Tafuta

Vatican News
Upo ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya ngazi zote za serikali na ambao umewawezesha wawe katika hali nzuri  kuhusiana na sheria nchini Rwanda Upo ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya ngazi zote za serikali na ambao umewawezesha wawe katika hali nzuri kuhusiana na sheria nchini Rwanda  (2019 Getty Images)

Rwanda:Wanawake nchini Rwanda wanashiriki maamuzi katika ngazi zote serikalini!

Bi Emma Rubagumya mbunge na mwanakamati wa Kamati ya masuala ya jinsia katika Bunge la Rwanda,anayewakilisha nchi yake katika Mkutano wa 63 wa Kamisheni ya hali ya wanawake CSW,katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York,anasema ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya ngazi zote imewaweka mahali pazuri!

Na Sr. Angela Rwezaula- Vatican

Ushiriki wa wanawake katika maamuzi ya ngazi zote za serikali umeiweka pazuri Rwanda. Hayo yamethibitishwa na mwakilishi wa Rwanda kwenye mkutano wa unaotathmini hali ya wanawake  kwenye mkutano unaoendelea mjini New York, Marekani ambapo anathibitisha kuwa, tangu wanawake walipoanza kushirikishwa moja kwa moja katika shughuli za serikali, Rwanda imepiga hatua kubwa katika nyanja zote. Bi Emma Rubagumya mbunge na  mwanakamati wa Kamati ya masuala ya jinsia katika Bunge la Rwanda  ambaye anaiwakilisha nchi yake katika Mkutano wa 63 wa Kamisheni ya hali ya wanawake CSW, huko  Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York Marekani, akizungumza nje ya mkutano huo anasema:  “Sisi kama wanawake tunapokuwa wengi katika ngazi za kufanya maamuzi,  inakuwa rahisi kwetu kwamba kila maamuzi yanayofanywa serikalini basi huwa wanawake wameweka mchango   wao ambao unatoka kwenye kujua matatizo hasa  yanayowakabili wanawake”.

Kadhalika katika mahojiano maalum mbunge Emma ameeleza hatua zilizopigwa, za wanakwa ya kuwa: “wanawake au watoto wa kike walikuwa hawana sheria ambayo inawasaidia kupata urithi. Sasa hivi ni kwamba watoto wa kike au wa kiume wanaweza kupata urithi kutoka kwa wazazi wao kwasababu wanawake waliokuwepo walisema  kwamba si vizuri urithi uwe kwa watoto wa kiume tu. Mambo ya kumiliki mali kama ardhi, mwanzoni wanawake hawakuwa na sheria inayowaruhusu kumiliki mali au ardhi  lakini sasa hivi  sheria tulizonazo zinawaruhusu wanawake kumiliki ardhi. Na kuhusu hatua iliyofikiwa dhidi ya ukatili wa kijinsia nchini Rwanda, Bi Emma Rubagumya anasema: hatukuwa na sheria ambazo zinawalinda wanawake au zinatoa adhabu kwa watu ambao wamefanya mambo ya unyanyasaji wa jinsia, lakini sasa hivi kuna sheria. Sasa hiyo ni mifano tu ambayo nimetoa lakini kuna sheria nyingi, kuna mikakati mingi  ambayo wanawake ambao wako kwenye ngazi za uamuzi wanatoa mchango wao. kwa hiyo faida ya kuwa na wanawake katika ngazi za uamuzi ianonekana kabisa Rwanda.”.

Hata hivyo kinyume na hali halisi ya kujikomboa huko kwa wanawake nchini Rwanda lakini bado mila na desturi zimeendelea kuwa mtihani mgumu sana  katika juhudi za ukombozi wa mwanamke katika kupata haki na sheria  sehemu mbalimbali duniani ikiwemo mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania, je kwa nini? Kwa mujibu wa Elizabeth Maro Minde kutoka katika Shirika la kijamii, linalojikita na haki za binadamu na jinsia liitwalo Kilimanjaro Women Information and Community Organization, akihojiana na mwandishi wa habari nje ya mkutano unaoendelea Mjini Newe York Marekani, anathibitisha wazi hali hiyo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa suala hilo ni muhimu katika hatua  na ndiyo maana nchi wanachama zinahimizwa kuhakikisha zinatokomeza kabisa mila na desturi ambazo zinapinga au kwenda kinyume  na maendeleo, kabla ya mwaka 2030 ili kutimiza ajenda ya maendeleo endelevu inayosisitiza kutomuacha yeyote nyuma hususani mwanamke. Nchini Tanzania ni jitihada kubwa zinazofanyika japokuwa kama anavyothibitisha katika baadhi ya maeneo ikiwemo mkoa wa Kilimanjaro, mila na desturi zimeendelea kuwa kikwazo na si suala geni. Yeye anabainisha kwamba, kazi yake kubwa ni kuhamasisha na kuelimisha jamii hususani wanawake kuhusu haki zao kisheria na jinsi ya kuzidai.

20 March 2019, 14:45