ILO: Takataka za plastiki na zile za kielektroniki zinachafua sana mazingira na ni hatari kwa usalama, maisha, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu! ILO: Takataka za plastiki na zile za kielektroniki zinachafua sana mazingira na ni hatari kwa usalama, maisha, ustawi na maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu! 

ILO: Taka za Kielektroniki ni hatari kwa mazingira na usalama wa watu!

Bwana Guy Ryder, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani, ILO, anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaweka sera na mikakati ya kuchakachua taka za kielekroniki, ili ziweze kutumia tena na hivyo kusaidia kusukuma mbele gurudumu la uchumi wa kimataifa, huduma kwa binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Taka hizi ni hatari sana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Takataka za plastiki zinaleta matatizo kwa samaki, ndege na watu. Katika mito na baharini, zinaweza kuleta madhara kwa samaki kwa sababu wanaweza kukanaswa na kushindwa kutoka. Takataka zilizoko ufukoni mwa bahari zimesababisha vifo vya viumbe wengi wa bahari. Umoja wa Mataifa unasema kwamba, asilimia 80%  ya plastiki zinaishia baharini, ikiwa ni karibu tani kati ya milioni 8 na milioni 12 kila mwaka.

Inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050 idadi ya plastiki kwenye bahari itakuwa ni kubwa zaidi kuliko idadi ya samaki. Kama hiyo haitoshi, chembechembe ndogo za plastiki ambazo zimepatikana kwenye maji ya kunywa na chumvi ya bahari, ni kiashiria kuwa kila binadamu duniani ana chembechembe za plastiki mwilini wake wake,  hali inayosababishwa na uchafuzi mkubwa wa mazingira utokanao na plastiki. Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, mwaka 2016 tani 480 bilioni za plastiki zilitumika na makadirio ni tani 560 bilioni zinatarajiwa kutumika ifikapo 2021. Kiasi kikubwa cha taka hizi, kitaishia: baharini, ziwani na mitoni, kiasi hata cha kuhatarisha maisha ya viumbe hai!

Hii ni changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa, changamoto ambayo inaweza kushughulikiwa kwa njia ya wongofu wa kiekolojia kama anavyokazia Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Laudato si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”.  Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa utunzaji wa mazingira, kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa haki, kwani uharibifu wa mazingira unalinganishwa na umaskini. Anaihimiza jamii pamoja na kuendelea kutunza furaha, amani na utulivu wa ndani; mambo ambayo yanategemeana na kukamilishana!

Shirika la Kazi Duniani, ILO, Kwa kushirikiana na Jukwaa la Uchumi Duniani, Mradi wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira, UNEP pamoja na wadau mbali mbali wamebainisha kwamba, licha ya taka taka za plastiki zinazoendelea kuchafua mazingira kiasi cha kutishia usalama wa viumbe hai, kuna wimbi kubwa la taka za kielektroniki kadiri ya tani milioni hamsini zinazozalishwa kila mwaka. Leo hii ni asilimia 20% ya taka hizi zinazoweza kuchambuliwa kitaalamu, ingawa thamani yake inakadiriwa kuwa ni zaidi ya Euro bilioni 55.

Bwana Guy Ryder, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani anasema kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaweka sera na mikakati ya kuchakachua taka za kielekroniki, ili ziweze kutumika tena na hivyo kusaidia kusukuma mbele gurudumu la uchumi wa kimataifa, huduma kwa binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira. Bwana  Ryder ameyasema haya hivi karibuni kwenye Mkutano wa wadau wa maendeleo uliofanyika huko Geneva, nchini Uswiss. Wajumbe wa mkutano huo wa siku tatu, walikazia kwa namna ya pekee kabisa, umuhimu wa kukuza na kudumisha uwekezaji katika hifadhi ya taka za kielektroniki pamoja na udhibiti wake katika ngazi mbali mbali. Taka hizi zikichakachuliwa vyema, zinaweza kutumika kama malighafi kwa wafanya biashara na wazalishaji viwandani, jambo ambalo linaweza hata kuongeza fursa za ajira, ustawi na maendeleo ya watu husika. Vinginevyo, taka za kielektroniki zinaelekea kuwa ni tsunami inayoendelea kuvamia ulimwengu na madhara yake ni makubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Taka hizi zinapaswa kukusanywa, kurudishwa tena kwenye mzunguko wa uzalishaji, ili hatimaye, zitengenezwe na kuwa ni bidhaa mpya, tayari kuuzwa sokoni. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na maboresho ya usalama wa kazi na wafanyakazi wenyewe kwa kulinda afya na haki zao msingi, ili wasigeuke kuwa wahanga wa taka za kielektroniki pamoja na kuendelea kuchafua mazingira nyumba ya wote! Wadau wanasikitika kusema kwamba, pengine ni vigumu kwa wafanyakazi katika sekta ya kudhibiti na uteketezaji wa taka za kielektroniki kubaini madhara yake mara moja. Taka hizi zinapoteketezwa na wafanyakazi kwenye Nchi changa na maskini duniani, wengi wao wanaathirika sana na daima kifo kiko mbele ya macho yao!

Utunzaji wa Mazingira

 

24 April 2019, 10:26