Tafuta

Vatican News
Katika kilele cha  Siku ya Maji duniani,Unicef imetangaza Ripoti mpya kuhusiana na vifo vya watoto kwa sababu ya kuhara kutokana na ukosefu wa maji salama na usafi Katika kilele cha Siku ya Maji duniani,Unicef imetangaza Ripoti mpya kuhusiana na vifo vya watoto kwa sababu ya kuhara kutokana na ukosefu wa maji salama na usafi  (ANSA)

Ripoti ya Unicef katika Siku ya maji duniani!

Ripoti ya UNICEF iliyotolewa katika kilele cha Siku ya Maji Duniania,inasema,viwango vya vifo katika nchi 16 wakati wa migogoro ya muda mrefu,kiasi kikubwa cha watoto chini ya umri wa miaka 5 wana uwezekano wa kufa mara 20 kutokana na magonjwa yanayohusiana na kuhara kwa sababu ya ukosefu wa maji salama na huduma bora za afya na usafi

Na Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Shirika la Saidia watoto UNICEF, waliyotoa tarehe 22 Machi 2019 ikiwa ni kilele cha Siku ya Maji duniani, inasema kuwa watoto chini ya miaka 15 katika nchi zilizokumbwa na migogoro kwa kipindi kirefu, nusu ya yao wana hatari kubwa mara tatu ya kufa kutokana na magonjwa ya kuhara ambayo chanzo chake ni ukosefu wa maji salama na huduma za usafi. Katika Ripoti iliyopewa jina:Maji chini ya shambulizi, inaonyesha viwango vya vifo katika nchi 16 wakati wa migogoro ya muda mrefu na inaonyesha kwamba, kwa kiasi kikubwa, watoto chini ya umri wa miaka 5 wana uwezekano wa kufa mara 20 kutokana na magonjwa yanayohusiana na kuhara kwa sababu ya  ukosefu wa upatikanaji wa maji salama  na huduma za afya na usafi ambao unatokana na migogoro moja kwa moja. Vikwazo tayari ni dhidi ya watoto wanaopata migogoro  hiyo ya muda mrefu na wengi wao hawawezi kufikia vyanzo vya maji salama, kwa mujibu wa Bi Henrietta Fore, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF.

Kwa hakika  kuna watu zaidi ya bilioni mbili ambao hawana uhakika wa maji safi na salama. Ukame wa kutisha ni chanzo kinachowapelekea watu kuzikimbia nchi na familia zao. Uchafuzi wa vyanzo vya maji na ukosefu wa uhakika wa maji safi na salama ni changamoto wazi  hasa katika nchi changa zaidi duniani na zile ambazo  migogoro ya kivita imedumu kwa muda mrefu. Hata hivyo uhakika wa maji safi na salama ni sehemu ya haki msingi za binadamu na ambayo inavaliwa njuga katika moja ya hatua za maendeleo endelevu kufikia mwaka 2030, japokuwa katika hali hii inaonesha ni kwa jinsi gani ilivyo dharura.

Kwa upande wa UNICEF wanasitiza kiu ukweli ni kwamba kuna watoto wengi ambao wanakufa kutokana na ukosefu wa maji salama kuliko risasi. Bila maji, watoto hawawezi kuishi. Na kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni, watu bilioni 2.1 duniani kote hawana maji ya salama na watu bilioni 4.5 hawatumii usafi wa mazingira safi. Bila maji safi na usafi wa mazingira, watoto wana hatari kubwa kwa lishe na magonjwa yanayoweza kuzuia, ambayo ni pamoja na kuhara, typhoid, kipindu pindu na polio. Inasisitiza Ripoti Vilevile watoto wasichana huathiriwa sana, kwani  huathiriwa na unyanyasaji wa kijinsia wakati wa kwenda kutafuta maji au wakati wanakwenda kuchanja kuni kadhalika hata kutafuta mahali pa kujisitiri kwa kutumia vibanda vyao.

