Tafuta

Familia na Kisukari ndiyo kauli mbiu inayoongoza Siku ya Kisukari duniani kwa mwaka 2018-2019 Familia na Kisukari ndiyo kauli mbiu inayoongoza Siku ya Kisukari duniani kwa mwaka 2018-2019 

Tarehe 14 Novemba ni Siku ya Kupambana na Kisukari Duniani!

Tarehe 14 Novemba ya kila mwaka ni Siku ya kupambana na Kisukari Duniani. Kwa mwaka 2018-2019 inaongozwa na kauli mbiu ya “Familia na Kisukari”. Vipindi viwili maalum vimetolewa kuhusu mpango wa kimkakati wa Shirikisho la Kimataifa la Kisukari ili kuwezesha kupanga, kuendeleza, kukuza na kushiriki

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Leo tarehe 14 Novemba, ni Siku ya kupambana na Kisukari Duniani. Kauli mbiu ya mwaka 2018-2019 ni Familia na Kisukari. Vipindi maalumu viwili vimetolewa kuwa bora katika kufikia kampeni ya Siku ya Kisukari Duniani, kwa mujibu wa mpango wa kimkakati wa Shirikisho la Kimataifa la Kisukari na ili kuwezesha kupanga, kuendeleza, kukuza na kushiriki.

Familia zina jukumu kuu katika kushughulikia mambo yanayochangia kisukari

Vifaa na hatua zitakazochukuliwa na shirikisho hilo katika muda huo wa miaka miwili ya kampeni dhidi ya kisukari inapania kutoa hamasisho kuhusu athari ya kisukari kwa familia na mfumo wa kuwasaidia walioathirika. Kadhalika kuzisaidia familia katika juhudi za kukabili, kuwahudumia, kuzuia na kuelimisha kuhusu kisukari. Zaidi ya watu milioni 425 wameathirika na kisukari. Visa vingi vya ugonjwa huo ni vya daraja ya pili, ambayo inaweza kuzuiwa kupitia mazoezi ya kila siku, vyakula vyenye afya, na kuishi katika mazingira bora. Familia zina jukumu kuu katika kushughulikia mambo yanayochangia kisukari hiyo ya daraja la pili, na lazima wapewe mafunzo, raslimali na mazingira ya kuishi maisha mazuri.

Ni mtu mmoja kati ya wawili wanaoishi na kisukari bila kutambuliwa. Kugunduliwa mapema na kupata matibabu ni muhimu katika kuzuia matatizo yanayochangiwa na ugonjwa wa kisukari, hivyo uhamasisho kuhusu ishara, dalili, na mambo hatari kuhusu aina zote za kisukari ni muhimu sana ili kusaidia kuugundua mapema. Ugonjwa wa kisukari unaweza kuwa wa gharama kwa mtu au familia. Katika mataifa mengi, gharama ya sindano ya insulini na ufuatiliaji pekee unaweza kutumia nusu ya mapato familia, na wengi wanashindwa kupata dawa za kisukari mara kwa mara na huduma. Shirikisho la Kimataifa la Kisukari linasema hali hiyo inaashiria kuwa ni lazima kuzuia gharama kuongezwa kwa waathirika na familia zao, suala ambalo linaathiri matokeo ya afya.

Shirikisho la Kimataifa la Kisukari

Shirikisho hilo linasema kuwa ni mtu mmoja miongoni mwa watu wanne wa familia moja anaweza kufikia mipango ya elimu kuhusu kisukari. Usaidizi wa familia katika kuwahudumia waathiriwa wa kisukari umetajwa kuboresha matokeo ya afya kwa waathiriwa hao. Kutokana na hilo Shirikisho la Kimataifa la Kisukari limesema ni muhimu kwa elimu inayoendelea kutolewa kuhusu kukabili kisukari kupatikana kwa urahisi kwa waathiriwa pamoja na familia zao, ili kupunguza athari za kihisia ambayo inaweza kuathiri ubora wa maisha.

