Tafuta

Vatican News
Waalimu nchini Guinea Bissau tangu mwezi Septemba 2018 wanaendesha mgomo baridi kwa madai ya nyongeza za msahara! Waalimu nchini Guinea Bissau tangu mwezi Septemba 2018 wanaendesha mgomo baridi kwa madai ya nyongeza za mshahara!  (AFP or licensors)

Mgomo wa waalimu nchini Guinea Bissau mwiba kwa elimu!

Waalimu nchini Guinea Bissau, tangu mwezi Septemba 2018 wamekuwa wakifanya mgomo baridi ambao utaendelea hadi mwishoni mwa mwezi Januari 2019, baada ya viongozi wa waalimu nchini humo kushindwa kufikia makubaliano na Wizara ya Elimu nchini Guinea Bissau kuhusu nyongeza ya mishahara kadiri ya kiwango kinachotolewa na nchi nyingine Afrika Magharibi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Elimu ni nyenzo muhimu na ya msingi inayomwezesha mwanadamu kuyasanifu mazingira kwa manufaa yake. Hii ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Kumbe, jamii inapaswa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kupanga, kutoa, kusimamia na kufanya tathmini ya elimu inayotolewa ili kuendeleza malengo yaliyobainishwa; kukidhi maadili na falsafa za kisiasa, mila na tamaduni njema za taifa husika. Elimu ni nyenzo ya kurithisha tunu msingi za maisha ya kiutu, kijamii, kitamaduni na kiroho kwa vizazi vyake.

Elimu huhitaji uwepo wa mbinu mkakati na ufundi wa kuweza kufikia malengo yanayotarajiwa yaani: kupata maarifa, ujuzi, ufundi au stadi za kukuza na kudumisha uhai wa jamii sanjari na kukuza utu wenye sifa zote zinazothaminiwa na jamii husika. Kuna haja ya kuwa na miongozo na mitaala muafaka kwa mujibu wa azma ya elimu, vifaa vya kutosha, mazingira bora ya kufundishia na kusomea pamoja na kuwa na waalimu waliotaalaumiwa katika taaluma ya kuwataalamu, watalaumiwa wa baadaye. Walimu wanapaswa kupata haki zao msingi, ili kutekeleza dhamana na majukumu yao barabara!

Mambo haya yanategemeana na kukamilishana! Yanaposigana kunakuwepo na hatari katika mfumo mzima wa elimu! Waalimu nchini Guinea Bissau, tangu mwezi Septemba 2018 wamekuwa wakifanya mgomo baridi ambao utaendelea hadi mwishoni mwa mwezi Januari 2019, baada ya viongozi wa waalimu nchini humo kushindwa kufikia makubaliano na Wizara ya Elimu nchini Guinea Bissau kuhusu nyongeza ya mishahara kadiri ya kiwango kinachotolewa na nchi nyingine Afrika Magharibi. Wizara ya Elimu nchini Guinea Bissau inawataka waalimu kuanza kazi tena tarehe 8 Januari 2019, tamko ambalo hadi sasa linakinzana na uamuzi wa waalimu nchini Guinea Bissau.

Wachunguzi wa mambo wanasema, Guinea Bissau kwa sasa inakabiliwa na hali tete sana kuhusiana na masuala ya kiuchumi, kisiasa na kijamii kutokana na kuenea kwa saratani ya rushwa na ufisadi wa mali ya umma pamoja na biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, hali ambayo inawatumbukiza vijana wengi katika janga na maafa makubwa kwa sasa na kwa siku za usoni! Watu wenye mapenzi mema wanaendelea kujiuliza hatima ya wanafunzi wa Guinea Bissau kwa sasa na kwa siku za mbeleni?

Mgomo Guinea Bissau
07 January 2019, 08:51