Ripoti mpya ya UN inasema:umri wa mwanamke kuolewa umeongezeka duniani kote na viwango vya uzazi vimeshuka  wakati wanawake wanazidisha kuwa na nguvu kiuchumi Ripoti mpya ya UN inasema:umri wa mwanamke kuolewa umeongezeka duniani kote na viwango vya uzazi vimeshuka wakati wanawake wanazidisha kuwa na nguvu kiuchumi 

Ripoti kuhusu maendeleo ya Wanawake 2019-2020:Familia katika ulimwengu unaobadilika

Kwa mujibu wa Ripoti mpya iliyotolewa tarehe 25 Juni 2019 na Umoja wa Mataifa kuhusu mienendo ya maendeleo ya wanawake duniani bila kusahau familia inathibitisha kuwa umri wa mwanamke kuolewa umeongezeka duniani kote na viwango vya uzazi vimeshuka huku wanawake wakizidisha kuwa na nguvu kiuchumi.

Na Sr. Angela Rwezaula –Vatican

Tarehe 25 Juni 2019 Umoja wa Mataifa kuhusu mienendo ya maendeleo ya wanawake duniani bila kusahau familia imetoa ripoti mpya inayothibitisha kuwa umri wa mwanamke kuolewa umeongezeka duniani kote na viwango vya uzazi vimeshuka huku wanawake wakizidisha  kuwa na nguvu kiuchumi. Ripoti iliyopewa jina Maendeleo ya Wanawake 2019-2020: Familia katika ulimwengu unaobadilika, imeandaliwa na shirika linaloshughulikia masuala ya wanawake la Umoja wa Mataifa,  (UN-Women) ambapo imesema kuwa kwa ujumla, theluthi moja ya kaya ni za wanandoa wanaoishi na familia, huku familia zinazojumuisha ndugu na jamaa ni asilimia 27, wakati idadi kubwa ya asilimia 8 ya kaya za mzazi mmoja zinaongozwa na wanawake. Ripoti imesema kuwa  familia hizo za mzazi mmoja zinazo ongozwa na wanawake ni wale ambao wanahaha kimaisha  huku na kule wakibadili kazi moja au nyingine, wakilea watoto na kufanya kazi za ndani bila malipo! Familia za wanandoa wa jinsia moja nazo pia zinaongezeka kwenye kanda zote za dunia kwa mujibu wa ripoti mpya.

Familia inaweakana ikawa chanzo cha ukatili wa ndani

Ripoti ikiendelea kuchambua kwamba familia kama taasisi inayotambuliwa kuwa ni sehemu ya malezi, inathibitishwa kuwa kuwa familia imebainika kuwa inaweza kuwa chanzo cha mizozano, ukosefu wa usawa na ghasia na mambo mengine. Leo hii, wanawake na wasichana bilioni 3 wanaishi kwenye nchi ambazo ubakaji ndani ya ndoa bado haujaharamishwa wazi, imesema ripoti hiyo huku ikongeza kuwa ukosefu wa wa haki na ukiukwaji mwingine wa haki unafanyika kwa njia nyingine. Kwa kusisitizia zaidi wametoa mfano wa masuala ya mirathi ambako katika nchi 1 kati ya 5 haki za mirathi kwa wavulana na wasichana ni tofauti, ambapo wavulana wana haki zaidi. Halikadhalika katika mataifa 19 wanawake kisheria wanatakiwa kuheshimu waume zao, ambapo takribani theluthi moja ya wanawake walioolewa katika nchi zinazoendelea wameripoti kuwa wana sauti ndogo au hawana sauti kabisa juu ya afya zao wenyewe.

Ufinyu wa fursa za ajira kwa wanawake walioolewa

Kwa kutazama hali halisi za ajira, Ripoti inasema kuwa, wanawake wanaendelea kuingia kwenye soko la ajira kwa kiasi kikubwa, japokuwa ndoa na uzazi vinakwamisha ushiriki wao wa kina sambamba na kupata kipato sahihi. Takwimu zinaonesha kuwa, duniani, zaidi ya nusu ya wanawake walioolewa wenye umri kati ya miaka 25 na 54 wako kwenye soko la ajira ikilinganishwa na theluthi mbili za wanawake ambao hawajaolewa na asilimia 96 ya wanaume waliooa. Ripoti inasema kuwa kichocheo kikubwa cha ukosefu huo wa usawa ni suala kwamba, “wanawake wanaendelea kufanya zisizo na malipo za malezi mara tatu zaidi na kazi za ndani kuliko wanaume kutokana na kutokuwepo kwa huduma nafuu za uangalizi au malezi. Hata hivyo ripoti imeangazia maendeleo kwenye likizo za uzazi kwa wanaume hususan katika mataifa ambayo yametenga likizo ya uzazi kwa wanaume. Kizingiti kingine kwa wanawake ni pale ambapo wanataka kuhama ambapo ruhusa inakuwa inatoka kwa mumewe na hivyo kumkwamisha katika harakati iwapo anataka kukimbia ghasia au kusaka ajira bora zaidi.

Je kufanyike nini kwa ajili ya mwelekeo bora

Ili kuondokana na vikwazo vya sasa ripoti ina mapendekezo mengi  kwa watunga sera, wanaharakati na watu wote ili kubadili familia ziwe na msingi wa usawa na haki ambamo kwao mwanamke anaweza kuwa na sauti, chaguo na usalama wa kimwili na kiuchumi. Miongoni mwao ni kubadilisha na kurekebisha sheria za familia ili kuhakikisha wanawake wanaweza kuchagua aolewe na nani na kwa wakati gani na pia kuweka fursa ya talaka iwapo itahitajika kufanya hivyo. Pendekezo lingine ni kuwekeza kwenye huduma za umma hususan elimu na afya ya uzazi ili wanawake na wasichana waweze kuwa na fursa ya kuchagua ni lini anataka kuwa na mtoto. Suala pia la likizo ya uzazi yenye malipo limependekezwa na serikali zisaidia malezi kwa watoto na wazee kama njia mojawapo ya kusaidia familia na kupanua wigo wa fursa kwa wanawake. Pendekezo lingine ni kuhakikisha kuna sheria zinazotekelezwa za kulinda usalama wa mwanamke dhidi ya aina zote za ukatili na kuwapatia haki na msaada pindi anapokabiliwa na ghasia hizo.

26 June 2019, 15:43