Serikali ya Tanzania imesema, wale watakaokwamisha ufufuaji wa zao la michikichi, watakiona cha mtema kuni! Serikali ya Tanzania imesema, wale watakaokwamisha ufufuaji wa zao la michikichi, watakiona cha mtema kuni! 

Tanzania: Watakaokwamisha ufufuaji wa zao la michikichi kukiona!

Serikali ya tanzania imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula, ambapo kwa mwaka inatumia zaidi ya sh. bilioni 600 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi. “Wizara ya Kilimo iwawezeshe watu wa utafiti ili waendelee na shughuli hiyo kwa kasi, iwaongeze watumishi kituoni hapa na ongezeni nguvu kwenye zao la michikichi kama mataifa mengine!

Na Mwandishi maalum kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Kigoma.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo nchini Tanzania, iwawezeshe watafiti katika kituo cha Utafiti cha zao la michikichi cha Kihinga mkoani Kigoma ili waweze kuongeza kasi ya uzalishaji wa mbegu bora za zao hilo. Amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu kwenye zao hilo la michikichi, hivyo Wizara ya Kilimo haina budi kukiwezesha kituo hicho kwa lengo la kuzalisha mbegu bora zitakazosambazwa kwa wakulima. Waziri Mkuu ameyasema hayo Jumapili, Februari 17, 2019 wakati alipotembelea Kituo cha Kihinga kwa ajili ya kukagua shughuliza uzalishaji wa mbegu za michikichi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kigoma.

Amesema Serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula nchini Tanzania, ambapo kwa mwaka inatumia zaidi ya sh. bilioni 600 kuagiza mafuta ya kula nje ya nchi. “Wizara ya Kilimo iwawezeshe watu wa utafiti ili waendelee na shughuli hiyo kwa kasi, iwaongeze watumishi kituoni hapa na ongezeni nguvu kwenye zao la michikichi kama yalivyofanya Mataifa mengine ya Costa Rica na Malaysia.” Amesema wakulima wa zao hilo wanahitaji kupata mafanikio, hivyo kituo hakina budi kuongeza nguvu ya uzalishaji wa mbegu bora. Ili wafikie malengo amewasahauri washirikiane na taasisi binafsi zinazozalisha mbegu. Pia Waziri Mkuu amesema chuo cha Maendeleo ya Jamii cha Kihinga, kiendelee kutoa elimu na Wizara ya Kilimo ijenge majengo yake inayoyahitaji kwa ajili ya kufanyia shughuli za utafiti. Eneo la chuo lina ukubwa kwa hekta 920.

Kwa upande wake, Mratibu wa Utafiti wa Kilimo kwa mikoa ya Tabora na Kigoma, Dkt. Filson Kagimbo amesema michikichi iliyopo sasa ina uwezo wa kuzalisha tani 1.6 ya mawese kwa hekta moja ambao kidogo na hauna tija. Amesema mbegu wanazozizalisha zinalenga kumuongezea tija mkulima kwa kuwa zitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani nne kwa hekta, pia wanaendelea kuangalia vinasaba vya mbegu vilivyopo ili wazalishe mbegu bora zaidi. “Tutakusanya vinasaba vyote vya mbegu tulivyonavyo na kuvitathimini na kuona uwezo wake na ikibidi tutaagiza kutoka nje ya nchi ili kuboresha zaidi.” Miche ya michikichi inachukua muda wa miezi 18 kutoka hatua ya uchavushaji hadi kusambazwa kwa wakulima.

Baada ya kumaliza shughuli ya ukaguaji wa uzalishaji wa mbegu kituoni hapo, Waziri Mkuu alikagua shamba la michikichi la Gereza la Kwitanga lenye ukubwa wa ekari 400 na kupanda mche kama ishara ya uzinduzi wa upandaji wa miche bora shambani hapo. Waziri Mkuu amesema Serikali imeamua kuongeza nguvu katika zao hilo na inategemea taasisi zake mbili za Jeshi la Magereza (Kwitanga) na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT-Bulombora), ambazo zina mashamba makubwa ya michikichi. Kadhalika Waziri Mkuu ameagiza elimu kuhusu kilimo cha zao la michikichi kuanzia hatua za awali hadi uzalishaji wa mafuta itolewe mashuleni ili wanafunzi waanze kupata ulewa na ifikishwe hadi kwa wananchi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali haitomvumia mtu yeyote  atakayebainika kuhujumu mkakati wake wa kulifufua zao la michikichi nchini Tanzania. Amesema wanataka kuona wakulima zao hilo wakinufaika kama wengine wa mazao makuu ya biashara, hivyo haitomfumbia macho mtu atakayezembea. Aliyasema hayo Jumapili, jioni Februari 17, 2019 mara baada ya kukagua shamba la michikichi la Kikosi cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Bulombora. Alisema Serikali inataka kuona wakulima wa zao hilo wakinufaika kama ilivyokuwa kwa wakulima wa korosho, chai, kahawa, pamba na tumbaku. Serikali imeamua kulifufua zao hilo kwa lengo la kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula kwani inatumia fedha nyingi kuagiza nje ya nchi. Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwaagiza viongozi mkoani Kigoma kwamba suala la kilimo cha michikichi liwe ajenda ya kudumu kwenye vikao vyao. Kadhalika, Waziri Mkuu aliiagiza Wizara ya Kilimo ianzishe shamba darasa la zao la michikichi ili wananchi waweze kujifunza mbinu bora za kulima zao hilo.

Awali, Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba alisema Serikali imetenga zaidi ya sh. bilioni 10 kwa ajili ya kuboresha kilimo cha zao la michikichi. Waziri huyo alisema kiasi hicho cha fedha kimetengwa katika bajeti ya wizara hiyo ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya kuboresha kilimo cha michikichi nchini Tanzania. Alisema iwapo kilimo cha zao hilo kitaboreshwa kitasaidia Serikali kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zikitumika kuagiza mafuta kutoka nje ya nchi. Pia, Waziri Mgumba alisema tayari wizara hiyo imeshaongeza watafiti zaidi ya 10 wa zao la michikichi katika kituo cha utafiti wa zao hilo cha Kihinga.  Waziri Mgumba amelipongeza Jeshi la Magereza na JKT kwa ushirikiano wanaoutoa kwa wizara katika kipindi hiki cha ufufuaji wa zao la michikichi. Naye Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Hussein Mwinyi amemhakikishia Waziri Mkuu kuwa maelekezo yote aliyoyatoa kuhusu kilimo cha michikichi watayatekeleza.

 

18 February 2019, 15:27