Kila kukicha watafiti hawakosi kuendelea na utafiti kwa ajili ya saratani ambayo inazidi kuua maelfu ya watu Kila kukicha watafiti hawakosi kuendelea na utafiti kwa ajili ya saratani ambayo inazidi kuua maelfu ya watu 

Saratani:Leo hii kuna matokeo mazuri ya kutumia mionzi dhidi ya saratani!

Yapo matokeo mazuri yaliyojionesha kwa kutumia njia ya mionzi dhidi ya saratani, kwa mujibu wa watafiti wa kisayansi leo hii ambao wanaendelea kila kukicha katika kutafuta njia za kupambana na ugonjwa huu hatari katika mataifa yote duniani

Angela Rwezaula - Vatican

Yapo matokeo mema ya kutumia mionzi, yanayonekana hasa dhidi ya saratani zinazozidi kuongezeka kwa haraka, lakini pia kwenye aina fulani za seli za afya zinajitokeza kwa haraka. Shukrani kwa kazi ngumu na nyeti ya watafiti ambao wanapata tiba mpya na wanajifunza kila siku ili kupata ubora zaidi wa tiba kuliko uliokuwa wa awali. Na kufuatia na utafiti mwingi, Shirika la Umoja wa Mataifa la nishati ya atomiki, (IAEA) limechukua hatua ya kusaidia mataifa 28 ya Afrika ambayo hayana hata mashine moja ya kutibu saratani. Lengo la Shirika la Nishati ya Atomiki (IAEA) ni kuhakikisha kuwa inabadili mwelekeo wa ugonjwa huo ambao mwaka 2012 kulikuwa na wagonjwa wapya 847,000 barani  humo na idadi inatarajiwa kufikia milioni 1.4 kwa mwaka 2030.  Saratani ni tatizo linalozidi kukua kila  uchao barani Afrika, wakati huu ambapo licha ya idadi ya wagonjwa kuongezeka,nchi 28 hazina hata mashine za kutibu ugonjwa huo, jambo ambalo Shirika la nishati ya atomiki duniani, (IAEA) linataka kubadili kwa kuingilia kati.

Msaada wa Shirika la Nishati ya Atomiki  kusaidia Zambia

Naye  Shaukat Abdulrazak mkuu wa Idara ya Nishati ya Atomiki kwa upadne wa  Afrika, (IAEA) amesema kuwa  wanasaidia nchi wanachama kwa kuzipatia fursa za mafunzo na pia kupitia mpango kushirikiana na serikali kununua pamoja vifaa vya kudhibiti saratani.Vile vile wanaweza kushughulikia suala la usalama na miundo mbinu. Shirika la Nishati ya Atomiki (IAEA) inasema, huduma ya mionzi ni mojawapo ya mbinu muhimu za kudhibiti saratani ikionesha  mfano  nchi ya Zambia ambayo kwa  mwaka 2007 ilianzisha kitivo chake cha kwanza cha kutibu ugonjwa huo na sasa ina mpango wa kuwa na kitivo cha pili. Serikali ya Zambia inakiri kuwa bila msaada wa Shirika la Nishati ya Atomiki (IAEA), isingaliweza kuwa na kituo hicho chenye vifaa vya hali ya juu.

Wagonjwa wa Saratani nchini Zimbabwe kupata huduma ya mionzi

Msaada wa Shirika la Nishati ya Atomiki (IAEA) umesaidia pia mafunzo kwa wahudumu wa afya nchini Zimbabwe kwa lengo la kuboresha usalama na tija kwenye huduma dhidi ya saratani. Hali hii imeongeza idadi ya wagonjwa wanaopata huduma za msingi dhidi ya saratani. Naye Daktari.Ntokozo Ndlovu ambaye ni Mhadhiri katika Idara ya sayansi za afya ya Chuo Kikuu cha Zimbabwe anasema:“Tulipokuwa hatuna huduma za kutosha za mionzi, wagonjwa wengi hawakuwa na mbadala. Na si kwamba huduma za mionzi zimeimarika, bali pia kiwango cha ubora wa mionzi ambayo tunapatia wagonjwa kimeongezeka.”

Msaada wa Kuwait kuwezesha wagonjwa wa saratani nchini Siria

Halikadhalika taarifa ya shirika la Afya ulimwenguni, WHO mwezi Desemba 2018 ilisema kuwa katika nchini Siria msaada kutoka Kuwait umewezesha angalau wagonjwa wa saratani kupata matibabu wanayohitaji na kuwarejeshea matumaini wakati  huu ambapo mapigano yanayoendelea nchini humo  na kusambaratisha huduma za afya. Msaada huo wa dola milioni moja kutoka Kuwait umewezesha shirika hilo kununua dawa muhimu za kutibu saratani pamoja na vifaa ambavyo vimesambazwa katika vituo nane vya kutibu ugonjwa huo nchini Siria.

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Siria Elizabeth Hoff alisema walishirikiana na hospitali za rufaa nchini humo ili kuandaa orodha ya dawa muhimu zaidi pamoja na vifaa ambapo vilivyopatikana vimepunguza pengo kubwa la matibabu ya saratani yaliyokuwa yanakabili nchi hiyo. Kabla kuanza mwa mzozo nchini Siria kunako mwaka 2011, huduma za tiba dhidi ya saratani zilikuwa zinapatikana bure katika vituo vyote vya afya. Hata hivyo mapigano licha ya kusambaratisha huduma, yamesababisha uhaba wa wahudumu wa afya, madaktari na vifaa katika vituo vyote 8 vya kutibu saratani.

Tayari wahudumu wa afya wa kitengo cha saratani katika hospitali ya watoto mjini Damasco, wanasema dawa zimeanza kuleta tofauti kubwa kwa wagonjwa na familia zao, na wakitoa mfano wa mtoto mmoja mwenye umri wa miaka 11 Yahya kutoka Ghouta ambaye zaidi ya mwaka mmoja uliopita aligunduliwa kuwa na saratani ya damu. Hata hivyo (WHO) inasema hivi sasa tiba mahsusi kutokana na msaada wa Kuwait umebadili maisha yake na ana afya njema. Kutokana na hili Shirika la Afya duniani (WHO) linashukuru Kuwait kwa msaada huo ambao umeleta mabadiliko chanya kwenye sekta ya afya hususan kwa kugusa wasiria walio maskini zaidi.

SARATANI
07 January 2019, 14:27