Tafuta

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi inaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. 

Siku ya Wanawake Duniani kwa Mwaka 2019

Umefika wakati kwa Mama Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha wanawake wanaoteseka kutokana na mifumo mbali mbali ya ukandamizaji: katika familia, maeneo ya kazi na hata katika maisha ya hadhara. Umaskini wa wanawake sehemu mbali mbali za dunia ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuwakoa kutoka katika utumwa mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inasema, kauli mbiu ya kitaifa ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 6 Machi 2019 nchini Tanzania inasema: “Badili Fikra Kufikia Usawa wa Kijinsia kwa Maendeleo Endelevu”. Kwa mwaka huu, Maadhimisho yataendelea kufanyika katika ngazi ya Mkoa ili kutoa wigo mpana kwa wanawake, wadau mbalimbali na kila Mtanzania kutathmini hatua tulizofikia kama Taifa katika masuala ya usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake na wasichana.  Aidha, Maadhimisho haya ni fursa ya kujadiliana namna ya kukabiliana na changamoto katika kufikia Maendeleo fungamani!

Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini ilifanya mkutano wake na wajumbe pamoja na mambo mengine, walipendekeza kufanyike Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Wanawake. Lengo ni kukuza na kudumisha utu, heshima na haki msingi za wanawake. Kanisa liwe na ujasiri wa kupambana na nyanyaso, dhuluma na uonevu wanaokumbana nao wanawake katika maisha na utume wao! Umefika wakati kwa Mama Kanisa kusikiliza na kujibu kilio cha wanawake wanaoteseka kutokana na mifumo mbali mbali ya ukandamizaji: katika familia, maeneo ya kazi na hata katika maisha ya hadhara. Umaskini wa wanawake sehemu mbali mbali za dunia ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga, ili kuwakoa kutoka katika utumwa mamboleo.

Wajumbe, wameshauri kama sehemu ya mikakati ya shughuli za kichungaji kukazia majiundo awali na endelevu katika Sakramenti ya Ndoa kwa kujikita katika: uzuri, utakatifu, ukweli na changamoto za Injili ya familia ndani na nje ya Kanisa. Lengo ni kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili wazazi waweze kuwajibika barabara katika malezi na makuzi ya watoto wao, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia zao. Changamoto kati ya kazi na wajibu wa kifamilia zinapaswa kuangaliwa vyema, ili kupambana na ubinafsi, uchoyo na utamaduni wa kifo unaotishia umoja na mafungamano ya wana ndoa! Kanisa litambue dhamana na wajibu wake kuwa ni “Mama na Mwalimu”.

Wajumbe, wamewahimiza wanawake kuendelea kujielekeza zaidi katika malezi na makuzi ya watoto wao; kwa kukazia pia mahusiano mema kati ya wakleri, watawa na wanawake katika jamii, ili kusaidiana na kukamilishana katika maisha na utume wa Kanisa. Jumuiya za Kikristo hazina budi kuwa makini na dhana ya usawa wa kijinsia unaotaka kung’oa tofauti msingi kati ya mwanaume na mwanamke kwa kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo, kwani hizi ni dalili za ukoloni wa kiitikadi unaoenea kwa kasi sehemu mbali mbali za dunia.  Ndoa za watu wa jinsia moja si sehemu ya haki msingi za binadamu! Sera za utoaji mimba na kifo laini ni kinyume kabisa cha Injili ya uhai na haki msingi za binadamu! Wajumbe wamekazia sheria kanuni na msingi wa maadili na utu wema. Kumbe, Kanisa lisichoke kufanya majadiliano ya kina na endelevu na wanasiasa wanaotaka kukumbatia utamaduni wa kifo.

Wanawake

 

05 March 2019, 10:53