Vatican News
Dau la plastiki limesafiri kilometa 500 kutoka Lamu,Kenya hadi Zanzibar,Tanzania kuelimisha jamii juu ya madhara ya plastiki kwa binadamu na viumbe vya majini  Dau la plastiki limesafiri kilometa 500 kutoka Lamu,Kenya hadi Zanzibar,Tanzania kuelimisha jamii juu ya madhara ya plastiki kwa binadamu na viumbe vya majini  

UNEP:Dau la plastiki limesafiri kutoka Kenya hadi Unguja!

Dau la plastiki likiwa limebeba wanamazingira kutoka shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP,limesafiri kilometa 500 kutoka Lamu,Kenya hadi Unguja Zanziba kwa lengo la kuhamasisha jamii za pwani juu ya madhara ya plastiki kwa binadamu na viumbe vya majini

Na Sr. Angela Rwezaula-Vatican

Dau la plastiki lililosafiri kilometa 500 kutoka Lamu, nchini Kenya hadi Mji Mkongwe, Zanzibar nchini Tanzania hatimaye limetia nanga Unguja likiwa limetimiza azma yake ya  kuelimisha jamii zilipo pwani kwa Kenya na Tanzania kuhusu madhara ya plastiki kwa binadamu, mazingira na viumbe vya majini. Likiwa limebeba wanamazingira kutoka shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP na kampuni iliyohusika na ujenzi, Flipflopi, dau hilo lilipata fursa kuhamasisha jamii hizo za pwani juu ya madhara ya plastiki. Walikutana na wanafunzi, wanajamii na viongozi wa serikali na kubadilishana mawazo kuhusu jinsi ya kubadili mtazamo wa matumizi ya plastiki. Dau hilo lililojengwa na Ali Skanda kwa tani elfu 10 za taka za plastiki lilianza safari yake tarehe 24 mwezi Januari huko Lamu, nchini Kenya na kupitia Kipini, Malindi, Watamu, Kilifi, Mombasa, Diani, Shimoni, Wete, Pemba Kusini, Nungwi na hatimaye  leo  tarehe 7 limetia nanga Mji Mkongwe Zanzibar. Bado kuna haja kubwa ya kuweza kujikita katika kuelimisha jamii kuhusu tatizo kubwa la utupaji wa taka na uchafuzi wa mazingira.

Uchafuzi wa mazingira na mwaliko wa kutunza mazingira

Uchafuzi wa mazingira unasababisha athari nyingi katika jamii. Uchafuzi huo wa mazingira unatokana na kutupa takataka ovyo katika sehemu zisizoruhusiwa kama barabarani, baharini na kwenye mazingira ya nyumba zetu na kadhalika. Wazalishaji wakubwa wa takataka ni viwanda, taasisi za elimu (shule na vyuo), hospitali, pia hata taasisi za dini. Ili kuepuka athari hizo elimu ya mazingira ni muhimu sana. Mabadiliko ya tabia ya hali ya hewa duniani ni miongoni mwa athari za uchafuzi wa mazingira. Hali ya joto imeongezeka duniani, barafu katika milima imepungua au imekwisha.

Kwa mfano  Mlima Kilimanjaro kwenye miaka ya 1970 na 1980 ulikuwa umefunikwa na barafu kwa kiasi kikubwa, kwa sasa barafu imeisha na inasikitisha sana . Hii imetokakana na athari za uharibifu wa mazingira. Maji katika bahari yameongezeka ina maana kina cha maji baharini kimepanda, visiwa vingine vimemezwa na bahari na kwa maana nyingi watu waliokuwa wanaishi katika visiwa hivyo kuhama. Athari nyingine ni kuibuka kwa magonjwa kama magonjwa ya ngozi na saratani. Haya yote yanatokana na maendeleo yasiyokuwa endelevu na ambapo wadau wengi na watetezi wa mazingira wanaendelea kujikita kwa dhati na mapambano dhidi ya tabianchi, ambayo kwa kiasi kikubwa imetokana na mikono ya binadamu. Tutunze mazingira kwa faida ya wote. Mazingira yatunzwe kwa kizazi hiki na kijacho. Kila mmoja akiwa mlinzi wa mwingine/mwenzake katika matumizi ya mazingira inawezakana kabisa kufanikiwa  kupunguza athari za binadamu katika mazingira na kupunguza magonjwa ya mlipuko na kuyahifadhi mazingira kwa kufurahia matunda ya mazingira mazuri kwa kizazi hiki na kijacho. Elimu ya mazingira ni muhimu kwa kila mtu.

Mpango wa UNEP

Mpango wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya mazingira (UNEP) ni shirika la Kimataifa ambalo lilianzishwa kunako mwaka 1972 dhidi ya mabadiliko ya tabiachi kwa ajili ya kukuza utetezi wa mazingira na matumizi ya ubunifu wa rasilimali asili. Makao makuu yake yako mjini Nairobi Kenya,lakini kwa kufanya kazi katika sehemu zote duniani kwa njia ya ofisi nyingine tawala na ambapo anakuwapo na mwakilishi maalum na mtaalam ambaye anachukua maamuzi juu ya siasa ya mazingira na shughuli zote zinazotazama kwa namna ya pekee maeneo husika. Mpango wa Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Mazingira (UNEP) inafikiriwa kama moja wa mwakili wa mazingira ndani ya umbu la Umoja wa Mataifa. Licha ya kuwa na makao yake makuu Nairobi lakini kuna ofisi zao zilizotawanyika duniani kote.

Ofisi ya Kanda ya Ulaya iko Makao makuu Gineva ikishikishana timu ya ofisi zilizoko Bruxelles,Vienna, Moscow na Paris. UNEP inakuza kwa kiasi kikubwa siasa na haki ya kimataifa katika suala la mazingira na kukutafuta data za mazingira kwa njia ya ripoti mbalimbali na kuweka bayana wakioneshaa hatari zinazoshmbulia mazingira. Kwa sasa UNEP inatoa kipaumbe cha kusaidia nchi mbalombali husika ili waweze kujikikimu katika ulinzi wa  tabianchi, kuchangia kupunguza hatari za majanga ya asili na ambayo mara nyingi yanasababishwa na mikono ya binadamu kwa sababu ya kutupa taka hovyo. Inahamasisha nchi wanachama kuwa na maono ya pamoja katika ulinzi wa mazingira na uendeshaji wa maji kwa namna  endelevu; wanasaidia uandeshaji wa kitaifa kwa sasa katika siasa ya mazingira na kutoa mafunzo na zana mbalimbali kwa ajili ya mazingira ili kuboresha utambuzi wa mazingira kwa ngazi ya kimataifa.

08 February 2019, 14:18