Tafuta

Waziri Mkuu wa Tanzania: Viongozi dumisheni: sheria, kanuni na taratibu za kazi ili kujenga mafungamano mema ya kijamii! Waziri Mkuu wa Tanzania: Viongozi dumisheni: sheria, kanuni na taratibu za kazi ili kujenga mafungamano mema ya kijamii! 

Viongozi dumisheni: sheria, kanuni na taratibu za kazi!

Watumishi wote wawe na mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao. Viongozi hao wanatakiwa wasimamie nidhamu kazini na uwajibikaji wa watumishi kwa wananchi, ambapo pia amewasihi watende haki kwa wananchi na watumishi walio chini yao. Pia lazima watumishi wa Serikali wawapokee na kuwahudumia wananchi kwa staha, wawasikilize kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Na Ofisi ya Waziri Mkuu – Dodoma, Tanzania.

Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amefungua mafunzo kwa Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa, ambapo amesema baada ya mafunzo hayo Serikali inatarajia watasimamia kikamilifu nidhamu katika utumishi wa umma na wao wenyewe watakuwa kioo katika kuzingatia miiko ya utumishi wa umma. Kadhalika, Waziri Mkuu amesema viongozi hao wa mikoa watazingatia kikamilifu mipaka ya madaraka yao na kwamba hatua watakazozichukua katika uongozi na utendaji wao zitazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo nchini.

Waziri Mkuu amefungua mafunzo hayo yanayoendeshwa na Taasisi ya Uongozi Jumatatu, Desemba 3, 2018 katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wakasimamie kikamilifu mapambano dhidi ya dawa ya kulevya. “Mkadumishe uhusiano mwema baina yenu na watumishi walio chini yenu, kwa kuzingatia kuwa kila mtumishi anao mchango katika kuboresha utendaji kwenye kituo chake cha kazi. Nina matarajio makubwa kuwa mtadumisha uhusiano mzuri kikazi na viongozi wa juu na pia uhusiano wa diplomasia ya heshima na viongozi wengine ndani ya mihimili yetu mitatu.”

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka viongozi hao wahakikishe kila mmoja wao anaandaa mpango kazi unaoainisha shughuli zake za kila siku. “Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi na Wakuu wa Idara wote na Watumishi wote wawe na mpango kazi wa utekelezaji wa majukumu yao.” Amesema viongozi hao wanatakiwa wasimamie nidhamu kazini na uwajibikaji wa watumishi kwa wananchi, ambapo pia amewasihi watende haki kwa wananchi na watumishi walio chini yao. Pia lazima watumishi wa Serikali wawapokee na kuwahudumia wananchi kwa staha, wawasikilize kero zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa waendelee kusimamia amani na utulivu kwenye mikoa yao ili watu waendelee kufanya shughuli zao bila wasiwasi wowote kwani amani na utulivu ndiyo itawawezesha nchi iendelee kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje. “Tunakumbushwa sisi viongozi tuhakikishe tunaziendeleza rasilimali za nchi hii kwa faida ya Watanzania wote bila kubagua jinsia, kabila, dini, rangi ya ngozi, mtu atokako ndani ya nchi ilimradi hajavunja sheria; wala ubaguzi mwingine wa aina yoyote.  Tunaaswa tuwahudumie Watanzania wote kwa usawa.”

Kuhusu mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo, Waziri Mkuu amesema zitawawezesha viongozi hao kupata fursa ya kutafakari na kujitathmini kuhusu hatua za kujiimarisha zaidi kiuongozi na kiutendaji. “Hatua hizo ni lazima ziwe pamoja na kubadilika kwa mtazamo na kujirekebisha endapo mtabaini maeneo mliyokuwa mkikosea tangu mlipokabidhiwa ofisi hadi sasa.”  Waziri Mkuu amesema mada zitakazowasilishwa kwenye mafunzo hayo zinahusu majukumu na mipaka ya kazi, ambapo watajifunza namna ya kufanya kazi bila mikwaruzano isiyo na tija baina yao na viongozi wa mihimili mingine ya dola, viongozi wa kisiasa na watendaji wengine Serikalini. 

Amesema mada nyingine inahusu uongozi, hisia na mahusiano mahali pa kazi, ambapo itawawezesha kujiimarisha katika mbinu za kuwaongoza watumishi walio chini yao kwa kujenga na kudumisha mshikamano na ushirikiano wa pamoja. Mada itafafanua pia namna mnavyotegemeana na watumishi wa kada na ngazi mbalimbali katika kutimiza majukumu yenu. Ni muhimu sana kufanya kazi kama timu moja ili muweze kuyafikia malengo ya taasisi kwa upana wake na si malengo ya mtu au kiongozi mmoja.” Amesema kwenye mada inayohusu muundo wa Serikali na namna inavyofanya kazi watauelewa vizuri zaidi muundo wa Serikali ulivyo na jinsi unavyofanya kazi. Pia wataielewa vizuri zaidi itifaki na kuheshimiana kwa ngazi mbalimbali kutoka Waziri, Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya, Makatibu Tawala, Wakurugenzi, Wakuu wa Idara hadi Wananchi. 

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja amesema mafunzo hayo ya wiki moja yatajikita katika maeneo makuu matatu ambayo ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kufanya maamuzi ya kimkakati yanayozingatia mahitaji na manufaa mapana ya sasa na ya baadae kwa jamii. Ametaja eneo la pili kuwa ni kuimarisha uwezo wa washiriki katika kuongoza rasilimali watu na kusimamia rasilimali nyingine ili kutekeleza kikamilifu na kwa mafanikio maamuzi ya kimkakati waliyoyafanya katika kipengele cha kwanza.

“Eneo la tatu ni la kuimarisha uwezo wa washiriki katika kujijengea sifa binafsi za uongozi ili awe na ushawishi kwa wananchi anaowaongoza. Hili ni jambo la msingi, kiongozi mwenyewe awe mfano bora wa kuigwa. Awe muadilifu, mtenda haki, mfuata sheria na taratibu pamoja na kufahamu na kuheshimu miiko ya uongozi.” Mafunzo hayo yamehudhuriwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Selemani Jafo. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu, George Mkuchika, Mkuu wa mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilith Mahenge na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Josephat Kandege pamoja na maafisa wengine wa Serikali.

03 December 2018, 13:35