Ripoti ya Unicef na Who inasema vituo vingi vya afya havina maji na vifaa vya kusafisha mikono,kuchambua taka. Huduma hizi na  maji muhimu katika kuzuia maambukizi Ripoti ya Unicef na Who inasema vituo vingi vya afya havina maji na vifaa vya kusafisha mikono,kuchambua taka. Huduma hizi na maji muhimu katika kuzuia maambukizi 

Ripoti mpya ya Unicef na Who kuhusu maji na huduma za usafi!

Ripoti ambayo imepewa jina“uwepo wa maji,huduma ya kujisafisha na usafi katika vituo vya afya”(WASH) iliyotolewa na Unicef na Who,ni ya kwanza kwa ukuu wa kiasi cha duniani ikiangazia maji,huduma za kujisafisha na usafi katika vituo vya afya.

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya pamoja iliyotolewa usiku wa kuamkia tarehe 3 Aprili 2019 mjini Geneva Uswisi na New York Marekani na shirika la afya duniani WHO na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, linasema kuwa kati ya vituo vinne vya afya duniani kote, kimoja kinakosa huduma za maji, hali inayowaathiri zaidi ya watu bilioni mbili. Ripoti hiyo ambayo imepewa jina “uwepo wa maji, huduma ya kujisafisha na usafi katika vituo vya afya” (WASH)ni ya kwanza ya ukubwa wa kiasi hiki duniani ikiangazia maji, huduma za kujisafisha na usafi katika vituo vya afya. Pia ripoti hiyo imegundua kuwa kituo kimoja kati ya vituo vitano vya afya hakina huduma ya kujisafisha, husuani kukosa vyoo au kuwa na vyoo visivyokidhi kiwango, hali ambayo inawaathiri watu bilioni 1.5 duniani. Aidha Ripoti hiyo inaendelea kusema kuwa, vituo vingi vya afya havina vifaa vya kusafisha mikono, kuchambua taka, hata mahali salama pa kuhifadhi taka. Huduma hizo ni za muhimu katika kuzuia maambukizi, kupunguza kusambaa kwa usugu bakteria na kutoa huduma bora hususani za kujifungua salama.

Naye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, “maji, huduma ya kujisafisha na huduma nyingine za usafi katika vituo vya afya ni mahitaji ya msingi ya kuzuia na kudhibiti maambukizi na pia kutoa huduma bora. Vitu hivyo ni vya msingi katika kuheshimu utu na haki za binadamu za kila mtu ambaye anatafuta huduma za afya na pia kwa wahudumu wa afya wenyewe”. Kutokana na hiyo, Bwana Guterres ametoa wito kwa watu mahali popote walipo kuunga mkono hatua hii ya WASH katika vituo vya afya. Na hiyo ni muhimu katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu, SDGs. Ripoti ya  WHO na UNICEF vile vile imegundua kuwa ni nusu tu yaani asilimia 55 ya vituo vya afya katika nchi zinazoendelea, LDCs, vyenye huduma ya msingi ya maji. Inakadiriwa kuwa mtoto 1 kati ya watoto 5 wanazaliwa katika nchi zinazoendelea, na kuwa kila mwaka, wanawake milioni 17 katika nchi hizi wanajifungua katika vituo vya afya vyenye uhaba wa maji, huduma za kujisafisha na usafi kwa ujumla.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF Henrietta Fore amenukiliwa akisema, “wakati mtoto anapozaliwa katika kituo cha afya ambacho kina uahaba wa maji, uhaba wa huduma za kujisafisha na uhaba wa usafi, hatari ya maambukizi na kifo kwa wote mama na mtoto inakuwa kubwa. Kila tukio la kujifungua linatakiwa kusaidiwa na mikono salama, iliyooshwa kwa sabuni na maji, kutumia vifaa vya kuua wadudu na mazingira masafi.” Vile vile katika Kijiji kidogo cha milima kiitwacho Daroot Korgon nchini Kyrgyzstan, imetengenezwa video ya UNICEF inayo mwonesha daktari mmoja tu ambaye anahudumia idadi ya watu takribani 25,000 na ambaye ameshuhudia jinsi ambavyo suluhuhisho dogo tu linavyoweza kuokoa maisha ya watoto wachanga kila siku. Dk Baktygul Pakirova anaishukuru UNICEF ilivyo isaidia hospitali anayoifanyia kazi na vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa kasi sana na kwamba ni watoto 10 hadi 15 wanazaliwa hapo kila wiki. Aidha anabainisha kwamba kama mtu angekwenda kutembelea hapo miaka miaka 7 iliyopita ilikuwa inashuhudiwa hali ya kutisha. Hakukuwa na maji ya kutiririka. Madirisha yalikuwa yametengenezwa kwa mbao na yalikuwa yanaruhusu upepo kuingia ndani. Hata akina mama walikuwa wanatetemeka kwa baridi wakati wa kujifungua.

Kadhalika anaeleza kuwa watoto walikuwa wanakufa kutokana na joto la chini katika miili yao, kutokana na tatizo linalo sababishwa na baridi kali. Vile vile anaishkuru UNICEF,  kwa kuboresha hali ya hospitali hiyo. Anaongeza kusema kuwa waliwapatia mafunzo. Walianza kwa kuunganisha mabomba na kuwaunganishia maji yanayotiririka. Waliwapatia  vifaa vya kutengeneza joto ili kupasha joto vyumba vyao vya kujifungulia. Walibadilisha madirisha na kuweka ya kisasa. Hivi leo idadi ya vifo vya watoto wachanga vimepungua sana.  Watafiti wa WHO na UNICEF wanaeleza kuwa zaidi ya vifo milioni moja kila mwaka vinahusishwa na ukosefu wa usafi wakati wa kujifungua. Maambuki yanafikia asilimia 26% kwa watoto wachanga na asilimia 11% ya wakati wa ujauzito.

Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa WHO  anaeleza kwamba: “fikiria kujifungua au kupeleka mtoto wako mgonjwa katika kituo cha afya ambacho hakina maji salama, vyoo au vifaa vya kujisafisha mikono.  Huo ndio uhalisia kwa mamilioni ya watu kila siku. Hakuna anayetakiwa kufanya hivyo na hakuna muhudumu wa afya anayetakiwa kutoa huduma katika mazingira hayo. Kuhakikisha vituo vyote vya vina huduma msingi za maji, huduma za kujisafisha na usafi, ni muhimu katika kufikia dunia ya afya, salama na ya usawa.” Kwa mujibu wa UNICEF, watoto wachanga 7,000 walikufa kila siku kwa mwaka 2017, kutokana na hali zinazo weza kuzuilika au kutibika. Hata hivyo katika mkutano mkuu wa afya wa dunia unaotarajiwa kufanyika mwezi Mei, 2019, serikali zitajadili maamuzi kuhusu maji, huduma za kujisafisha na usafi katika vituo vya afya.

04 April 2019, 14:58