Tafuta

Vatican News
Tarehe 20 Machi ni Siku ya Furaha duniani Tarehe 20 Machi ni Siku ya Furaha duniani  

Tarehe 20 Machi ni Siku ya Furaha Duniani!

Kila tarehe 20 Machi ni Siku ya Furaha duniani ambayo ilitangazwa kunako tarehe 28 Juni 2012 na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.Kwa mujibu wa Ripoti ya Umoja wa Mataifa mwaka 2018,nchi zilizo na furaha zaidi ni Finland,Norway,Danimark,Swissland,Netherland,Sweden na Australia.Je ni kwa nini ziwe nchi zenye furaha zaidi?

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Tarehe 20 Machi ya kila mwaka ni Siku ya Furaha duniani, japokuwa si wote wanajua ni kwa kwa sababu na lengo lipi. Siku hii iliundwa kunako tarehe 28 Juni 2012 na Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ili iweze kuadhimishwa katika nchi zote wanachama.

Ni kwa nini kulianzishwa siku ya furaha?

Ili kuweza kupata sababu ya siku hii  ya furaha Kimataifa, imefungwa katika  ibara  ya A/RES/66/281  ya Mkutano wa Umoja wa Mataifa, ambapo wanathibitisha kwamba, kutafuta furaha ni moja ya lengo kuu msingi wa maisha ya binadamu na zaidi ni kutambua mbinu inayojumuisha zaidi, ya usawa katika ukuaji wa uchumi na ambao kwa dhati unalenga maendeleo endelevu ya mwanadamu; aidha kuondokana na umasikini na hatimaye kuweza kuwa na furaha na ustawi wa watu wote! Mambo haya na zaidi ni moja ya mambo mengine ya kumwezesha mwanadamu aonje kweli ustawi wa  maisha yake katika jamii. Kutokana na msingi, ndipo waliamua kutangaza tarehe 20 Machi kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Furaha na kuwaalika nchi zote wanachama  wa  Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa na kikanda, pamoja na mashirika ya kiraia, yakiwemo yale mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi, kusherehekea sikukuu ya Siku ya Furaha duniani kwa namna inayofaa, hata kwa njia ya kufanya shughuli  za pamoja zinazolenga elimu, ili kukuza ufahamu katika umma. Kwa asili, suala la kutafuta furaha linawakilisha moja ya haki za msingi kabisa za kibinadamu na lengo msingi la maisha ya binadamu!

Jayme Illien na wazo la kuanzishwa kwa siku hii

Alikuwa ni mshauri maalum wa Umoja wa Mataifa Jayme Illien, aliyechagua siku hii ya tarehe 20 Machi iliyoangukia kwa dhati katika kuanza kwa msimu mpya wa vipindi vya mwaka.  Ni kipindi na siku ambayo inasikika na watu wengi duniani. Miaka thelathini na mbili kabla ya kuanzisha kwa Siku ya Furaha ya Duniani, Jayme Illien alikuwa ni yatima aliyeokolewa kutoka katika mitaa ya Calcutta na Watawa Wamisionari wa upendo wa Mama Teresa. Jayme baadaye alikabidhiwa kwa mama mmoja mwenye  umri wa miaka 45 kutoka Marekani  aitwaye Anna Belle Illien  na ambaye, baada ya kumchukua mtoto huyo, alianzisha  Shirika moja la Kimataifa lilisilo la Kiserikali huko Atlanta linalohusika na kuwasaidia watoto yatima.

Nchi zilizo na furaha zaidi duniani

Kwa mujibu wa Ripoti  ya Umoja wa Mataifa kuhusu Furaha duniani  kwa mwaka 2018 inathibitisha kuwa nchi iliyo na furaha zaidi duniani ni Finland. Zifuatia nchi ya Norway ambayo ilikuwa ya kwanza kwa mwaka 2017, pia  Danimark, Island, Swissland, Netherland, Sweden na  Australia. Nchi ya Italia ni ya 47 tu, lakini kwa nchi 10 za kwanza zinaonesha kuwa masaa ya jua hayaingiliani nasuala la  furaha hiyo. Hata hivyo kufuatia na maelekezo, inadhihirisha kwamba furaha inategemeana na misaada ya kijamii, kuwa na matumaini ya kijamii na yaliyo endendelevu, uhuru kamili, ukarimu na kutokuwapo na aina zozote za ufisadi au rushwa ndani ya jamii, ili kumwezesha mwanadamu kuonja furaha ya kweli ya roho na mwili kwa ujumla!

