Tafuta

Waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Falme za Kiarabu wanasubiri kwa hamu kukutana na Papa Francisko Waamini na watu wenye mapenzi mema nchini Falme za Kiarabu wanasubiri kwa hamu kukutana na Papa Francisko 

Papa Francisko Abu Dhabi: Watu wanataka kumwona "LIVE!

Wananchi wa Falme za Kiarabu wanamwona Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni kielelezo na chombo cha amani, maridhiano na udugu; mambo msingi yanayoweza kuimarisha majadiliano ya kidini katika ukweli, amani na utulivu kati ya watu wa Mataifa. Itakumbukwa kwamba, hii ni mara ya kwanza katika historia ya Kanisa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea Falme za Kiarabu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Hija ya 27 ya Kitume ya Baba Mtakatifu Francisko huko kwenye Falme za Kiarabu inaongozwa na kauli mbiu “Nifanye chombo cha amani”. Wananchi wa Falme za Kiarabu wanamwona Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni kielelezo na chombo cha amani, maridhiano na udugu; mambo msingi yanayoweza kuimarisha majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi; amani na utulivu kati ya watu wa Mataifa. Itakumbukwa kwamba, hii ni mara ya kwanza kabisa katika historia ya Kanisa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea Falme za Kiarabu.

Hija hii ya kitume, inakwenda sanjari na uwepo wa Imam Ahmad Muhammad Al-Tayyib, Imam mkuu wa Msikiti mkuu wa Al-Azhar, ulioko Cairo, nchini Misri, ambaye anaheshimiwa sana miongoni mwa viongozi wa dini ya Kiislam Madhehebu ya Sunni. Viongozi hawa wawili wamekuwa na ushawishi mkubwa katika mchakato wa majadiliano ya kidini sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Abu Dhabi, huko kwenye Falme za Kiarabu itapambwa kwa matukio na mikutano ya viongozi mbali mbali wa kidini, inayopania kukuza na kudumisha udugu wa kibinadamu, haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Kati ya matukio makuu yanayotarajiwa kuwakusanya watu wengi ni maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa Zayed, hapo tarehe 5 Februari 2019. Inakadiriwa kwamba, zaidi ya waamini na watu wenye mapenzi mema 135, 000 wataweza kushiriki. Wachunguzi wa mambo wanasema, hili litakuwa ni tukio kubwa na la aina yake kuwahi kuhudhuriwa na watu wengi kiasi hiki.

Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2019 umetangazwa na Nchi za Falme za Kiarabu kuwa ni Mwaka wa Maridhiano na wengine wanapenda kuuita Mwaka wa Kuvumiliana. Mwaka 2018, Waziri Sheikha Lubna Al Qassimi alitembelea mjini Vatican na kubahatika kukutana na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini. Falme za Kiarabu zina historia kubwa ya majadiliano ya kidini na uhuru wa kuabudu. Kunako mwaka 1965 Kanisa la kwanza la Kikatoliki lilijengwa huko Abu Dhabi. Lakini, katika kumbu kumbu inaonesha kwamba, huko kwenye Nchi za Falme za Kiarabu kulikuwepo na Makanisa pamoja na Monasteri kwa ajili ya watawa kunako karne ya saba. Takwimu zinaonesha kwamba kuna jumla ya Makanisa 76 kwa ajili ya Ibada na Serikali inaendelea kutoa ardhi kwa ajili ya kujenga nyumba za ibada nchini humo!

falme za Kiarabu

 

31 January 2019, 17:34