Tafuta

Vatican News
CENI: Uchaguzi mkuu nchini DRC kufanyika tarehe 30 Desemba 2018 CENI: Uchaguzi mkuu nchini DRC kufanyika tarehe 30 Desemba 2018  (AFP or licensors)

Sakata la Uchaguzi Mkuu DRC, sasa ni tarehe 30 Desemba 2018

CENI, imetangaza kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu nchini humo, uliokuwa unatarajiwa kufanyika Jumapili tarehe 23 Desemba na sasa utafanyika tarehe 30 Desemba 2018. Hatua hii imechukuliwa na Tume ili kuhakikisha kwamba, vifaa vya kupigia kura vinafika kwenye vituo kwa wakati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, CENI, imetangaza kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu nchini humo, uliokuwa unatarajiwa kufanyika Jumapili tarehe 23 Desemba na sasa utafanyika tarehe 30 Desemba 2018. Hatua hii imechukuliwa na Tume ili kuhakikisha kwamba, vifaa vya kupigia kura vinafika kwenye vituo kwa wakati. Itakumbukwa kwamba, hivi karibuni, ghala kuu ya Tume ya Uchaguzi DRC iliteketea kwa moto na kusababisha kuungua kwa baadhi ya vifaa muhimu vya uchaguzi.

Tayari Tume ya Uchaguzi imekutana na kujadiliana na wanasiasa kuhusu hatua hii na kufikia muafaka. Wachunguzi wa masuala ya kisiasa wanasema, ikiwa kama kweli demokrasia itashika mkondo wake na uchaguzi mkuu kufanyika, basi hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa wananchi wa DRC kushuhudia mabadiliko ya uongozi wa kisiasa kwa njia demokrasia na amani. Uchaguzi mkuu nchini DRC umekuwa ukiahilishwa tangu mwaka 2017 na hatimaye, kupangwa kufanyika tarehe 23 Desemba 2018 baada ya vuta nikuvute ya wapinzani na Rais Joseph Kabila anayemaliza muda wake wa uongozi kukosa sifa za kuongoza nchi tangu tarehe 20 Desemba 2016 ambapo muda wake wa uongozi ulipokwisha kikatiba.

DRC ambayo imebarikiwa kuwa na utajiri mkubwa wa mali asili na madini, imekumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa muda mrefu kutokana na uchu wa mali, madaraka na utajiri wa haraka haraka. Bwana  Corneille Nangaa, Rai wa Tume ya Uchaguzi nchini DRC amewahakikishia wananchi wa DRC kwamba, mara tu baada ya uchaguzi mkuu matokeo yataanza kutangazwa. Kwa sasa viongozi wanaopimana misuri katika kinyang’anyiro cha Urais ni Emmanuel Ramazani Shadary pamoja na viongozi wa vyama vya upinzani Bwana Felix Tshisekedi pamoja na Bwana Martin Fayulu.

Uchaguzi DRC 2018

 

 

22 December 2018, 10:40