Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei inaadhimisha Siku ya Umoja wa Afrika! Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei inaadhimisha Siku ya Umoja wa Afrika! 

Siku ya Umoja wa Afrika: 25 Mei 2019: Afya Bora Inarefusha maisha!

Maadhimisho ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Afya Bora ina refusha maisha”. Mada hii inapania kulinda na kudumisha maisha, ili kukabiliana na vifo vya watoto wadogo Barani Afrika pamoja na kuendeleza misingi ya haki, amani na maridhiano Barani Afrika. Haya ni mambo msingi yanayofumbatwa katika maendeleo fungamani ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 25 Mei, inaadhimisha Siku ya Umoja wa Afrika, kumbu kumbu endelevu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika, OAU kunako mwaka tarehe 25 Mei 1963 huko mjini Addis Ababa, nchini Ethiopia. Kunako tarehe 11 Julai 2001, Mkutano mkuu wa OAU uliamua kuunda Umoja wa Afrika kama sehemu ya mbinu mkakati wa kukuza na kudumisha Umoja na mshikamano miongoni mwa nchi za Kiafrika na tarehe 9 Julai 2002, Umoja wa Afrika ukazaliwa rasmi!

Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika ulikuwa na jukumu la kupambana na ukoloni, mifumo ya ubaguzi wa rangi, vita, njaa na umaskini, uliokuwa unadhalilisha utu, heshima na haki msingi za watu wa familia ya Mungu Barani Afrika. Umoja wa Afrika unataka kukuza na kudumisha umoja na mshikamano katika medani mbali mbali za maisha ya watu Barani Afrika: kiuchumi, kijamii, kisiasa na kitamaduni ili kuondokana na ukoloni mamboleo pamoja na ukoloni wa kiitikadi na utamaduni wa kifo, unaofumbatwa mara nyingi kwenye masharti ya misaada kwa Bara la Afrika.

Maadhimisho ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2019 yanaongozwa na kauli mbiu “Afya Bora ina refusha maisha”. Mada hii inapania kulinda na kudumisha maisha, ili kukabiliana na vifo vya watoto wadogo Barani Afrika pamoja na kuendeleza misingi ya haki, amani na maridhiano Barani Afrika. Haya ni mambo msingi yanayofumbatwa katika maendeleo fungamani ya binadamu. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na kuwajengea uwezo wanawake na vijana Barani Afrika, ili waweze kushiriki kikamilifu katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe wasiwe ni watazamaji tu!

Siku ya Umoja wa Afrika inapaswa kuwa ni kielelezo cha utambulisho wa familia ya Mungu Barani Afrika katika umoja na utofauti wake! Licha ya changamoto mbali mbali zinazoendelea kulikumba Bara la Afrika katika ujumla wake, lakini pia kuna haja ya kutangaza na kuonesha mazuri yanayopatikana Barani Afrika. Baba Mtakatifu Francisko tarehe 30 Novemba 2015 alizindua kwa mara ya kwanza maadhimisho ya Jubilei ya Huruma ya Mungu, kwenye Jimbo kuu la Bangui, nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Huu ni mwaliko wa kuliangalia Bara la Afrika pasi na kuwa na maamuzi mbele!

Umoja wa Afrika
25 May 2019, 13:27