Wanapaswa kujiadhali sana na hadhi yao. Wasichana wengi hawewezi kwenda shuleni wakati wa siku zao kwa sababu shuleni hakuna maji na usafi wa kutosha na mazingira magumu. Vitisho hivi vimebainika wakati wa migogoro na  wakati mashambulizi yasiyochagua  na ambayo yanaharibu miundombinu, kuumiza wafanyakazi na kukata vyanzo vya nishati vinavyowawezesha kupokea maji na kutumia mifumo ya usafi. Migogoro ya silaha pia huzuia ufikiaji wa vifaa muhimu vya ukarabati na matumizi kama vile mafuta ya taa na petroli. Huduma nyingi mara nyingi na  muhimu zinakataliwa kwa makusudi. Mashambulizi ya makusudi juu ya vifaa vya maji na usafi wa mazingira ni mashambulizi dhidi ya  watoto walio katika mazingira magumu, anathibitisha Fore na kuongeza kusema kuwa maji ni haki ya msingi. Ni lazima kwa maisha.

UNICEF inafanya kazi hata katika nchi zenye mgogoro ili kutoa maji safi ya kunywa na usafi wa kutosha kwa kuboresha na kutengeneza mifumo ya maji, kusafirisha maji, kujenga vibanda na kukuza uelewa  juu ya vitendo vya usafi. Ripoti hiyo imehesabu viwango vya vifo katika nchi 16 zenye  migogoro ya muda mrefu kwa mfano  Afghanistan, Burkina Faso, Cameroon, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ethiopia, Iraq, Libya, Mali, Myanmar, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Syria na Yemen. Katika nchi hizi zote, isipokuwa Libya, Iraq na Syria, watoto wenye umri wa miaka 15 na wachanga wana uwezekano mkubwa wa kufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na maji kuliko sababu ya vurugu. Isipokuwa Syria na Libya, watoto wenye umri wa chini ya umri wa miaka 5 ni mara 20 zaidi ya uwezekano wa kufa kutokana na magonjwa ya kuhara yanayohusiana na maji na usafi wa mazingira usio salama kuliko unyanyasaji wa pamoja.

Kadhalika katika kilele hiki cha Siku ya Maji duniani, Tanzania imechukua hatua ili kila mtu apate maji ifikapo 2030 ambayo ni hatua ya Malengo ya Maendeleo Endelevu. Malengo hayo ni kutaka kutomwacha mtu nyuma katika kupata huduma hiyo kwa kuzingatia lengo namba 6 la malengo ya maendeleo endelevu. Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. John Jingu, jijini New York, Marekani kandoni mwa mkutano wa 63 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani, CSW, na kusema hatua hiyo ni kupitishwa kwa sheria ya mfuko wa maji itakayoondolea adha wanawake na wasichana kutafuta maji mwendo mrefu. Bwana Jingu anasema “Maji ni changamoto kubwa. Serikali imepitisha sheria ya mfuko wa maji na sasa tunao mfuko wa maji na moja ya malengo ya mfuko wa maji ni kuhakikisha kuwa huduma ya maji inafika kila kona ya nchi, inafika mijini na vijijini kila mwananchi aweze kupata huduma ya maji, Niseme kwamba bado hatujakamata nchi nzima lakini maeneo mengi juhudi zinaendelea kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji safi na salama.”

Katika kuadhimisha duniani kote siku ya maji  ambamo inahesabika kuwa mabilioni ya watu wanaishi pasipo huduma ya maji safi na salama hatuna budi kuenzi hatua za maendeleo endelevu. Na ikumbukwe kwamba katika mojawapo ya malengo ya Maendeleo endelevu ya  Umoja wa Mataifa ili kufikia 2030 ni upatikanaji wa maji kwa kila mmoja na matumizi yake mazuri. Upatikanaji wa maji kwa kila mmoja ni muhimu zaidi ili kuyafanikisha malengo yote kumi na saba yaliyowekwa na Umoja wa Mataifa.

22 March 2019, 14:49