Unicef inaomba msaada kwa ajili ya watoto nchini Msumbiji baada ya kimbuga Idai wapate kurudi shuleni Unicef inaomba msaada kwa ajili ya watoto nchini Msumbiji baada ya kimbuga Idai wapate kurudi shuleni 

UNICEF:Zaidi ya watoto laki tatu nchini Msumbiji wanashindwa kwenda shule!

Unicef inasema kimbunga Idai kilichopiga Msumbiji mwezi Machi kimesababisha zaidi ya watoto 305,000 nchini humo kushindwa kuhudhuria shuleni na majengo 3,400 kuharibiwa.Kutokana na hiyo inawaomba wadau wake na watu wenye mapenzi mema kuwasaidia ili waweze kukidhi haja ya dharura kwa watoto hao.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Taarifa ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF iliyotolewa tarehe 20 Aprili 2019 mjini New York, Marekani na Beira Msumbiji imesema kimbunga Idai kilichopiga Msumbiji mwezi Machi kimesababisha zaidi ya watoto 305,000 nchini humo washindwe kuhudhuria shuleni na kama hiyo haitoshi vyumba 3,400 vya madarasa vimeharibiwa kabisa kwenye maeneo yaliyo kukumbwa na kimbunga hicho ikiwemo hata vyumba 2,713 jimboni Sofala pekee yake.

Unicef inaomba msaada kutoka kwa wadau wake ili kujenga shule imara

UNICEF inasema katika baadhi ya maeneo, ya shule zinahitajika ukarabati mkubwa kwasababu shule hizo, zilitumika kama makazi ya dharura kwa watoto na familia zao ambazo zilipoteza makazi. Katika kusisitiza  juu ya ujenzi na ukarabati ili uweze kuwa imara na kuhimili majanga ya asili siku za mbele, Unicef inawasihi wadau wa kibinadamu ili kuendelea kushirikiana na kutafuta suluhisho ikiwemo kupata vituo vya muda vya watoto ili kujifunza na angalau watoto waendelee na masomo haraka iwezekanavyo. Taarifa inasema kwamba ukosefu wa kutokwenda  shuleni watoto  kwa muda mrefu, unaweza kuwa na madhara makubwa ya muda mfupi na muda mrefu kwa watoto.  Aidha Unicef inaonesha  wasiwasi kwamba,  uharibifu wa miundombinu ya shule nchini Msumbiji  unaweza kuwa na madhara makubwa kwenye viwango vya uandikishaji watoto shuleni na kujifunza wakati  huu ambapo tayari viwango hivyo ni vya chini.

Watoto waliojiandikisha kwa ajili ya sekondati ni chini ya 20%

Takwimu zinaonyesha kuwa nchini Msumbiji, idadi idadi ya watoto waliojiandikisha kwa ajili ya shule ya sekondari ni chini ya asilimia 20. Walimu nao, kwa mujibu wa Unicef, wameathirika kutokana na kimbunga hicho kwa maana hiyo, Unicef inataka msaada pia uwalenge wao, ikiwemo msaada wa fedha ili waweze kujenga upya maisha yao na hatimaye warejee kufundisha. Hata hivyo tayari Unicef inashirikiana na wadau wengine kusaidia Watoto ili warudi  shuleni kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuwapatia vifaa vya shule na kujenga vituo vya muda vya kujifunzia, mahema na kukarabati mifumo ya maji safi na huduma kwa ujumla ya usafi. Kadhalika Unicef ili kufanikisha mipango hiyo nchini Msumbiji na mataifa mengi ya Zimbabwe na Malawi yaliyokumbwa na kimbunga Idai, imeomba dola milioni 122 kwa ajili ya operesheni za miezi 9 ijayo.

20 April 2019, 15:29