Tafuta

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa: Athari za mabadiliko ya tabianchi bado ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa: Athari za mabadiliko ya tabianchi bado ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa 

Umoja wa Mataifa Mwaka 2019: Utu na heshima ya binadamu!

Mwaka 2019 uwe ni mwaka ambao Jumuiya ya Kimataifa itajizatiti zaidi kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, sanjari na kuboresha maisha ya wananchi wengi duniani. Mwaka 2019 uwe ni mwaka wa amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres katika salam na matashi mema kwa mwaka 2019 anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha: haki msingi za binadamu, utu na heshima yake; daima kwa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu wengi zaidi duniani. Mwaka 2018 umekuwa ni mwaka ambao umegubikwa kwa kiasi kikubwa na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha watu kukata tamaa ya maisha.

Bado mtutu wa bunduki unaendelea kurindima, kuna kinzani na migawanyiko ya watu kutokana na sababu mbali mbali hali ambayo pia imesababisha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasikitika kusema kwamba, kila kukicha kuna ongezeko kubwa la matabaka ya watu duniani, kiasi kwamba, idadi ya maskini, yaani “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi” inazidi kuongezeka, wakati ambapo utajiri na rasilimali dunia, zinaendelea kumilikiwa na watu wachache duniani.

Licha ya patashika nguo kuchanika sehemu mbali mbali za dunia, lakini Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anasema, kuna alama za matumaini kwa baadhi ya nchi duniani yaani: Mkataba wa kusitisha vita uliotiwa sahihi huko Yemen; mkataba wa amani kati ya Eritrea na Ethiopia na kwamba, Serikali ya Sudan ya Kusini itaheshimu mkataba wa amani uliowekwa kati yake na wapinzani, ili amani na utulivu viweze kurejea tena Sudan ya Kusini ambako watu wanaendelea kuteseka kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe, magonja na baa la njaa. Dhuluma na nyanyaso za watu wa kabila la Rohingya huko nchini Myanmar ni kati ya changamoto pevu kwa Jumuiya ya Kimataifa ili kuhakikisha kwamba, utu, heshima na haki msingi za wananchi hawa zinalindwa na kudumishwa. Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola huko DRC, umekwisha waathiri watu zaidi 560 na kati yao, 288 wamekwisha kufariki dunia.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameridhishwa na makubaliano yaliyofikiwa juu ya “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unaopania pamoja na mambo mengine: kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa, kiasi cha kutishia umoja na mshikamano wa kimataifa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia!

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, amepongeza juhudi za Jumuiya ya Kimataifa zilizofanikisha Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 Katowice, Poland ambao unakazia umuhimu wa utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kama kielelezo cha mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Umoja wa Mataifa utaendelea kujikita katika ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu sanjari na kuanzisha jukwaa la kimataifa ambalo matatizo na changamoto za Jumuiya ya Kimataifa zitaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kuzingatia misingi ya haki, amani na usawa!

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, amewakumbuka askari 20 kutoka Tanzania waliouwawa wakiwa wanatekeleza dhamana na wajibu wa kulinda amani chini ya Umoja wa Mataifa pamoja na Bwana Kofi Annan, Katibu mkuu wa saba wa Umoja wa Mataifa aliyefariki dunia tarehe 13 Septemba 2018 huko Accra, Ghana. Anasema Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana na hali ngumu inayofumbatwa katika wasi wasi kwa watu. Mwaka 2019 uwe ni mwaka ambao Jumuiya ya Kimataifa itajizatiti zaidi kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, sanjari na kuboresha maisha ya wananchi wengi duniani. Mwaka 2019 uwe ni mwaka wa amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Umoja wa Mataifa

 

03 January 2019, 09:14