Tafuta

Sekta ya utalii nchini Tanzania inaendelea kuwa ni kivutio kikubwa kwa wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia! Sekta ya utalii nchini Tanzania inaendelea kuwa ni kivutio kikubwa kwa wageni kutoka sehemu mbali mbali za dunia! 

Tanzania yaendelea kupeta katika sekta ya utalii Afrika Mashariki

Waziri Mkuu amewaomba watalii hao wapange muda wao na watafute fursa nyingine ya kuja Tanzania kutembelea mbuga nyingine za ukanda wa Kusini pamoja fukwe nzuri za Zanzibar. "Tumefarijika sana na ujio wenu na tunaamini mtaenda kutangaza mazuri mliyoyaona kwa wengine. Mbuga nyingine ni Ngorongoro, Ruaha, Selous, fukwe nzuri za Zanzibar na mlima Kilimanjaro,"

Na Mwandishi maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Dar es Salaam.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka watalii kutoka Israel wakawe mabalozi wazuri wa kuitangaza Tanzania pindi wakirudi huko kwao. Ametoa wito huo Jumamosi, Aprili 27, 2019 kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro (KIA) wakati akiwaaga watalii 274 walioondoka nchini Tanzania mchana kurejea kwao Israeli. Watalii hao ni miongoni mwa watalii 1,000 waliowasili nchini tangu Aprili 20, mwaka huu na kutembelea maeneo kadhaa ya vivutio kwenye ukanda wa Kaskazini.

Kundi la kwanza liliondoka Ijumaa usiku, la pili Jumamosi, la tatu limeondoka saa 10 jioni na la mwisho litaondoka saa 2 usiku.  Waziri Mkuu amewaomba watalii hao wapange muda wao na watafute fursa nyingine ya kuja Tanzania kutembelea mbuga nyingine za ukanda wa Kusini pamoja fukwe nzuri za Zanzibar.  "Tumefarijika sana na ujio wenu na tunaamini mtaenda kutangaza mazuri mliyoyaona kwa wengine. Tunazo mbuga nyingine za Rubondo, Katavi, Ngorongoro, Ruaha, Selous, fukwe nzuri za Zanzibar na mlima Kilimanjaro," amesema. Pia amewashukuru mawakala wa utalii nchini pamoja na Mkurugenzi wa kampuni wakala wa utalii ya Another World kutoka Israel Bw. Carmel Shlomo kwa kuamua kuitangaza Tanzania kama kivutio namba moja cha utalii barani Afrika. 

Kwa upande wake, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla aliwashukuru watalii hao kwa kuamua kuitembelea Tanzania licha ya kuwa wangeweza kwenda maeneo mengine yaliyo jirani na Israel. "Natambua uchovu mlionao sababu ya urefu wa safari kutoka Israel hadi hapa, lakini nawashukuru kwa uamuzi wenu wa kuja Tanzania katika kipindi hiki ambacho tunafanya maboresho kwenye sekta ya utalii ili tuweze kutoa huduma bora zaidi," alisema. Alisema Tanzania ina vivutio vingi vya utalii na hii inawezekana kwa sababu iliamua kutenga zaidi ya robo ya ardhi yake kwa ajili ya mbuga na hifadhi za taifa za wanyama. Pia alizishukuru kampuni za utalii za Tanzania na Israeli kwa kushirikiana kuleta watalii wengi kiasi hicho. Alizitaja kampuni hizo kuwa ni Excellent Guides, Mauly Tours and Safaris, Matembezi, Leopard Tours and Safaris, African Queen Adventures na TAWISA zote za kutoka Tanzania. Kamuni za kutoka Israeli ni Another World, My Trip, Camel na Safari Company.

Kwa upande wao, baadhi ya watalii kutoka Israel wamesema wamevutiwa na waliyaona hapa nchini na wameahidi kurudi tena ili watembelee vivutio vingine zaidi. Bibi Naomi Peer Moscovich na mabinti zake Dana na Lihi wamesema wamevutiwa na wingi wa wanyama waliowaona lakini pia wameguswa na ukarimu wa watu waliokutana nao.  "Tunaondoka na neno moja kubwa nalo ni kwamba hatutaisahau Tanzania" (we say Unforgettable Tanzania) na tutarudi tena hivi karibuni," alisema Dana Peer Moscovich ambaye ni dada yake Lihi.  Hafla ya kuwaaga watalii hao ilihudhuriwa pia na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii nchini, Jaji Thomas Mihayo, Katibu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Adolf Mkenda na Wakuu wa Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha, Mama Anna Mghwira na Bw. Mrisho Gambo. 

27 April 2019, 16:14