Tafuta

Vatican News
Familia ya Mungu nchini Italia inawakumbuka watu walioguswa na kutikiswa na tetemeko la ardhi lililotokea mjini Aquila tarehe 6 Aprili 2009. Familia ya Mungu nchini Italia inawakumbuka watu walioguswa na kutikiswa na tetemeko la ardhi lililotokea mjini Aquila tarehe 6 Aprili 2009.  (ANSA)

Rais Mattarella: Miaka 10 tangu tetemeko la ardhi litokee Aquila

Mchakato wa ukarabati wa mji wa Aquila umekwisha kuanza, lakini bado kuna kazi kubwa sana mbele ya wananchi wa Aquila; jambo la msingi na kujenga umoja na mshikamano, ili mji huu uweze kushuhudia tena tunu zake msingi, mahusiano na mafungamano ya kijamii bila kusahau shughuli zake za kiuchumi! Bado sehemu kubwa ya makazi ya wananchi yanapaswa kufanyiwa ukarabati!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Sergio Mattarella wa Italia, katika kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 10 tangu tetemeko la ardhi lilipotokea mjini Aquila, amewaandikia ujumbe wa matumaini wananchi wa Aquila, akiwataka kusonga mbele na kwamba, Serikali iko pamoja nao. Ni vigumu sana kufuta katika historia madhara makubwa yaliyosababishwa na tetemeko hili la ardhi na kwamba, anawakumbuka kwa namna ya pekee: wananchi walioguswa na kutikiswa na janga hili katika maisha na historia yao. Serikali ya Italia inataka kuendelea kuonesha uwepo wake wa karibu na mshikamano kwa waathirika wote!

Mchakato wa ukarabati wa mji wa Aquila umekwisha kuanza, lakini bado kuna kazi kubwa sana mbele ya wananchi wa Aquila; jambo la msingi na kujenga umoja na mshikamano, ili mji huu uweze kushuhudia tena tunu zake msingi, mahusiano na mafungamano ya kijamii bila kusahau shughuli zake za kiuchumi! Bado sehemu kubwa ya makazi ya wananchi yanapaswa kufanyiwa ukarabati mkubwa! Mjini kati, amana na utajiri wa mambokale umeharibiwa sana, lakini wafanyakazi wanaokarabati amana ya mambokale wameonesha matumaini makuba. Rais Sergio Mattarella anaendelea kusema kwamba, kumekuwepo na mshikamano mkubwa wa hali na mali; kitaifa na kimataifa kwa ajili ya wananchi wa Aquila. Matumaini na mshikamano ni silaha madhubuti zinazopaswa kumwilishwa katika mchakato wa ujenzi na ukarabati wa mji wa Aquila, ili kufyekelea mbali hali ya kukata tamaa na woga usiokuwa na mashiko!

Ujenzi na ukarabati wa mji wa Aquila unaendelea kuwa bado ni changamoto kubwa ya kitaifa. Taasisi na wadau mbali mbali hawana budi kuhakikisha kwamba wanajitahidi kutegemeza miradi hii, kwa kujikita katika ukweli na uwazi pamoja na kuwashirikisha wananchi mahalia. Hii iwe ni fursa ya kujenga na kudumisha mtandao wa mshikamano wa maisha ya kijamii. Chuo Kikuu cha Aquila ni muhimu sana katika shughuli za usalishaji na huduma, kinapaswa kutumia rasilimali watu na fedha kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa mji huu, ili kuendelea kuwa kweli ni alama ya hamasa na matumaini.

Rais Sergio Mattarella wa Italia anahitimisha ujumbe wake kwa kusema, familia ya Mungu mjini Aquila inayo haki ya kuwa na matumaini ya kesho iliyo bora zaidi, kwa kuwafikiria vijana wa kizazi kipya; kwa kuendelea kuwakumbuka na kuwaombea wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Aquila waliopoteza maisha yao kwenye tetemeko hili lililotokea tarehe 6 Aprili 2009. Tetemeko hili lilifyekelea mbali ndoto ya maisha ya wanafunzi hawa na hadi sasa uchungu wa maafa yale, bado umekita katika akili na nyoyo za watu. Vijana wanayo haki ya kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi, chachu ya kuendelea kutekeleza mradi wa ukarabati wa Aquila kwa haraka zaidi!

Rais Mattarella: Aquila
06 April 2019, 15:06