Tafuta

Taadhali ya mlipuko wa Ebola nchini Uganda baada ya kuthibitishwa vifo vya watu watatu katika Kituo cha Ebola cha Kasese Taadhali ya mlipuko wa Ebola nchini Uganda baada ya kuthibitishwa vifo vya watu watatu katika Kituo cha Ebola cha Kasese  

Dharura ya Ebola Uganda:Vifo vya watu watatu vimethibitiswa katika kituo cha Ebola Kasese

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limezindua mkakati kwa kukabiliana na Ebola nchini Uganda kufuatia kuthibitishwa kwa visa vitatu ikiwemo vifo viwili Magharibi ya nchi hiyo.Mpango huo umetangazwa siku mbili tu baada ya wizara ya afya ya Uganda na shirika la afya duniani kuthibitisha mlipuko wa Ebola katika kituo cha matibabu ya Ebola cha Kasese.

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limezindua mkakati kwa kukabiliana na Ebola nchini Uganda kufuatia kuthibitishwa kwa visa vitatu ikiwemo vifo viwili Magharibi ya nchi hiyo. Mpango huo wa UNICEF umetangazwa siku mbili tu baada ya wizara ya afya ya Uganda na shirika la afya duniani kuthibitisha mlipuko wa Ebola uliosababisha vifo viwili vya mtoto wa miaka 5 na bibi yake kwenye kituo cha matibabu ya Ebola cha Kasese, walioingia Uganda kutokea nchi jirani ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo DRC ambako mlipuko wa Ebola unaendelea.

Eneo la Kasese nchini Uganda kuna jumla ya watoto laki nne

Eneo hilo la Kasese kwa mujibu wa UNICEF lina jumla ya watoto 400,000 na shirika hilo baada ya maandalizi ya miezi kadhaa sasa inaingia katika hatua ya kukabiliana na ugonjwa huo. Akizungumzia umuhimu wa mipango thabiti ya kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo, mwakilishi wa UNICEF nchini Uganda Dk. Doreen Mulenga amesema “wakati fikra na sala zetu zikiwa pamoja na familia ya kijana aliyepoteza maisha pamoja na bibi yake, hii ni kumbusho kwamba hata kisa kimoja tu cha Ebola ni angalisho kubwa.Tunapaswa kufanya kila liwezekanalo kuzuia mlipuko huu kusambaa na kuzia vifo Zaidi. UNICEF inazidisha juhudi zake na kupunguza uwezekano wa athari kubwa zaidi za mlipuko huu kwa Watoto na jamii nchini Uganda.” Katika miezi kadhaa iliyopita UNICEF imekuwa ikiisaidia serikali ya Uganda katika utekelezaji wa program mbalimbali za kuhakikisha jamii katika wilaya za Magharibi mwa Uganda zinazopakana na DRC zimejiandaa na uwezekano wa mlipuko wowote wa Ebola.

Msaada wa UNICEF katika jitihada za kupambana na Ebola

Msaada wa UNICEF katika juhudi hizo ni pamoja na kutembelea kaya zaidi ya 350,000 na kuwafikishia taarifa muafaka za kuzuia na kuchukua hatua haraka dhidi ya Ebola, kufanya mikutano zaidi ya 14,000 mashuleni, makanisani, misikitini, masokoni, kwenye vituo vya taxi, vituo vya boba-boda na mabasi, lakini pia kwenye mikusanyiko kama ya mazishi ili kujadiliana nao njia za kuzuia na jinsi ya kuchukua hatua za haraka kusaka huduma za afya . Mkakati huu umewafikia watu takriban milioni 2.4. Mbali ya hayo UNICEF imekuwa ikisambaza maji, masuala ya usafi na vifaa vya usafi katika vituo zaidi ya 500 vya afya , kwa shule zaidi ya 1000 na vituo vya mpakani zaidi ya 60. Pia shirika hilo la watoto duniani limekuwa lijenga uwezo kwa ajili ya kuzuia na kudhibiti maambukizi katika vituo vya afya kupitia maji, usafi na  usimamizi na mafunzo kwa wafanyakazi wa vituo vya afya kwa madhumuni ya kuzia ugonjwa wa Ebola.

UNICEF imetoa mafunzo hata kwa wafanyakazi wa kujitolea karibia 1500

UNICEF imetoa mafunzo pia kwa wafanyakazi wa kujitolea karibu 1,500 wa chama cha msalaba mwekundu nchini Uganda kwa ajili ya kuzisaidia jamii zilizoathirika kukabiliana na changamoto zitokanazo na Ebola. Bi. Mulenga amesema “uelewa ni njia bora ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya Ebola. Kutoa elimu muafaka na mambo ya kuzingatia kwa jamii na miongoni mwa mambo UNICEF inayoyafanya ni kusaidia kikamilifu katika hilo.” UNICEF inahitaji dola milioni 3.9 ili kusaidia juhudi za serikali ya Uganda katika kukabiliana na Ebola hususani katika kutoa elimu kuhusu hatari na kuhamasisha jamii, masuala ya maji, usafi, lishe kwa Watoto na msaada wa kisaikolojia kwa Watoto na familia zao.

15 June 2019, 15:39