Tafuta

Vatican News
Mkutano wa 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP24 umefunguliwa rasmi huko Katowice, nchini Poland. Mkutano wa 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP24 umefunguliwa rasmi huko Katowice, nchini Poland. 

COP24 Katowice: Mkutano wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi

Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa ya maendeleo duniani. Athari zake ni pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; kuongezeka kwa joto; ukame; mafuriko; njaa, vita kati ya wakulima na wafugaji, pamoja na ongezeko kubwa la wadudu waharibifu wa mimea, na magonjwa ya mifugo na binadamu; kukauka kwa vyanzo vya maji; kuyeyuka kwa theluji n.k.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP 24 umefunguliwa rasmi huko Katowice, Poland, Jumapili, tarehe 2 Desemba na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 14 Desemba 2018 na unahudhuriwa na wajumbe zaidi ya 30, 000 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Wanachama wa Umoja wa Mataifa wanapaswa kuonesha mshikamano wa kimataifa kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Zinapaswa kuwa na uelewa wa pamoja sanjari na kuguswa na mahangaiko pamoja na mateso yanayoendelea kujitokeza sehemu mbali mbali za dunia kutokana na maafa asilia, ili hatimaye, kuweza kufikia makubaliano ya utekelezaji wa Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015, ili kuokoa maisha ya watu na rasilimali za dunia!

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa mjini Vatican mwanzo mwa mwaka 2018, alikazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kwani majanga asilia yamekuwa ni sababu ya maafa makubwa kwa watu na mali zao sehemu mbali mbali za dunia. Lakini, ikumbukwe kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya kazi za binadamu, kumbe, kuna haja ya watu kuwajibika pamoja na kutekeleza kwa vitendo Mkataba wa Paris wa Mwaka 2015 juu ya udhibiti wa mabadiliko ya tabianchi unaopania pamoja na mambo mengine; kupunguza hewa ya ukaa inayosababisha madhara makubwa katika afya. Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi, kwa njia ya huduma na mshikamano shirikishi kama alama ya matumaini katika ulimwengu mamboleo.

Mabadiliko ya tabianchi yamekuwa changamoto kubwa ya maendeleo duniani. Athari zake ni pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; kuongezeka kwa joto; ukame; mafuriko; njaa, vita kati ya wakulima na wafugaji, pamoja  na ongezeko kubwa la wadudu waharibifu wa mimea, na magonjwa ya mifugo na binadamu; kukauka kwa vyanzo vya maji; kuyeyuka kwa kiwango kikubwa cha theluji duniani sanjari na kuongezeka kwa kina cha bahari; mmomonyoko wa fukwe; maji chumvi kuingia katika nchi kavu. Hivi vyote vina athari kubwa sana katika masuala ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kiusalama.

Usimamizi na uratibu mkamilifu wa utekelezaji wa mipango, mikakati na miradi ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi niu muhimu sana. Kuimarisha miundombinu na uhifadhi wa taka ngumu katika miji mikubwa ili kuhakikisha mafuriko hayaleti madhara katika shughuli za kiuchumi na ustawi wa jamii; na kuboresha mfumo wa ushirikishwaji mkamilifu wa  wadau na  wananchi kwa ujumla  katika mipango na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayohusiana na mabadiliko ya tabianchi.

Makubaliano haya yanahitaji mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa ili kufanikisha utekelezaji wake, kwani athari za mabadiliko ya tabianchi hazichagui wala kubagua nchi maskini wala tajiri, wote wanaathirika ingawa kwa viwango tofauti. Hii ni changamoto ya kuwekeza katika teknolojia rafiki na mazingira. Utekelezaji huu ni hatua kubwa katika mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza mamilioni ya watu katika umaskini wa hali na kipato.

Wanasayansi na watetezi wa mazingira wanasema, utekelezaji wa makubaliano haya unaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, tayari kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu. Jambo la msingi ni kupunguza hewa ya ukaa sanjari na kudhibiti uchafuzi wa mazingira. Kila nchi mwanachama wa Umoja wa Mataifa anapaswa kuhakikisha kwamba anachangia kwa hali na mali katika mchakato huu katika ngazi ya kitaifa, kikanda na kimataifa, bila kusita na kutumbukia tena kwenye uchafuzi wa mazingira. Hii ni changamoto kwa Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha kwamba wanatekeleza kwa dhati Ajenda ya Maendeleo Endelevu na fungamani ifikapo mwaka 2030.

Utekelezaji wa makubaliano haya unajikita kwa namna ya pekee, katika utashi wa kisiasa unaopania kukuza na kudumisha mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi. Kushindwa kutekeleza itifaki hii athari zake zitaendelea kujionesha katika chumi na maendeleo ya watu duniani na ikumbukwe kwamba, waathirika wakuu ni wananchi wanaotoka katika nchi maskini zaidi duniani! Mahusiano na mafungamano ya kijamii hayana budi kufumbatwa na kuratibiwa katika: ukweli, haki na mshikamano tendaji; kwa kutambua na kuheshimu haki asili, haki msingi, utu na heshima ya binadamu pamoja na haki sawa mambo msingi katika uhuru, haki na amani, kama yanavyobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa.

Mabadiliko Tabianchi 2018
03 December 2018, 09:12