Watoto milioni moja wa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wako hatarini wakati huu wa msimu wa baridi. Unicef inaomba msaada kwa ajili yao Watoto milioni moja wa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wako hatarini wakati huu wa msimu wa baridi. Unicef inaomba msaada kwa ajili yao 

Unicef:dola milioni 33 zinahitajika kusaidia watoto dhidi ya baridi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ombi la dola milioni 33 ili kufikisha misaada wa takribani watoto milioni moja wa maeneo ya nchi za Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini kunyemelewa na baridi ya msimu

Sr. Angela Rwezaula - Vatican

Takribani watoto milioni moja wa eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wako hatarini wakati huu ambapo msimu wa baridi kali unanyemelea eneo hilo. Kutokana na hali hiyo ambayo watoto hao wanahitaji msaada wa haraka, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF limetoa ombi la dola milioni 33 ili kufikisha misaada.

Mkurugenzi wa UNICEF wa kanda ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika, Geert Cappelaere

Katika taarifa hiyo iliyotolewa mjini Amman, Jordan, UNICEF inasema endapo haitapata msaada huo haraka  watoto hao watapata tabu wakati wa baridi kali ambapo fedha hizo zikipatikana zitatumika kuwanunulia nguo za kuleta joto, blanketi, maji na vifaa vya muhimu vya kujikimu. Mkurugenzi wa UNICEF wa kanda ya Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika Geert Cappelaere, amesema kuwa mgogoro wa muda mrefu, kuhamahama, na kutokuwa na ajira vimezifanya familia nyingi kupungukiwa na fedha. Kadhalika ameongeza kusema  kuwa uhaba wa chakula chenye lishe, huduma za kiafya, vimewafanya watoto kukonda na wako hatarini kupata magonjwa  ya njia ya hewa na bila msaada  wa kuwalinda dhidi ya baridi watoto hao watakabiliwa na hali ngumu.

Baridi pia itaziathiri familia nyingi ambazo zinaishi katika makambi

Taarifa ya UNICEF inaendelea kueleza kuwa hali ya baridi pia itaziathiri familia nyingi ambazo zinaishi katika kambi zilizojaa pomoni  huku zikiwa hazina vifaa vya kutosha vya kuwakinga dhidi ya baridi kali. Kwa mujibu wa UNICEF, watoto wawili walifariki dunia katika kipindi cha baridi kali kilichopita walipokuwa wanajaribu kusalimisha maisha yao  kutoka Siria kwenye vita hadi Lebanon. UNICEF katika kipindi chote cha baridi kali, inapanga kuwafikia watoto milioni 1.3 nchini Siria, Iraq, Jordan, Lebanon, Uturuki na Misri  kuweza kuwapa nguo za joto, blanketi, maji ,vifaa vya kujikimu katika usafi na pia kutoa pesa taslimu kwa familia.

 

 

29 November 2018, 15:15