Tafuta

Vatican News
Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema mauaji ya watu 535 ni uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini DRC. Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inasema mauaji ya watu 535 ni uhalifu dhidi ya ubinadamu nchini DRC.  (AFP or licensors)

UN: Uhalifu dhidi ya ubinadamu: mauaji ya watu 535 nchini DRC.

Taarifa ya Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa inaonesha kwamba, watu zaidi 535 waliuwawa kikatili katika mapambano yaliyotokea Mwezi Desemba 2018, Magharibi mwa DRC. Hili ni kosa la uhalifu dhidi ya ubinadamu. Watu hawa walicharazwa viboko, wakanyanyaswa na wengine kuchomwa moto wakiwa hai! Hivi nivitendo vya kinayama vinapaswa kukemewa na wote!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa katika taarifa yake iliyotolewa, tarehe 13 Machi 2019 kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko Geneva, nchini Uswiss inaonesha kwamba, watu zaidi 535 waliuwawa kikatili katika mapambano yaliyotokea Mwezi Desemba 2018, Magharibi mwa DRC. Hili ni kosa la uhalifu dhidi ya ubinadamu. Watu hawa walicharazwa viboko, wakanyanyaswa na wengine kuchomwa moto wakiwa hai.

Tume hii inasema, mapigano haya yalitokea kati ya tarehe 16-18 Desemba 2018 katika Jimbo la Mai-Ndombe na kuwayahusisha makabila Batende na Banunu. Chanzo cha mauaji haya ni ugomvi wa mahali pa kumzikia kiongozi mkuu wa kabila la Banunu mjini Yumbi, jambo ambalo Batende wameona kuwa kama dharau dhidi yao. Idadi ya watu waliofariki dunia katika mapigano haya inawezekana ikawa ni kubwa zaidi watu 890 na kwamba, kuna uwezekano mkubwa kwamba, baadhi ya maiti zilitupwa mtoni.

Wakati huo huo, Rais Felix Tshisekedi wa DRC ametoa msamaha kwa wafungwa wa kisiasa 600 waliofungwa wakati wa utawala wa Joseph Kabila, hatua muhimu sana katika uongozi wake. Kati ya “vigogo” walioachiwa huru wamo akina Firmin Yangambi aliyefungwa kutokana na kosa la kutishia usalama wa taifa kunako mwaka 2009 na kupatikana na hatia ambayo ilimfanya apewe adhabu ya kifungo cha miaka 20 jela. Mwingine ni Franck Diongo, toka Chama cha Upinzani, aliyekuwa amefungwa jela kwa miaka 5. Rais Felix Tshisekedi ameahidi kuwaruhusu wananchi wote wa DRC waliokimbia nchi yao kwa hofu za dhuluma za kisiasa, kurejea na kuanza kushiriki katika ujenzi wa nchi yao.

Joseph Kabila aliyemaliza muda wake wa uongozi kwa njia ya kidemokrasia Desemba 2018, aliingia madarakani kunako mwaka 2001 baada ya baba yake Rais Laurent Kabila, aliyemwangusha Rais Mobutu Sese Seko madarakani kunako mwaka 1997 kuuwawa. DRC, tangu mwaka 1960 imekuwa ikiandika historia ya uongozi kwa damu ya viongozi waliouwawa kuanzia kwa Waziri mkuu wa kwanza Bwana Patrice Lumumba, aliyeuwawa miezi minne tu, baada ya DRC kujipatia uhuru wake kutoka kwa Ubelgiji. Itakumbukwa kwamba, Rais Felix Tshisekedi alishinda uchaguzi mkuu uliofanyika tarehe 30 Desemba 2018, bila kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia!

Umoja wa Mataifa

 

15 March 2019, 12:00