Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 inapania kuonesha mshikamano wa dhati na Familia ya Mungu Barani Afrika. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 inapania kuonesha mshikamano wa dhati na Familia ya Mungu Barani Afrika. 

Mshikamano wa Papa Francisko na Familia ya Mungu Barani Afrika!

Bara la Afrika kwa sasa lina kiu kubwa ya: haki, amani, upatanisho na matumaini ya kuweza kuanza upya na kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti pasi na kukata tamaa hasa baada ya matukio ya vita, ghasia, kinzani na majanga asilia ambayo yamelikumba Bara la Afrika kwa siku za hivi karibuni! Hija ya Baba Mtakatifu Francisko inapania kuimarisha: amani na matumaini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 kwa kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Bara la Afrika kwa sasa lina kiu kubwa ya: haki, amani, upatanisho na matumaini ya kuweza kuanza upya na kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti pasi na kukata tamaa hasa baada ya matukio ya vita, ghasia, kinzani na majanga asilia ambayo yamelikumba Bara la Afrika kwa siku za hivi karibuni!

Taarifa za hivi karibuni zilizotolewa na Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, watu waliopoteza maisha kutokana na Kimbunga cha Idai kilichotokea hivi karibuni huko Msumbiji, Zimbabwe na Malawi ni zaidi ya watu 800. Nchi iliyoathirika sana ni Msumbiji ndiyo maana hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji inaongozwa na kauli mbiu “matumaini, amani na upatanisho” mambo msingi yanayohitajika kwa wakati huu, ili familia ya Mungu iweze kuanza upya kwa ari na moyo mkuu. Katika shida na mahangaiko ya wananchi wa Msumbiji, kwa sasa kuna mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu ambao tayari umekwisha kusababisha watu kadhaa kupoteza maisha.

Mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu kwa sasa unatishia maisha ya watu ambao wameathirika sana kutokana na maafa yaliyosababishwa na kimbunga cha Idai. Kuna uhaba mkubwa sana wa maji safi na salama pamoja na huduma za afya. Shirika la Afya Duniani, WHO linasema, mlipuko wa ugonjwa wa Kipindupindu unaweza kusababisha maafa makubwa katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika. Kwa upande wake, Bwana Antònio Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa amesikika akisema kwamba, maafa yaliyosababishwa na kimbungu cha Idai hivi karibuni ni kati ya majanga makubwa kuwahi kutokea katika historia ya Bara la Afrika kwa miaka ya hivi karibuni.

Umoja wa Mataifa unaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuchangia kwa hali na mali ili kusaidia kuokoa maisha ya watu huko Msumbiji, Zimbabwe na Malawi pamoja na kuanza mchakato wa kukarabati miundo mbinu iliyobomolewa kwa mafuriko, ili watu waweze kurejea tena katika maisha ya kawaida kwa imani, matumaini na moyo mkuu. Kwa sasa kiasi cha dola milioni 282 zinahitajika kwa ajili ya kusaidia Msumbiji kuweza kukabiliana na janga la kimbunga cha Idai. Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Msumbiji inapania pamoja na mambo mengine, kuonesha mshikamano wa upendo kwa familia ya Mungu nchini Msumbiji, ambayo imepitia vipindi vigumu vya vita ya wenyewe kwa wenyewe pamoja na majanga asilia ambayo yamekuwa pia ni chanzo kikuu cha maafa makubwa kwa watu na mali zao!

Papa Barani Afrika: Mshikamano
28 March 2019, 07:52