Tafuta

Vatican News
Rais Sergio Mattarella wa Italia amemtumia Papa Francisko salam na matashi mema kwa Sherehe ya Pasaka 2019. Rais Sergio Mattarella wa Italia amemtumia Papa Francisko salam na matashi mema kwa Sherehe ya Pasaka 2019.  (ANSA)

PASAKA YA BWANA 2019: Salam za Mattarella kwa Papa Francisko

Rais Mattarella anasema, huu ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza kwa misingi ya kidini na kisiasa. Katika salam hizi, Rais Mattarella anakazia zaidi umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mama Kanisa anakiri na kufundisha katika Kanuni ya Imani kwamba: Akasulubiwa pia kwa ajili yetu sisi; akateswa kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato, akafa, akazikwa. Akafufuka siku ya tatu ilivyoandikwa. Fumbo la Pasaka ni kiini cha imani ya Kanisa inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa watu wa Mataifa. Kwa njia ya mateso, kifo, ufufuko kutoka kwa wafu na kupaa mbinguni, mwanadamu amekombolewa kutoka katika dhambi na mauti! Rais Sergio Mattarella kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, katika maadhimisho ya Sherehe ya Pasaka ya Bwana kwa mwaka 2019 amemtumia Baba Mtakatifu Francisko salam na matashi mema.

Anasema, Roho ya Pasaka ni mwaliko wa kusonga mbele kwa ari na ujasiri mkuu ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuendelea kupyaisha matumaini, utajiri mkubwa unaobubujika kutoka katika mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko. Rais Mattarella anasema, huu ni wakati wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza kwa misingi ya kidini na kisiasa. Katika salam hizi, Rais Mattarella anakazia zaidi umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote!

Rais Mattarella anampongeza Baba Mtakatifu kwa hija za kichungaji ambazo amezitekeleza kwa namna ya pekee nchini Italia, kielelezo cha uwepo wake wa karibu kwa familia ya Mungu nchini humu. Anamshukuru Baba Mtakatifu, kwa ujumbe aliowatumia wananchi wa Abruzzo, wakati wa kumbu kumbu ya Miaka 10 tangu Mkoa wa Marche na viunga vyake, ulipoathiriwa kwa tetemeko la ardhi kunako mwaka 2009. Rais Mattarella anamtakia pia Baba Mtakatifu heri na baraka, wakati wa kuadhimisha Siku kuu ya Mtakatifu Gregori, Shahidi, somo wake!

21 April 2019, 16:07