Tafuta

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesema, familia ya Mungu nchini Msumbiji inaendelea kujiandaa kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko Mwezi Septemba 2019. Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji amesema, familia ya Mungu nchini Msumbiji inaendelea kujiandaa kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko Mwezi Septemba 2019. 

Hija ya Kitume ya Papa Francisko Msumbiji! Matumaini, Amani & Upatanisho

Familia ya Mungu nchini Msumbiji inaendelea kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kumpokea na kumkaribisha Papa Francisko; hujaji wa matumaini, amani na upatanisho. Bara la Afrika kwa sasa lina kiu kubwa ya: haki, amani, upatanisho na matumaini ya kuweza kuanza upya na kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti pasi na kukata tamaa hasa baada ya matukio ya vita, ghasia na kinzani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican

Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, Jumanne tarehe 9 Julai 2019 ametembelea Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao makuu mjini Roma na kukutana na kuzungumza na muasisi wa Jumuiya hii Professa Andrea Riccardi, Rais wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Bwana Marco Ipagliazzo pamoja na viongozi kadhaa. Kwa hakika, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imekuwa ni nyumba ya amani kwa familia ya Mungu kutoka Msumbiji, iliyosaidia FRELIMO na RENAMO kuwekeana sahihi Mkataba wa Amani kunako mwaka 1992 na huo ukawa ni mwanzo wa hija ya amani nchini Msumbiji. Kwa hakika bado kuna changamoto ya kuhakikisha kwamba, amani ambalo ni jina jipya la maendeleo fungamani ya binadamu inadumishwa nchini Msumbiji, lakini hatua kubwa imekwisha kutekelezwa hadi sasa!

Rais Filipe Nyusi, amewaalika waandishi wa habari kuweka kumbukumbu ya kudumu na endelevu ya mchango wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Msumbiji. Kimsingi, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imekuwa ni mpatanishi katika mchakato wa haki, amani na upatanisho wa kitaifa nchini Msumbiji.Tangu Mwaka 2002, Jumuiya ya Mtakatifu Egidio imeendesha kampeni inayojulikana kama “The Dream” yaani “Ndoto” kwa ajili ya kusaidia kutoa tiba kwa wagonjwa wa Ukimwi hasa Msumbiji, Malawi, Tanzania, Guinea Conakry, Kenya, Angola, Guinea Bissau, Nigeria, DRC, Cameroon na baadhi ya Nchi za Kiafrika ambazo zinaendelea kufanyiwa tathmini. Jitihada hizi zinawezesha kudhibiti maambukizi ya ugonjwa wa Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, pamoja na kuzisaidia familia ambazo zimeathirika kwa Ukimwi.

Familia ya Mungu nchini Msumbiji anasema Rais Nyusi imefaidika sana na huduma hii, kiasi cha kusaidia kudhibiti maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto. Rais Nyusi anasema, Familia ya Mungu nchini Msumbiji inaendelea kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko; hujaji wa amani na mhudumu wa furaha ya Injili. Bara la Afrika kwa sasa lina kiu kubwa ya: haki, amani, upatanisho na matumaini ya kuweza kuanza upya na kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti pasi na kukata tamaa hasa baada ya matukio ya vita, ghasia, kinzani na majanga asilia ambayo yamelikumba Bara la Afrika kwa miaka ya hivi karibuni! Hija ya Baba Mtakatifu Francisko inapania kuimarisha: amani na matumaini!

Akiwa Msumbiji, Baba Mtakatifu atatembelea pia Mradi wa Dream uliopo Zimpeto, nje kidogo ya mji wa Maputo, mahali pa mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa wagonjwa wa UKIMWI! Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 kwa kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji, Kimbunga Idai kimesababisha uharibifu mkubwa katika baadhi ya maeneo nchini Msumbiji, Malawi na Zimbabwe katika kile ambacho Umoja wa mataifa unasema huenda ni janga baya zaidi kama matokeo ya athari za mabadiliko ya tabianchi kuwahi kushuhudiwa kusini mwa Afrika.

Kimbunga cha Idai kimesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Watu milioni 1.7 wameathiriwa na janga hilo nchini Msumbiji na wengine 920,000 nchini Malawi. Rais Nyusi ametumia fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza vijana wa Msumbiji waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa waathirika. Amewapongeza na kuwashukuru pia wahisani mbali mbali waliochangia kuokoa maisha ya watu wa Mungu nchini Msumbiji. Serikali ya Msumbiji, inaendelea kujizatiti katika mchakato wa ujenzi wa Beira mpya! Kila jambo linawezekana! Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kunako mwaka 2018 imeadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya alisema karama ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inafumbatwa katika: Sala, Maskini na Amani; karama ambayo imeendelea kukua na kukomaa katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita.

Changamoto iliyoko mbele yake kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, wanaiwekeza ili iweze kuzaa matunda mengi zaidi ili kung’oa hofu, mashaka na hasira dhidi ya wahamiaji na wageni, maskini na watu ambao wanaotofautiana nao kwa sababu mbali mbali. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iwe ni mahali pa kukuza na kudumisha karama hizi kwa ajili ya kuendeleza Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo! Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iwe ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano na katika maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayowatenga na kuwanyanyasa maskini; na kwamba, kwa sasa tofauti kati ya watu inakuwa ni chanzo cha kinzani na uhasama. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi.

Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma; wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa binadamu, kati ya watu wa mataifa, familia na tamaduni zao. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iendelee kushikamana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapatia nafasi ya kwenda katika shule ya amani! Wawe karibu sana na wazee wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, lakini kwao wawe ni marafiki bila kusawahau waathirika wa vita, njaa na magonjwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maskini wawe ni amana na utajiri wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, kwani wote ni wa Kristo, dira na mwongozo wa kuyaangalia ya mbeleni kwa ari na moyo mkuu, wakijitahidi kudumu katika sala, huduma kwa maskini pamoja na kutafuta ili hatimaye kuendeleza amani duniani! Kwa mtindo huu wa maisha, kwa hakika, Mwenyezi Mungu ataendelea kuambatana nao katika hija ya maisha yao!

Papa: Msumbiji



09 July 2019, 15:43