Vatican News
Rais John Pombe Magufuli amewataka watanzania kuheshimu sheria za usalama na kutunza barabara kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rais John Pombe Magufuli amewataka watanzania kuheshimu sheria za usalama na kutunza barabara kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. 

Rais Magufuli: Heshimuni sheria na kutunza barabara!

Rais Magufuli amewataka watanzania kutii na kuheshimu sheria za nchi kwa kutoendeleza maeneo ya hifadhi ya barabara kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi na kujiletea umaskini. “Watanzania tujifunze kuheshimu sheria, ukisogelea barabara hasa hifadhi ya barabara madhara yake ni umaskini.

Na Mwandishi maalum – Dar es Salaam.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amewataka watanzania kuheshimu sheria mbalimbali za nchi ili kuepuka madhara yatakayotokana kwa kutoheshimu sheria hizo. Akizungumza leo tarehe 19 Desemba 2018 huko Kimara Stopover jijini Dar es salaam, wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa upanuzi wa njia nane wa barabara ya Morogoro kutoka eneo la Kimara hadi Kibaha mkoani Pwani, yenye urefu wa kilometa 19.2 na kugharimu shilingi bilioni 141.5. 

Rais Magufuli amewataka watanzania kutii na kuheshimu sheria za nchi kwa kutoendeleza maeneo ya hifadhi ya barabara kwani kwa kufanya hivyo ni kukiuka sheria za nchi na kujiletea umaskini. “Watanzania tujifunze kuheshimu sheria, ukisogelea barabara hasa hifadhi ya barabara madhara yake ni umaskini, nataka kuwaambia wananchi waliobomolewa nyumba zao na wakiwemo ndugu zangu ni kwa sababu ya kutoheshimu sheria” alisema Rais Magufuli

Rais Magufuli, alifafanuwa kuwa Serikali ilitumia fedha nyingi kuweka alama za kuonesha hifadhi za barabara nchi nzima lakini kwa  bahati mbaya  baadhi ya wananchi hawakutii sheria na kuendeleza maeneo hayo ya hifadhi kwa kujenga nyumba za makazi ama  za biashara. Aidha, Rais Magufuli alielezea kuwa Sheria ya barabara iliyotungwa mwaka ya 1932 na kufanyiwa mabadiliko mwaka 1967 imeainisha upana mita 90 kila upande wa barabara kutoka Ubungo hadi Stopover, na kutoka Stopover hadi Kibaha dampo upana wa mita 121 kila upande, ambapo upana wa barabara hiyo unabadilika na kupungua mita kadhaa katika maeneo mbalimbali. Vilevile, Rais Magufuli alisisitiza kuwa sheria hiyo imewekwa makusudi kwa kutambua umuhimu wa barabara hiyo inayounganisha Bandari ya Dar es Salaam, mikoa mbalimbali pamoja na nchi za jirani.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, alisema kuwa  barabara hiyo ya Morogoro itakayoitwa “Tanzania One”, ina hifadhi ya kutosha na kwa sasa inapitisha magari 50, 000 kwa siku ni muhimu kwa maendeleo ya  nchi na ukuaji wa uchumi kwa ujumla Aidha, Waziri Kamwelwe alisisitiza kuwa Serikali itasimamia sheria ili kuhakikisha barabara hiyo inadumu kwa kuzingatia matumizi yake ikiwemo uzito wa magari yanayopita katika barabara hiyo. “Kuanzia Januari, Mosi, 2019, tunaanza kusimamia udhibiti wa uzito wa magari, sisi watanzania tumeruhusu uzito wa magari tani 56 kutumia barabara zetu, Afrika kusini wanabeba tani 51, katika Afrika yote Tanzania ndio tunabeba tani nyingi, hivyo tutasimamia sheria katika kutunza barabara zetu”alisema Waziri Kamwelwe

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Miundombinu, Selemani Kakoso alisema kuwa miradi yote inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano inapitia Bungeni na wabunge kutoka vyama vyote vya siasa wanapata nafasi ya kushiriki na kuchambua kwa karibu miradi hiyo ya Serikali. “Nawaomba watanzania waiamini Serikali ya Awamu ya Tano kwani imeendelea kufanya maajabu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali mfano huu wa barabara ya njia nane, pia tulipe kodi ili tutekeleze miradi ya maendeleo ya umeme, afya na maji” alisema Kakosa.

19 December 2018, 15:36