Tafuta

Vatican News
Panama ni kitovu cha uinjilishaji, kituo kikuu cha biashara na diplomasia ya kimataifa huko Amerika ya Kati Panama ni kitovu cha uinjilishaji, kituo kikuu cha biashara na diplomasia ya kimataifa huko Amerika ya Kati.  (Vatican Media)

Panama ni kitovu cha uinjilishaji, biashara na diplomasia

Panama inataka kuwa mahali ambapo haki na amani; upendo na mshikamano; uhuru na ustawi wa mataifa vitaweza kuchipua na kustawi. Panama inapaswa kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa watu kuheshimiana na kuthaminiana. Huu ndio utume ambao Panama inataka kuutekeleza, ili kuwa ni chombo cha amani na mjenzi wa mazingira bora.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Juan Carlos Varela Rodríguez wa Panama katika hotuba yake, Alhamisi, tarehe 24 Januari 2019 amemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko na ujumbe wake Panama, nchi ambayo imesimikwa katika amani, majadiliano, umoja na mshikamano unaounda historia ya Panama kwa takribani miaka 500 sasa. Panama kijiografia, imekuwa ni nchi ya uinjilishaji, daraja la biashara na kwamba, ndoto Bwana Simòn Bolivar, Muasisi wa Panama, ameiwezesha nchi hii kuwa na nafasi muhimu sana katika medani mbali mbali za kimataifa. Mwelekeo huu unathibitishwa na uwepo wa umati mkubwa wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia.

Panama imekuwa ni njia ambayo watangazaji na mashuhuda wa Injili kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamepitia, kiasi kwamba, leo hii Panama ni chombo cha huduma na uinjilishaji. Panama inapaswa kuendelea kuwa ni njia ya mawasiliano, mahali pa kujenga na kudumisha mshikamano na mafungamano ya kijamii; Panama iwe ni kiungo cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Mahali ambapo haki na amani; upendo na mshikamano; uhuru na ustawi wa mataifa vitaweza kuchipua na kustawi. Panama inapaswa kuendeleza mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa watu kuheshimiana na kuthaminiana. Huu ndio utume ambao Panama inataka kuutekeleza, ili kuwa ni chombo cha amani na mjenzi wa mazingira bora, nyumba ya wote.

Rais Juan Carlos Varela Rodríguez amelishukuru na kulipongeza Kanisa Katoliki nchini Panama kwa mchango wake katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya watu; kielelezo cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Amepongeza mchango wa Shirika la Wayesuit nchini Panama. Wakati huu Panama ni mwenyeji wa Siku ya Vijana Duniani, kutoka zaidi ya mataifa 150, ambao wanataka kusikiliza ujumbe wa amani, upendo na mshikamano, tayari kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao, ili kujenga dunia bora zaidi.

Rais Juan Rodríguez amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kukazia dhamana na wajibu wa wanasiasa, wito wa hali ya juu kabisa kwa wanasiasa, kielelezo cha upendo katika mchakato wa kutafuta ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Panama, ni kielelezo cha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene yanayowaunganisha watu, ili kutoa kipaumbele cha kwanza kwa binadamu na mahitaji yake msingi; kwa kuwajali maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wanaoshiriki katika maadhimisho haya, kati yao, wamo watetezi wa haki msingi za binadamu.

Hija ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kati, imekuja wakati ambapo kuna changamoto kubwa! Kumbe, uwepo wake kwa watu wengi, amekuwa ni chombo cha faraja, imani na matumaini hasa kwa wale wote wanaoteseka kutokana na vita, kinzani, migogoro na mipasuko wa kijamii. Watu wanaoteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi; vitendo vya uhalifu wa kupangwa bila kusahau wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ambalo limekuwa ni “mwiba mchungu” huko Amerika ya Kusini. Kwa hakika watu wanataka: haki, amani, usawa! Na kwa maneno haya, Rais Juan Carlos Varela Rodríguez amemkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili, tayari kuanza rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani.

Rais wa Panama

 

25 January 2019, 13:07