Mtaalam Laurie Santos wa saikolojia na sayansi ya ubongo chuo kikuu,Yale 

Katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya furaha, kuna  hata ushuri kwambwa iwapo huna raha, usijali kwa sababu unaweza kujifunza kuwa mtu mwenye furaha zaidi maishani. Kama wanavyojifunza wanamuziki na wanariadha kuwa bora na kufanikiwa, basi inabidi na wewe ufanye vivyo hivyo iwapo unataka kuwa na furaha. Na hivyo ni kwa sababu huwezi tu kuwa na furaha,ni lazima ujizoezeshe” kwa mujibu wa wataalam, kama vile  Laurie Santos, mhadhiri wa saikolojia na sayansi ya ubongo kutoka chuo kikuu cha Yale nchini Marekani.

Kwa upande wa Santos yupo katika nafasi nzuri ya kutuonyesha namna ya kuepukana na huzuni. Katika  darasa lake  la “Saikolojia na maisha mazuri” lina umaarufu mkubwa katika historia ya miaka 317 ya uwepo wa chuo hicho kikuu cha Yale nchini Marekani. Kwa mujibu wa mtaalam huyo Santos, anasema, Sayansi imedhihirisha kwamba kuwa na furaha inahitaji jitihada za kusudi. Sio rahisi na huchukua muda, lakini inawezekana. Na ili kuweza kufanya hivyo  Profesa Santon anatoa vidokezo vitano vikuu vya kukusaidia kuipata furaha maishani mwako.

Tengeneza orodha ya kuwa na shukrani

Profesa Santos anawataka wanafunzi waandike mambo ambayo wanashukuru kuwa nayo maishani mwao, kila siku usiku kabla ya kulala, kwa muda wa wiki nzima. Hii inakuwa orodha yao ya mambo wanayoshukuru kuwa nayo. Na anathibitisha kuwa huenda likaonekana kuwa jambo rahisi lakini tumewaona wanafunzi wanaofanya zoezi hili kila siku na wanaonekana kuwa na furaha zaidi.

Lala zaidi na kwa muda mrefu

Changamoto ni kujitahidi kulala kwa saa nane, kila siku kwa wiki nzima. Huu umeonekana kuwa mtihani mkubwa zaidi kuutimiza kwa mujibu wa Santos. “Huenda likaonekana kuwa jambo la ujinga, lakini tunajua kwamba kulala kwa muda zaidi na usingizi mzuri kunapunguza nafasi ya wewe kuugua msongo wa mawazo na huimarisha tabia ya mtu”.

Tafakari

Profesa Santos anasema, chukua muda wa dakika angalau 10 kila siku kukaa kimya na kutafakari kila siku. Yeye binafsi anatoa ushuhuda kuwa alipokuwa mwanafunzi ilimsaidia sana kufanya hivyo. Sasa yeye ni mhadhiri anawaeleza wanafunzi wake kwa kutumia tafiti mbali mbali zinazothibitisha kwamba kutafakari na mazoezi mengine yanayo changamsha akili yanaweza kukusaidia kuwa na furaha zaidi.

Kuwa na mahusiano karibu na uzungumze na familia na rafiki

Kwa mujibu wa Profesa Santos, anathibitisha kuwa kuna utafiti unaoongezeka na kubaini kwamba kuwa na muda mzuri na mwafaka na familia na marafiki wa karibu unasaidia kupata furaha. Kukaa na watu tunaowapenda au kuwa na mahusiano ya karibu katika jamii, kimtazamo wa kisaikolojia, inasaidia kuimarisha afya yako. Ma siyo jambo kubwa,anasema Santos, la muhimu  hakikisha tu unajivinjari, utambue kwamba umetenga muda huu kuwa na walio karibu na wewe na utambue namna mnavyotumia muda huo.

Punguza uhusiano wako katika mitandao ya kijamii na uwe na  mahusiano halisi

Huenda tukapata furaha isiyo halisi kutoka kwa marafiki wa mitandao ya kijamii lakini ni muhimu  usijali hilo. Hiyo ni kutokana na kwamba, utafiti wa sasa unaonyesha watu wanaotumia mitandao ya kijamii kama Instagram, huwa hawana furaha ukilinganishwa na wasio tumia mitandao hiyo sana.

Kwa maana hiyo, katika kuhitimisha na kukazaia  juu ya mtaalam huyo, iwapo unataka kuwa na furaha ya dhati maishani, anza kwa kuwa mtu mwenye shukrani zaidi, lala mapema usiku,punguza mawazo na jihusishe zaidi na  watu wanaokupa furaha na unaowapenda wakati huo huo kuachana na mitandao ya kijamii kwa kiasi flani ili kukazia kutengeneza mahusiano ya karibu na dhati. Kama kwa wengine iliweza kuwasaidia na inawasaidia ni wazi kuwa unaweza kukusaidia hata wewe.

20 March 2019, 10:27