Ebu tujifunze juu ya magonjwa  yasiyo ambukiza

Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni magonjwa ambayo hayasambazwi kwa mtu mwingine kwa kuwa hakuna vimelea mwilini vinavyohusiana na magonjwa hayo. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza ni kama ya moyo na mishipa ya damu, figo, saratani, kifua sugu, kisukari, magonjwa ya akili na mengine ya kurithi kama vile ugonjwa wa selimundu (Sickle Cell Disease). Ripoti ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) inadai magonjwa yasiyo ya kuambukiza ndio chanzo kikubwa cha vifo ulimwenguni, yakifanya ongezeko la vifo vyote kwa kila  mwaka. Magonjwa yasiyo ya kuambukiza huua watu zaidi ya milioni 36 kila mwaka. Inakisiwa kuwa mwaka 2020 magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza yatasababisha asilimia 73 ya vifo vyote duniani na asilimia 60 ya ukubwa wa tatizo la magonjwa duniani.

Kisukari ni moja ya muuaji wa kimya kimya, na je kisukari  nini?

Kisukari ikiwa ni moja ya muuaji wa kimya kimya katika kundi hili la magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Watu milioni 285 duniani kote wameathiriwa na kisukari ambayo ni sawa na asilimia 6.6 ya idadi ya watu wote ulimwenguni pia ikishika nafasi ya 5 kwa kusababisha vifo duniani. Nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya watu wenye kisukari ni China wagonjwa milioni 43.2, India wagonjwa milioni 40.9, Marekani wagonjwa milioni 25.8, Urusi wagonjwa milioni 9.6 na Brazil wagonjwa milioni 6. Nchi zenye idadi kubwa ya watu wazima wenye kisukari ni Nauru kwa asilimia 30, Bahrain kwa asilimia 25.5, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa asilimia 25, Saudi. Sukari mwilini hutokana na vyakula pamoja na vinywaji tunavyotumia kila siku na hutumika kuupa mwili nguvu. Glukosi ni aina ya sukari ambayo huzipa chembe za mwili nishati. Hata hivyo ili glukosi iingie ndani ya chembe hizo inahitaji insulini. Insulini ni kemikali (Homoni) ambayo hutokezwa na kongosho (Pancrease).

Kisukari ni ugonjwa unaotokana na mtu kuwa na sukari nyingi kupita kiasi kwenye damu. Ugonjwa huo huvuruga utaratibu wa kuingiza sukari ndani ya chembe kutoka kwenye damu kwa kuwa chembe huhitaji sukari ili kupata nishati. Ugonjwa wa Kisukari hutokea pale ambapo tezi ya kongosho inaposhindwa kutengeneza kichocheo (Homoni) aina ya insulin au pale mwili unaposhindwa kutumia vizuri kichocheo hicho na kusababisha kuongezeka kwa sukari (Hyperglycemia) au kushuka kwa kiwango cha sukari (Hypoglycemia). Ugonjwa wa kisukari unaweza kusababishwa na kuwa na kiwango kidogo cha insulin mwilini, mwili kutosikia kichocheo hicho au yote mawili.

Takwimu mbalimbali za ugonhwa wa kisukari

Kulingana na ripoti mbalimbali karibu watu milioni 316 ulimwenguni pote wana kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu, ingawa wengi wao hawajui wana kiwango hicho. Kwa mfano, nchini Marekani pekee asilimia 90 ya watu wenye sukari nyingi kwenye damu hawatambui kama wana tatizo hilo. Ingawa asilimia 8.3 ya watu watu wa Marekani wana Kisukari ambayo ni sawa na watu milioni 25.8 na kufanya Kisukari cha 7 kusababisha vifo vya watu Marekani. Mamilioni ya watu wana ugonjwa huo lakini hawana habari! Ni ngumu zaidi kutibu ugonjwa wa kisukari kwa kuwa mtu anaweza kuishi nao kwa muda mrefu kabla haujagunduliwa. Hiyo ndiyo sababu watu husema kwamba ugonjwa huo huua kimyakimya.

