Tafuta

Vatican News
Rais Sergio Mattarella wa Italia, hivi karibuni amefanya mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na Vatican: Amekazia: Utu, Haki, Amani na Mshikamano wa Kidugu Rais Sergio Mattarella wa Italia, hivi karibuni amefanya mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na Vatican: Amekazia: Utu, Haki, Amani na Mshikamano wa Kidugu  (ANSA)

Yaliyojiri Katika Mahojiano Maalum na Rais Mattarella wa Italia

Rais Sergio Mattarella wa Italia anasema: Umefika wakati wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kuondokana na misimamo mikali ya kiimani inayopelekea hali ya kutovumiliana na kushikamana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni msingi wa ujenzi wa amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Umoja wa Ulaya unapaswa kurejea tena katika misingi ya kuanzishwa kwake; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu. Umefika wakati wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kuondokana na misimamo mikali ya kiimani inayopelekea hali ya kutovumiliana, kuthaminiana na kushikamana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni msingi wa ujenzi wa amani duniani.

Kanisa bado linaendelea kuchangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo fungamani ya binadamu, licha ya changamoto nyingi linazo kabiliana nazo! Tasnia ya habari inao mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha haki, amani, demokrasia na mafungamano ya kijamii! Haya ni kati ya mambo mazito yaliyobainishwa hivi karibuni na Rais Sergio Mattarella wa Italia, katika mahojiano maalum na vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican. Katika miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na ongezeko kubwa la vitendo vya watu kutovumiliana, kuthaminiana wala kushikamana katika ngazi ya kimataifa.

Rais Sergio Mattarella anasema, matukio kama haya yamegusa na kuitikisa hata Italia, lakini, mwelekeo wa mshikamano na maridhiano kati ya watu bado unatawala! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wananchi wa Bara la Ulaya kurejea tena katika mawazo ya waasisi wa Umoja wa Ulaya kwa kutoa kipaumbele cha kwanza, kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Italia inapaswa kujisikia kuwa ni Jumuiya inayojikita katika tunu msingi za: umoja, upendo na mshikamano wa dhati ili kukabiliana na changamoto mamboleo, athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; ongezeko la pengo kati ya maskini na matajiri; ukosefu wa fursa za kazi na ajira pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Matokeo yake ni kuibuka kwa hofu na wasi wasi kuhusu ulinzi na usalama; ongezeko la umaskini wa hali na kipato; chuki na uhasama wa kisiasa; kiasi cha kukosa mvuto na mashiko kwa wananchi wanaowawakilisha. Rais Mattarella anakaza kusema, huu ni mwelekeo wa kimataifa unaopaswa kurekebishwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Uhusiano kati ya Kanisa na Serikali ya Italia ni mzuri na kwamba, Kanisa limekuwa na mchango mkubwa katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Familia ya Mungu nchini Italia, inaendelea kuonesha upendo wa pekee kwa Baba Mtakatifu Francisko anayejipambanua kwa kuwapenda na kuwajali maskini; haki na amani pamoja na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Kanisa limekuwa na mchango wa pekee katika huduma ya elimu na afya; ustawi na maendeleo ya wazee na maskini; wakimbizi na wahamiaji bila kuwasahau wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na sababu mbali mbali. Kwa njia hii, Kanisa limeendelea kuchangia katika mshikamano na mafungamano ya kijamii yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya kila siku! Majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali duniani ni changamoto pevu inayopaswa kuvaliwa njuga ili kujenga na kudumisha uhuru wa kuabudu na kidini; haki, amani, maridhiano na mshikamano wa dhati, vigezo msingi katika ujenzi wa udugu wa kibinadamu.

Haya ni mambo ambayo yamebainishwa kwenye Hati ya Udugu wa Kibinadamu iliyotiwa mkwaju kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari 2019, huko Abu Dhabi, kwenye Umoja wa Falme za Kiarabu. Hati hii ni muhimu sana katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki na amani duniani, ili kuondokana na misimamo mikali ya kidini na kiimani, ambayo imesababisha mashambulizi ya kigaidi kuendelea kusababisha majanga katika maisha ya watu pamoja na kuhatarisha mafungamano na mshikamano ya kijamii na kidini. Tofauti msingi zinazojionyesha miongoni mwa watu ziwe ni utajiri na amana ya upendo na mshikamano na wala si sababu ya chuki na uhasama kati ya watu wa Mataifa.

Majadiliano ya kidini yawe ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya watu kwa kushirikiana, kushikamana na kusaidiana kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake. Majadiliano na udugu ni chanda na pete katika ujenzi wa haki, amani na maridhiano. Serikali husika hazina budi kuhakikisha kwamba, zinaimarisha utawala wa sheria dhidi ya vitendo vya kigaidi, hali inayohitaji pia elimu na majiundo makini, ili kuwa na dhamiri nyofu! Umoja wa Ulaya unapaswa kufahamika kuwa ni Jumuiya inayosimikwa katika tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho na wala si masuala ya kiuchumi peke yake. Mawazo haya ni muhimu sana kwani ni msingi wa ujenzi wa Umoja wa Ulaya kama ulivyoasisiwa. Uhuru wa watu kutembea pasi na vikwazo; athari za Vita Kuu ya Kwanza na ya Pili ya Dunia. Vijana wanapaswa kuelimishwa kuhusu madhara ya Vita Baridi yaliyopelekea dunia kugawanyika katika mifumo ya kisiasa.

Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya uchoyo, ubinafsi na ubabe usiokuwa na tija wala mashiko katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Changamoto kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Bara la Ulaya ni kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za binadamu zinapewa kipaumbele cha kwanza! Umoja na mshikamano wa kidugu; usawa na maendeleo fungamani ya binadamu yapate umwilisho katika misingi ya maadili, utamaduni na ukuaji na maendeleo ya kiuchumi. Rais Sergio Mattarella anasema, kuna kiu kubwa ya Serikali ya Italia kuendelea kushirikiana na kushikamana na Mataifa mengine duniani katika masuala ya: kitamaduni, kisayansi, kisiasa, kiuchumi pamoja na ulinzi na usalama, ili kudumisha haki na amani duniani. Italia bado ina uwezo wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Rais Mattarella 2019
20 May 2019, 08:47