Tafuta

Jeshi la Sudan Kongwe limempindua Rais Omar Al Bashir na kumwondoa kutoka madarakani! Jeshi la Sudan Kongwe limempindua Rais Omar Al Bashir na kumwondoa kutoka madarakani! 

Yaliyojiri: Serikali ya Al Bashir wa Sudan Kongwe yapinduliwa!

Serikali iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Omar Al Bashir na kujitwalia madaraka. Aliyekuwa Rais wa Sudan Kongwe, Omar Al Bashir amezuiliwa nyumbani kwake na kwamba, majadiliano yanaendelea ili kuunda Serikali ya mpito! Jeshi la Sudan Kongwe limewatia mbaroni: Waziri mkuu wa Sudan Bwana Mohamed Taher Ella, Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Bwana Abdul Rahim M. Hussein

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jeshi la Sudan Kongwe, Alhamisi, tarehe 11 Aprili 2019 limepindua Serikali iliyokuwa chini ya uongozi wa Rais Omar Al Bashir na kujitwalia madaraka. Aliyekuwa Rais wa Sudan Kongwe, Omar Al Bashir amezuiliwa nyumbani kwake na kwamba, majadiliano yanaendelea ili kuunda Serikali ya mpito! Jeshi la Sudan Kongwe limewatia mbaroni: Waziri mkuu wa Sudan Bwana Mohamed Taher Ella, Aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Bwana Abdul Rahim Mohammed Hussein pamoja na waliokuwa Makamu wa Rais, Bwana Ali Osman Mohamed Taha pamoja na Bakri Hassan Saleh. Mwingine ni Msaidizi wa Bashir Bwana Ahmed Mohamed anayetafutwa na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita “The Hague-ICC” kwa shutuma za mauaji mkoani Darfur.

Jeshi la Sudan Kongwe linaendelea kuwasaka kwa udi na uvumba viongozi wengine 100 kutoka Serikalini. Mapinduzi haya ya kijeshi yamepelekea hadi wakati huu watu zaidi ya 50 kupoteza maisha. Katika miezi ya hivi karibuni, hali ya kisiasa na kijamii ilianza kuwa tete sana nchini Sudan Kongwe, lakini, Serikali haikuweza kusoma alama za nyakati, kiasi kwamba, vuguvugu likaanza kushika kasi na hapo Serikali ikaanza kutembeza mkong’oto wa nguvu hadi pale Jeshi lilipoingilia kati na matokeo yake ni mapinduzi ya kijeshi, Sudan Kongwe!

Omar Al Bashir mwenye umri wa miaka 75 aliingia madarakani kwa mapinduzi ya kijeshi kunako mwaka 1989. Tangu wakati huo, Sudan Kongwe ilianza kupoteza mwelekeo na kujikuta inatumbukia katika vita ya wenyewe kwa wenyewe, lakini zaidi kati ya Sudan ya Kaskazini na Sudan ya Kusini, iliyopelekea Sudan ya Kusini kupiga kura ya maoni na kuamua kujitenga na kuwa nchi huru Julai, 2011! Lakini hata hivyo mkono wa Rais Omar Al Bashir uliendelea kufanya kazi, kiasi cha kuitumbukiza Sudan ya Kusini katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kunako mwaka 2013. Mauaji ya kimbari yaliyofanyika mkoani Darfur kunako mwaka 2003 yaliendelea kuacha kurasa chungu sana katika medani za maisha ya Jumuiya ya Kimataifa.

Rais Omar Al Bashir alituhumiwa na Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana kwa karibu sana na Osama Bin Laden, aliyekuwa amehifadhiwa nchini humo kati ya mwaka 1992-1996. Huo ukawa ni mwanzo wa kuundwa kwa Kikosi cha Kigaidi cha Al Qaeda ambacho kimekuwa ni tishio kubwa kwa usalama, amani, utulivu na mafungamano ya watu mbali mbali duniani! Serikali ya Marekani kunako mwaka 1998 ikaituhumu Sudan Kongwe kuhusika na mashambulizi ya Balozi zake nchini Kenya na Tanzania. Rais Bill Clinton, akaamua kuishikisha adabu Sudan kwa kulipua kiwanda chake cha kutengeneza dawa! Matukio yote haya yaliweza kudhibitiwa na Rais Omar Al Bashir kiasi cha kuendelea kutawala kwa kipindi cha miaka yote hii!

Mazoea yana taabu sana! Ikumbukwe kwamba, tangu mwaka 1956 Sudan imekuwa ikitawaliwa kijeshi. Hii ni nchi ya kwanza kuanza kutekeleza SHARIA kwa wananchi wake wote. Sudan imekuwa ikiungwa mkono na China pamoja na Urussi! Wananchi wakavumilia, lakini, Mwaka 2019, ukaanza kuonesha nyufa na mipasuko mikubwa ya kijamii kwa mfumuko wa bei ya mahitaji msingi kupanda na kufikia asilimia 44%. Huo ukawa ni mwanzo wa mtikisiko wa uchumi kitaifa na matokeo yake wananchi wakaanza kufanya maandamano makubwa yaliyoasisiwa na msichana anayejulikana kwa jina la Alaa Salah, mwanafunzi, mwenye umri wa miaka 22 aliyejitokeza hadharani kuonesha nguvu ya umma katika kudai haki yake, kwa kutaka maisha bora zaidi kwa wananchi wa Sudan Kongwe!

Ni mwanafunzi aliyetumia mitandao ya kijamii kufikisha ujumbe kwa umati mkubwa wa watu, wakamuunga mkono kwa ajili ya haki, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Alaa Salah atakumbukwa katika historia ya Sudan kwa kuchochea mchakato na hatimaye, kuanguka kwa Rais Omar Al Bashir ambaye ameiongoza Sudan Kongwe kwa Miaka 30 kwa kutumia mkono wa chuma!

Mapinduzi ya Kijeshi Sudan Kongwe
12 April 2019, 17:48