Nchini Burkina Faso inakabiliwa na mzozo wa wakimbizi wa ndani huku zaidi ya watu 100,000 wamefukuzwa makwao Nchini Burkina Faso inakabiliwa na mzozo wa wakimbizi wa ndani huku zaidi ya watu 100,000 wamefukuzwa makwao  

Burkina Faso:Mahitaji ya kibinadamu yameongezeka kwa kiwango cha juu tangu mwezi Juni 2018!

Kufuatia ongezeko la ukosefu wa usalama unao chochewa na uwepo wa vikundi vilivyojihami na mizozo baina ya jamii mbalimbali katika maeneo ya kaskazini ya kati na mashariki mwa Burkina Faso kumesababisha ongezeko la mahitaji ya kibinadamu kwa kiwango cha juu kuanzia mwezi Juni 2018 hadi miezi ya hivi karibuni

Na sr. Angela Rwezaula - Vatican

Naibu Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, (OCHA) Bi Ursula Mueller ambaye yupo ziarani nchini Burkina Faso amesema kuwa mahitaji ya kibinadamu yameongezeka kwa kiwango cha juu tangu mwezi Juni  2018 na katika miezi ya hivi karibuni. Msemaji wa OCHA mjini Geneva, Uswisi, Jens Laerke, amemnukuu Bi Ursula Muellera kisema kuwa hali hiyo ni kufuatia ongezeko la ukosefu wa usalama ikichochewa na uwepo wa vikundi vilivyojihami na mizozo baina ya jamii mbalimbali katika maeneo ya kaskazini ya kati na mashariki mwa Burkina Faso .

Kwa mujibu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, (OCHA), Burkina Faso inakabiliwa na mzozo wa wakimbizi wa ndani huku zaidi ya watu 100,000 wamefukuzwa makwao na zaidi ya nusu wamekimbia katika kipindi pekee cha miezi miwili iliyopita. Aidha zaidi ya watu 120,000 hawapati huduma za afya na wengine 670,000 wako katika hatari ya kukumbwa na njaa, watoto 130,000 wakikabiliwa na utapiamlo uliokithiri mwaka huu wakati shule zimefungwa na kuwanyima watoto 150,000 fursa ya kupata elimu.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu misaada ya kibinadamu, (OCHA) imesema kufikia mwishoni mwa mwezi Februari 2019  takriban watu 1.2 walikuwa wanahitaji msaada nchini Burkina Faso. Na mamlaka nchini Burkina Faso na watoa misaada wametoa msaada, lakini hatua zaidi zahitajika kufanyika kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya watu walioathirika, amesema Bi. Mueller.

Mwezi Februari 2019 serikali na watoa msaada walizindua ombi la dharura la dola milioni 100 kwa ajili ya kusaidia watu 900,000 wanaokabiliwa na mzozo ambapo hadi kufikia sasa ombi hilo limefadhiliwa kwa asilimi 16 tu. Jumatatu tarehe  4 Machi 2019, mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF umetoa milioni 4 kwa ajili ya kuimarisha msaada kwa wakimbizi wa ndani, jamii zinazowahifadhi na utoaji wa huduma kwa wanawake na wasichana 15, 500.

06 March 2019, 14:10