Tafuta

Vatican News
UNESCO: Kwa mara ya kwanza Siku ya Elimu Duniani inaadhimishwa tarehe 24 Januari 2019. UNESCO: Kwa mara ya kwanza Siku ya Elimu Duniani inaadhimishwa tarehe 24 Januari 2019. 

UNESCO: Siku ya Elimu Duniani, 24 Januari 2019

Bi Audrey Azoulay, Mkurugenzi mkuu wa UNESCO katika ujumbe wake kwa Siku ya Kwanza ya Elimu Duniani anakaza kusema, elimu ni kati ya vipaumbele vilivyotolewa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, kama chachu ya mageuzi yanayofumbatwa katika ubora, usawa na fursa kwa wote kuweza kujiendeleza zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa, UNESCO  linasema elimu ni kati ya haki msingi za binadamu, ni sehemu ya mafao ya wengi na inawajibisha jamii nzima. Ni kutokana na umuhimu wa elimu katika jamii, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, mwezi Desemba 2018 likaazimia kuanzishwa kwa Siku ya Elimu Duniani, itakayokuwa inasherehekewa kila mwaka ifikapo tarehe 24 Januari. Lengo la Umoja wa Mataifa ni kubainisha na kuendeleza dhamana ya elimu kama sehemu ya mchakato wa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu: kiutu na kijamii.

Bi Audrey Azoulay, Mkurugenzi mkuu wa UNESCO katika ujumbe wake kwa Siku ya Kwanza ya Elimu Duniani anakaza kusema, elimu ni kati ya vipaumbele vilivyotolewa kwenye Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, kama chachu ya mageuzi yanayofumbatwa katika ubora, usawa na fursa kwa wote kuweza kujiendeleza. Bila elimu bora, itakuwa vigumu sana kuweza kupambana na mnyororo wa umaskini unaoendelea kupekenyua maisha ya watoto, vijana na wazee wengi duniani.

Bi Azoulay anasema, Jumuiya ya Kimataifa itashindwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi wala kwenda na wakati katika matumizi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Elimu bora itasaidia sana mchakato wa kujenga na kudumisha usawa kati ya watu, dhamana inayohitaji utashi wa kisiasa kama sehemu ya utekelezaji wake! Takwimu za Umoja wa Mataifa zinabainisha kwamba, kuna watoto na vijana zaidi ya milioni 262 ambao hawana nafasi ya kuhudhuria masomo shuleni.

Watoto milioni 617 hawajui kusoma wala kuandika na kwamba, asilimia 40% ya idadi ya watoto hawa ni wasichana wanaoishi katika maeneo ya vijijini! Hali ya Elimu Kusini mwa Jangwa la Sahara inaonesha kwamba, kuna zaidi ya watoto milioni 4 ambao wengi wao ni wakimbizi na wahamiaji wamelazimika kuacha kuendelea na masomo kutokana na vita, kinzani pamoja na mipasuko ya kijamii.

Umoja wa Mataifa kuhusu LENGO NAMBA NNE: Kuhakikisha Elimu Bora, Yenye Usawa na Kutoa Fursa kwa Wote Kujiendeleza. Lengo hili linasisitiza kuwezesha kila mtu kusoma, kujifunza na kuhakikisha kwamba binadamu wote wanafikia vipawa vyao kikamilifu. Kuhakikisha kuwa wasichana na wavulana wote wanahitimu elimu ya msingi na sekondari; bure, yenye ubora na usawa unaoleta tija. Kuongeza mahudhurio ya wanafunzi shuleni. Kuhakikisha kuwa wasichana na wavulana wote wana fursa sawa ya kupata elimu bora ya awali ili iwaandae kwa elimu ya msingi.

Kuhakikisha fursa sawa kwa wanawake na wanaume ili wapate elimu ya juu, mafunzo na ufundi stadi kwa gharama nafuu. Kuongeza idadi ya vijana na watu wazima wenye ujuzi pamoja na ufundi stadi kwa ajili ya ajira, kazi zenye heshima na ujasiriamali. Kuondoa matabaka ya kijinsia ndani ya elimu na kuhakikisha upatikanaji wa elimu katika ngazi zote ikiwemo mafunzo ya ufundi stadi kwa ajili ya watu wanaoishi katika maeneo hatarishi hususani, wenye ulemavu na watoto.

UNESCO: Siku ya Elimu Duniani 2019
22 January 2019, 15:35