Tafuta

Vatican News
Watanzania watakiwa kutumia maadhimisho ya Wiki ya Sjeria kujipatia elimu na huduma ya Mahakama! Watanzania watakiwa kutumia maadhimisho ya Wiki ya Sjeria kujipatia elimu na huduma ya Mahakama!  (AFP or licensors)

Wiki ya Sheria: Wananchi jipatieni elimu na huduma ya Mahakama

Waziri Mkuu amesema jambo hilo ni jema kwani masuala ya kisheria si mepesi kujulikana kwa kila mwananchi na kwa sababu hiyo, wananchi wengi wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo ya kisheria. Amesema wananchi wengi hawajui taratibu na mienendo ya kimahakama na wakati mwingine wanakosa au kupoteza haki zao kwa kigezo cha kutofuata taratibu ili kupata haki zao hizo.

Na Mwandishi Maalum, Ofisi ya Waziri Mkuu – Dodoma. 

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kushirikiana na Mhimili wa Mahakama katika kuhakikisha huduma bora za utoaji haki zinawafikia wananchi kwenye maeneo wanayoishi kwa wakati. “Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli ni mdau muhimu wa Mahakama na inafuatilia kwa karibu changamoto zote zinazoikabili pamoja na wadau wengine katika mfumo wa utoaji haki.” 

Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumamosi, Februari 2, 2019 wakati akifungua wiki ya Sheria Tanzaniakatika viwanja wa Nyerere Square jijini Dodoma. Ametoa wito kwa wananchi watembelee mabanda ya maonesho hayo. Amesema kupitia wiki ya sheria wanachi watapata elimu kuhusu masuala ya sheria pamoja na kushuhudia na kunufaika na maboresho yanayofanywa na Mahakama kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika utoaji haki. Waziri Mkuu amesema jambo hilo ni jema kwani masuala ya kisheria si mepesi kujulikana kwa kila mwananchi na kwa sababu hiyo, wananchi wengi wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo ya kisheria. 

Amesema wananchi wengi hawajui taratibu na mienendo ya kimahakama na wakati mwingine wanakosa au kupoteza haki zao kwa kigezo cha kutofuata taratibu ili kupata haki zao hizo. “Nitoe rai kwa wananchi watumiae ipasavyo fursa hii ya Wiki ya Sheria inayoambatana na maonesho kwa lengo la kupata elimu na huduma mbalimbali hususan za kisheria.” Akizungumzia kuhusu dhamira ya Mahakama kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) katika kuleta mabadiliko kwenye utoaji haki, amesema ni hatua nzuri na itasaidia kuboresha utoaji wa haki kwa wakati.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewasihi katika matumizi hayo ya mifumo ya TEHAMA wasikatishwe tamaa na changamoto zitakazojitokeza kwani mara nyingi kitu kipya chochote hakikosi changamoto za hapa na pale.  “Binafsi naunga mkono uamuzi wa dhati wa Mhimili wa Mahakama kutumia TEHAMA katika usajili wa mashauri. Uamuzi huo unakwenda sanjari na azma ya Serikali ya kuhakikisha TEHAMA inatumika vema kwenye taasisi za umma kwa lengo la kutoa huduma bora na kwa wakati.” Kadhalika, Waziri Mkuu amesema matumizi bora ya TEHAMA yataipunguzia Serikali na mihimili mingine ya dola gharama za uendeshaji hususan katika utoaji huduma kwa wnanchi.

Amesema lengo la Serikali ni kuona kuwa huduma bora zinawafikia wananchi kwa urahisi na vilevile, zinapatikana wakati wote. “Nitoe wito kwa wadau muhimu wakiwemo Mawakili wa Serikali na Mawakili wa Kujitegemea, nao kutumia mifumo ya TEHAMA katika kusajili mashauri na wala wasiwe wao wa kwanza katika kulaumu na kubeza.”  Amesema Mawakili wote wa Serikali na Kujitegemea, wanapaswa kuwa sehemu ya kutatua changamoto zitakazoibuka katika matumizi ya mifumo hiyo ya TEHAMA kwa kuwasilisha mapendekezo kuhusu namna bora ya kuiboresha. Ameongeza matumizi ya TEHAMA siyo tu yatawawezesha kutoa huduma kwa wakati, lakini yataweka uwazi ambao utawapunguzia malalamiko mengi kuhusu watumishi wenu na utoaji haki. Waziri Mkuu amewataka watumie vema Wiki ya Sheria kwa ajili ya kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuhusu mapinduzi ya matumizi ya TEHAMA yanayoendelea Mahakamani.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Profesa Ibrahimu Juma amesema kwa kipindi cha wiki nzima, maonesho ya Wiki ya Sheria yatafanyika jijini Dodoma pamoja na kwenye Mahaka zote nchini, kuanzia ngazi ya wilaya. Pia, Jaji Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha viongozi wa vijiji, kata, wilaya, mkoa, idara na wizara, wabunge, majaji, mahakimu na watumishi wa umma wahudhurie maonesho hayo ya Wiki ya Sheria. Ametolea mfano banda la maonyesho la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu litawakumbusha kuwa mamlaka yao mihimili mitatu ya dola yanatokana na nguvu ya sheria, nguvu ambayo haimuonei mwananchi yeyote.

Jaji Mkuu amesema watu watakaoshiriki katika maonesho hayo kwa kutembelea mabanda watumie nafasi hiyo kujifunza na kutathmini umuhimu na hadhi ya mfumo wa kimahakama katika kustawisha maisha yao pamoja na kuwasaidia kupata haki kwa mujibu wa sheria. Kabla ya kufungua maadhimisho hayo ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika nje ya jiji la Dar es Salaam, Waziri Mkuu alishiriki matembezi ya kilomita tano pamoja na Jaji Mkuu na viongozi wengine yaliyoanzia Mahakama Kuu Dodoma hadi viwanja vya Nyerere Square na kisha alitembelea mabanda.

04 February 2019, 14:36