Tafuta

Vatican News
Hali tete ya ulinzi na usalama nchini DRC inakwamisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola. Hali tete ya ulinzi na usalama nchini DRC inakwamisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola.  (AFP or licensors)

Hali tete ya ulinzi na usalama DRC inakwamisha vita dhidi ya Ebola!

Hali tete ya kisiasa nchini Jamhuri ya Watu wa Congo, DRC., inakwamisha mchakato wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini humo ambao unaendelea kuhatarisha usalama na maisha ya watu wengi zaidi. Hali tete ya usalama wa raia na mali zao, inaweza kusababisha mlipuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Afya Duniani, WHO, aliyeteuliwa tarehe Mosi, Januari 2017 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema, hali tete ya kisiasa nchini Jamhuri ya Watu wa Congo inakwamisha mchakato wa mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ebola nchini humo ambao unaendelea kuhatarisha usalama na maisha ya watu wengi zaidi. Hali tete ya usalama wa raia na mali zao, inaweza kusababisha mlipuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola.

Vurugu na ghasia vilitawala wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa kwanza kufanyika kidemokrasia nchini DRC tangu mwaka 1960. Wakati wote huu, DRC imekuwa ikitawaliwa kwa mapinduzi ya kijeshi pamoja na vita ya wenyewe kwa wenyewe inayosababishwa hasa na uchu wa madaraka, fedha na utajiri wa haraka haraka kiasi kwamba, utu na heshima ya wananchi wa DRC vinawekwa rehani. Rais Joseph Kabila anayemaliza muda wake  amesema, kuahirishwa kwa uchaguzi kwenye miji ya Beni na Butembo huko mashariki mwa DRC, hakuhusiani na msingi wowote wa kisiasa bali ni maeneo ambayo yameathirika kwa kiasi kikubwa na ugonjwa wa Ebola.

Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, hivi karibuni, alituma ujumbe wa mshikamano wa haki na amani, kwa familia ya Mungu nchini DRC, kwa kuonesha masikitiko yake kwa baadhi ya wananchi kutengwa katika zoezi la kupiga kura, hapo tarehe 30 Desemba 2018. Maaskofu wanasema, sababu zilizotolewa na CENI hazina mashiko, kwani tayari mbinu mkakati ulikuwa umetangazwa ili kuhakikisha kwamba, wananchi wanalindwa dhidi ya ugonjwa wa Ebola, ili waweze kushiriki katika zoezi hili la kidemokrasia, kama sehemu ya utekelezaji wa haki zao msingi kikatiba!

Maaskofu pia wanapenda kuungana na wananchi wa Yumbi walioathirika kutokana na vurugu zilizojitokeza na kusababisha makazi kadhaa ya watu kuchomwa moto! Maaskofu wamelaani vitendo hivi kwa kusema kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu yanapaswa kulindwa, kuendelezwa na kudumishwa. Maaskofu wanaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inatekeleza vyema dhamana na wajibu wake wa kuwalinda raia na mali zao.

Hivi karibuni, Makundi makubwa ya waandamanaji yalichoma matairi na kushambulia vituo vya Ebola mjini Beni baada ya Tume Huru ya uchaguzi nchini DRC, CENI kutangaza kwamba, Tume itachelewesha upigaji kura mpaka mwezi Machi, 2019 huko Beni, Butembo na maeneo yanayozunguka kwa sababu ya mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Wagonjwa 24 walikimbia katika moja ya kituo cha matibabu wakati kiliposhambuliwa na waandamanaji Wizara ya Afya nchini DRC ilisema. Waandamanaji pia waliandamana kwenye ofisi za Tume Huru ya uchaguzi mjini Beni kudai haki yao ya kupiga kura.

CENI pia imeahirisha  zoezi la upigaji kura katika mji wa Yumbo magharibi kwa sababu ya ghasia za kikabila. Wanasiasa wa eneo hili wamepinga vikali hatua hii kama ni njia ya kutaka kukienzi Chama tawala kuendelea kubaki madarakani! Matokeo ya uchaguzi mkuu, awamu ya kwanza nchini DRC, yanatarajiwa kutangazwa tarehe 6 Januari 2019.

WHO: Ebola DRC
02 January 2019, 10:15