Tafuta

Vatican News
Rais Klaus Werner Iohannis wa Romania amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete katika kutetea: utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi! Rais Klaus Werner Iohannis wa Romania amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusimama kidete katika kutetea: utu, heshima, ustawi na mafao ya wengi!  (AFP or licensors)

Hija ya Kitume Romania: Hotuba ya Rais wa Romania

Romania inampongeza Papa Francisko kwa uongozi wake, ambao umejipambanua kwa kuweka msimamo sahihi kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Umoja wa Ulaya unataka kukuza na kudumisha: misingi ya haki, amani, demokrasia na umoja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Klaus Werner Iohannis wa Romania, Ijumaa tarehe 31 Mei 2019, katika hotuba yake ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini Romania, amegusia amana na urithi wa maisha ya kiroho kutoka kwa Mtume Andrea na kwamba, familia ya Mungu nchini Romania, imejiandaa vyema ili kumwonjesha upendo unaobubujika kutoka katika sakafu ya nyoyo zao. Huu ni upendo unaofumbata utajiri wa utamaduni na imani, hasa wakati huu, Kanisa linapo adhimisha mafumbo yake yaani: Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni na Pentekoste. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Romania anasema Rais Iohannis ni mwendelezo wa imani iliyooneshwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 9 Mei 1999, kwa kuitaka Romania kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Umoja wa Ulaya, kwa kutambua dhamana na wajibu wake wa kihistoria pamoja na kuimarisha umoja na mafungamano ya kijamii.

Romania inampongeza Baba Mtakatifu kwa uongozi wake, ambao umejipambanua kwa kuweka msimamo sahihi kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Umoja wa Ulaya unataka kukuza na kudumisha: misingi ya haki, amani, demokrasia, umoja mambo yanayokita mizizi yake katika uhuru na tunu msingi za maisha. Utawala wa mabavu hauna tena nafasi na kwamba, haki msingi za binadamu zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote. Mwaka 2020, Romania na Vatican, wataadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu nchi hizi mbili zilipoanzisha uhusiano wa kidiplomasia. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya uhusiano wa kidiplomasia na Vatican, kunako mwaka 2015, viongozi wa Romania walipata nafasi ya kutoa mwaliko kwa Baba Mtakatifu Francisko kutembelea Romania, ili kuimarisha zaidi mafungamano haya ya kidiplomasia.

Rais Klaus Werner Iohannis wa Romania anasema, Bara la Ulaya lina kiu ya haki, amani na maridhiano yanayofumbatwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama watoto wa Mungu; kwa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Romania ina makundi madogo madogo ya watu yapatayo 20 ambayo yanaendelea kuishi kwa amani na utulivu. Kuna waamini wa Kanisa la Kiorthodox na Kanisa Katoliki, wote hawa wanaishi kwa amani na upendo, kwa kusaidiana kama ndugu. Serikali iko mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini unaheshimiwa na kudumishwa na wote bila kusahau ukarimu unaoshuhudiwa na Kanisa Katoliki kwa wananchi wa Romania wanaoishi mbali na nchi yao!

Changamoto mamboleo ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inapambana na umaskini, uharibifu wa mazingira, ulaji wa kupindukia, vita na mipasuko. Kuna haja ya kuonesha mshikamano na huduma ya upendo kwa wakimbizi na wahamiaji na kila mtu akijitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake!

Rais Romania
31 May 2019, 18:39