwanza kufika mwezini, kauli ambayo alitoa mara baada ya kutembelea Umoja wa Mataifa wiki tatu baada ya safari yao hiyo ya kipekee. Katika safari yake kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Armstrong, ambaye aliambatana na wanaanga wenzake waliosafiri na chombo kiitwacho Apollo-11 hadi mwezini.

Kila mmoja alishuhudia tukio la kipekee mwezini

“Hakuna mtu yeyote hapa ambaye hakushuhudia wanaanga hao wakitembea hatua za kipekee mwezini. Wakati huo, mamia kati yetu kupitia redio na televisheni tulishiriki katika tukio hili la kihistoria.”. “Chombo cha Apollo-11 kilifika salama mwezini na kurejea kwa mafanikio makubwa ardhini na kutudhihirishia kile ambacho binadamu anaweza kufanikisha kwa kutumia rasilimali zilizopo na teknolojia pindi binadamu hao wakishirikiana kwa maslahi ya binadamu wote,” Ni maneno ya Bwana U Than Katiku Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa wakati ule.

Zawadi kwa wanaanga waliotua mwezini

Wakati wa ziara yao kwenye Umoja wa Mataifa, wanaanga hao walikabidiwa zawadi ambayo ni bapa la kumbukumbu linalofanana na lile waliloacha mwezini likiwa na maneno: “Hapa, binadamu kutoka sayari ya dunia walitua mwezini Julai 1969 baada ya kuzaliwa kristo. Tumefika kwa amani kwa ajili  ya binadamu wote”. Kumbukumbu zingine ambazo zimehifadhiwa kwenye Umoja wa Mataifa zinazo husiania  na safari hiyo ni sampuli mfano wa mwamba wa  mwezi. Hii ilikuwa ni zawadi kutoka kwa Rais Richard Nixon wa Marekani, zawadi ambayo ilikabidhiwa tarehe 20 mwezi Julai mwaka 1970 wakati jamii ya kimataifa ilipoadhimisha mwaka mmoja tangu safari ya Apollo-11 mwezini. Wanaanga hao watatu Armstrong, Aldrin na Collins, walifika tena Umoja wa Mataifa na kushiriki kwenye hafla maalum ya kukabidhi jiwe hilo.

Rais wa Baraza Kuu kushiriki maadhimisho ya miaka 50 tangu Apollo-11 kutua mwezini

Hata hivyo Ijumaa tarehe  19 Julai 2019, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Bi María Fernanda Espinosa alikuwa mgeni rasmi kwenye tukio maalum la maadhimisho ya miaka 50 ya chombo cha Apollo-11 kutua mwezini, tukio ambalo limeandaliwa na kampuni ya Google. Katika tukio hilo, Bi. Espinosa ameungana na wanaanga wanawake kutoka shirika la anga za juu la Marekani, NASA, wajasiriamali, wataalamu wa tabianachi, wanaanga, vijana na wanachama wa chama cha masuala ya anga za juu cha New York, NYSA. Tukio hilo pia limeangazia jinsi ya kuchagiza ubunifu na ujasiriamali ambao unachochea zaidi wanawake kushiriki masuala ya anga za juu. Bi. Espinosa amekuwa mwamasishaji mkubwa wa kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika nyanja za sayansi, teknolojia, uhandishi na hesabu, STEM. Duniani kote, wanawake ni chini ya asilimia 30% ya watafiti wote na ni chini ya theluthi moja tu ya wanafunzi wanawake ambao huchagua masomo ya STEM wanapojiunga na elimu ya juu.

20 July 2019, 14:53