Cerca

Vatican News
Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa usalama wa maisha ya watu duniani! Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa usalama wa maisha ya watu duniani!  (AFP or licensors)

COP24 Katowice: Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kwa maisha!

Athari za mabadiliko ya tabianchi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha ubora wa maji safi na salama; usalama, uhakika na ubora wa chakula na lishe duniani na matokeo yake ni kuongezeka vifo na majanga asilia kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 ni sehemu ya mchakato wa Jumuiya ya Kimataifa kuandaa Mpango Kazi wa Utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21 uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015. Nchi zinazoendelea duniani, zinazitaka nchi tajiri zaidi kuonesha mshikamano wa dhati katika mchakato wa mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, ili kujenga matumaini ya leo na kesho kwa vizazi vijavyo!

Nchi zenye viwanda vingi duniani zilikuwa zimeahidi kuchangia walau bilioni mia moja kama ruzuku kwa ajili ya Nchi changa ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi hadi kufikia mwaka 2020; lakini hadi sasa kiwango hiki hakijafikiwa na madhara ya mabadiliko ya tabianchi yanaendelea kuongezeka kila kukicha! Benki ya Dunia, katika kipindi cha mwaka 2021-2025 itachangia kiasi cha dola za kimarekani, bilioni mia mbili kama sehemu ya mbinu mkakati wa kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotishia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Teknolojia rafiki kama sehemu ya mchakato wa kupambana na ongezeko la joto duniani bado inagonga mwamba, kwa hofu ya wafanyakazi kupoteza fursa za ajira ingawa madhara ya uchafuzi wa mazingira ni makubwa sana!

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kulinda afya ya umma kutokana na athari za mabadiliko makubwa ya tabianchi, changamoto kubwa katika mapambazuko ya karne ya ishirini na moja ambayo imejielekeza zaidi katika ukuaji wa teknolojia na viwanda kiasi cha kutishia: usalama na afya ya umma! Athari za mabadiliko ya tabianchi zimechangia kwa kiasi kikubwa kuporomosha ubora wa maji safi na salama; usalama, uhakika na ubora wa chakula na lishe duniani na matokeo yake ni kuongezeka vifo na majanga asilia kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira!  Takwimu zinaonesha kwamba, gharama ya majanga asilia duniani imeongezeka sana kiasi cha kufikia asilimia 150% katika kiwango cha kimataifa. Gharama hizi kati ya mwaka 1978-1997 zilikuwa ni sawa na kiasi cha dola za Kimarekani bilioni 895.

Takwimu kati ya mwaka 1998-2017 zinaonesha kwamba, kiasi cha dola trilioni 2. 25 zimetumika katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi sehemu mbali mbali za dunia. Shirika la Afya Duniani katika taarifa yake ya Mwezi Oktoba, 2018 lilibainisha kwamba, watoto milioni 600 wanafariki kila mwaka kutokana na magonjwa yanayoshambulia mfumo wa hewa. Uchafuzi wa hali ya hewa unatishia usalama wa maisha ya watu wengi duniani. Inakadiriwa kwamba, watu milioni 7 hufariki kila mwaka sehemu mbali mbali za dunia kutokana na uchafuzi wa mazingira.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres katika hotuba ya ufunguzi rasmi wa Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 amesikika akisema, athari za mabadiliko ya tabianchi zinatishia maisha, usalama na maendeleo endelevu ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Anaendelea kukazia umuhimu wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu “SDGs” kwani ni chachu muhimu sana kwa utandawazi wa mshikamano na haki. Kumekuwepo na ongezeko kubwa za gharama za kiuchumi, kijamii na kimazingira katika kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kumbe, umefika wakati wa kuchukua hatua zitakazosaidia kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. Kushindwa kutekeleza Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, ni kuendelea kushuhudia majanga na maafa yakiwaandama watu sehemu mbali mbali za dunia, kiasi cha kuhatarisha uchumi wa kimataifa. Mkutano huu unalenga kutoa: mwongozo, sheria, kanuni na utekelezaji wake, dhamana ambayo ni nyeti sana kwa wakati huu, licha ya madhara makubwa yanayoendelea kusababishwa na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Vatican inapenda kukazia mambo makuu yafuatayo kama sehemu ya Utekelezaji wa Makubaliano ya Mkataba wa Paris kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, COP21: Kwanza kabisa ni kanuni maadili; Pili: Utu wa mwanadamu, mapambano dhidi ya umaskini; sera na mikakati ya maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu na: Tatu ni kuweka mipango thabiti itakayokidhi mahitaji msingi ya binadamu kwa sasa na kwa siku za mbeleni!

COP24: Changamoto

 

05 December 2018, 09:51