Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 13 Juni 2019 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Unyanyapaa Dhidi ya Walemavu wa Ngozi: Kauli mbiu " Bado Nimesimama Imara" Jumuiya ya Kimataifa tarehe 13 Juni 2019 inaadhimisha Siku ya Kupambana na Unyanyapaa Dhidi ya Walemavu wa Ngozi: Kauli mbiu " Bado Nimesimama Imara" 

Siku ya Kimataifa ya Walemavu wa Ngozi, 2019: Mshikamano!

Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2013 ulianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Unyanyapaa dhidi ya walemavu wa ngozi “Albino” sehemu mbali mbali za dunia. Umoja wa Mataifa unasema kwamba, hawa ni watu wanaobaguliwa, wanaoteswa na kuuwawa kikatili kutokana na kushamiri kwa imani za kishirikina, hali ambayo inachangiwa pia na elimu duni pamoja na umaskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Siku ya Kupambana na unyanyapaa dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi kwa mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Bado nimesimama imara na waswahili “wangechombeza kwa kusema, “Bado niko ngangari, nimesimama kama mkuki wa kimasai”. Siku hii inaadhimishwa tarehe 13 Juni 2019. Kauli mbiu hii imechaguliwa ili kutambua, kuadhimisha na kuwatia moyo watu wenye ulemavu wa ngozi kuendelea kusimama imara, “kamili gado” hata kama bado kuna changamoto mbali mbali wanazoendelea kukumbana nazo katika maisha yao.

Hili ni kundi la watu wanaobaguliwa, kunyanyaswa, kuteswa na hata kuuwawa kikatili. Wanakabiliwa na changamoto ya kupata matibabu muafaka, elimu makini na wakati mwingine, wanapotea katika mazingira ya kutatanisha. Licha ya mambo yote haya, bado kuna haja ya kusema, wanaendelea kusimama imara! Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, haki zao msingi zinasimamiwa na kudumishwa na wote. Itakumbukwa kwamba, Umoja wa Mataifa kunako mwaka 2013 ulianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Unyanyapaa dhidi ya walemavu wa ngozi “Albino” sehemu mbali mbali za dunia.

Umoja wa Mataifa unasema kwamba, hawa ni watu wanaobaguliwa, wanaoteswa na kuuwawa kikatili kutokana na kushamiri kwa imani za kishirikina, hali ambayo inachangiwa pia na elimu duni pamoja na umaskini. Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi, teknolojia na tiba ya binadamu, lakini bado kuna watu wana aamini kwamba, baadhi ya viungo vya walemavu wa ngozi vinaweza kutibu magonjwa na hata wakati mwingine kuleta utajiri wa chapuchapu! Matokeo yake, kumekuwepo na wimbi kubwa la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi, “Albino”.

Wanasiasa hasa nyakati za kampeni za kuwania uongozi pamoja na wafanyabiashara ni kati ya watu wanaotuhumiwa kujihusisha sana na utekaji na mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi. Walemavu wa ngozi,  wanakabiliwa na wimbi la umasikini ambapo wengi wao hawajapata elimu na hivyo kuwa na maisha magumu lakini pia kutojua mbinu za kujiinua kiuchumi kutokana na jamii kuwaona kana kwamba hawana uwezo wa kufanya shughuli mbalimbali lakini hii ni dhana potofu ambayo imepitwa na wakati! Walemavu wa ngozi wanapaswa kulindwa, kuwezeshwa kielemu pamoja na kujengewa uwezo wa kiuchumi na kiafya ili kupambana na hali zao.

Walemavu Ngozi
13 June 2019, 15:44