Tafuta

Vatican News
Salam na matashi mema kutoka kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa Papa Francisko. Salam na matashi mema kutoka kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia kwa Papa Francisko.  (AFP or licensors)

Siku ya Vijana Duniani 2019: Matashi mema kwa Papa Francisko!

Ni matumaini ya Rais Mattarella kwamba, vijana wataendelea kuchakarika katika ujenzi wa leo na kesho yao wakiwa wanawajibika pamoja na kujenga sanaa na utamaduni wa kukutana na wengine kama jirani. Mwishoni, Rais Mattarella amemtakia Baba Mtakatifu afya njema na maendeleo katika utekelezaji wa dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu alipowasili kwenye anga la Italia, amemtumia salam na matashi mema Rais Sergio Mattarella wa Italia, akimtaarifu kwamba, amerejea kutoka nchini Panama. Baba Mtakatifu anasema, nchini Panama, amekutana na vijana jasiri, wenye ari na moyo mkuu wanaotaka kujikita katika leo na kesho inayofumbata amani na udugu; kwa kuendelea kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo! Anapenda kumhakikishia Rais Mattarella na familia ya Mungu nchini Italia katika ujumla wake, sala zake za daima.

Rais Sergio Mattarella kwa upande wake, amechukua fursa hii kwa niaba ya familia ya Mungu nchini Italia, kumkaribisha tena kwa mikono miwili. Anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa ujumbe wa matumaini aliowaachia vijana wa kizazi kipya waliokuwa wanakutana huko Panama kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani. Ni matumaini ya Rais Mattarella kwamba, vijana wataendelea kuchakarika katika ujenzi wa leo na kesho yao wakiwa wanawajibika pamoja na kujenga sanaa na utamaduni wa kukutana na wengine kama jirani. Mwishoni, Rais Mattarella amemtakia Baba Mtakatifu afya njema na maendeleo katika utekelezaji wa dhamana na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Papa: Italia
29 January 2019, 14:32