Nini chanzo cha kisukari

Ili kuelewa vyema ugonjwa wa kisukari ni muhimu kwanza kuelewa namna chakula kinavyovunjwa vunjwa na kutumiwa na mwili ili kuzalisha nguvu. Wakati chakula kinapoyeyushwa matukio kadhaa hutokea. Moja ni sukari inayoitwa glucosi ambayo ni chanzo cha nishati/nguvu mwilini huingia katika damu. Tukio la pili ni kiungo kinachoitwa kongosho (Pancrease) kutengeneza kichocheo cha insulini. Kazi ya insulini ni kuondoa glucosi katika damu na kuingiza katika misuli, seli za mafuta na ini, ambako hutumika kama nishati. Watu wenye kisukari huwa na kiwango kikubwa cha sukari kwenye damu kuliko inavyotakiwa kwa sababu miili yao haiwezi kupeleka sukari kwenye seli za mafuta, ini na misuli ili ihifadhiwe kwa ajili ya kuzalisha nguvu. Hii ni kutokana na moja ya sababu zifuatazo, huenda kongosho zao haziwezi kutengeneza insulini ya kutosha au seli za mwili wao haziathiriwi na insini kama inavyotakiwa au sababu zote hizo mbili. Kula sukari nyingi sio sababu ya ugonjwa wa kisukari. Lakini lazima tuseme kwamba kula sukari nyingi si nzuri kwa afya yako kwani utaongeza uzito wa kuweza kuathiri uwezo wa mwili wako kujikinga na maradhi tofauti. Ugonjwa wa kisukari umeitwa kwa kufaa "ugonjwa unaoathiri kiini cha nishati ya mwili". Mwili unaposhindwa kutumia glukosi, mifumo mbalimbali ya mwili inaweza kuacha kufanya kazi au hata kusababisha kifo.

Ugonjwa wa Kisukari kitaalamu hujulikana kama 'DIABETES MELLITUS'. Jina 'Diabetes Mellitus' linatokana na neno la Kigiriki linalomaanisha 'kunyonya' na neno la Kilatini linalomaanisha 'tamu kama asali'. Maneno hayo yanafafanua vizuri sana ugonjwa huo, kwani maji hupita mwilini mwa mtu aliye na ugonjwa wa kisukari kana kwamba yananyonywa na mdomo na kupitia kwenye njia ya mkojo kisha kutoka nje ya mwili. Isitoshe mkojo huwa na ladha tamu kwa kuwa una sukari. Ndiyo sababu kabla ya kuvumbua njia bora za kupima ugonjwa huo, mbinu moja ya kutambua kama mtu ana ugonjwa wa kisukari ilikuwa kumwaga mkojo wa mgonjwa karibu na kichuguu cha sisimizi. Ikiwa sisimizi wangevutiwa na mkojo huo basi hilo lilimaanisha kwamba mkojo una sukari.

Je ni nani anaweza kuwa na uginjwa wa kisukari

Watu walio katika makundi yafuatayo wana uwezekano mkubwa wa kupata ugonjwa wa kisukari:Wenye uzito uliozidi; wenye historia ya kuwa na wagonjwa wa kisukari katika familia zao; Wanawake waliozaa watoto wenye kilo 4 au zaidi;Watu wasiojishughirisha au wasiofanya mazoezi; Wenye shinikizo la damu; Wenye msongo wa mawazo na Wenye matumizi makubwa ya pombe na sigara.

Kutokana na hili, watu hawa wanashauriwa kupima sukari yao kila mwaka wakiwa na umri wa miaka 45 na kuendelea. Kuna hatari kubwa ya kuugua ugonjwa huo ikiwa mtu ana mafuta mengi katika tumbo na kiuno chake kuliko katika mapaja yake. Mafuta katika kongosho na ini huvuruga uwezo wa mwili wa kudhibiti kiasi cha sukari kwenye damu. Wavutaji wa sigara wanakabiliwa na hatari kubwa zaidi kwani zoea hilo hudhuru moyo na mfumo wa mzunguko wa damu na kubana mishipa ya damu. Kitabu kimoja kinasema kwamba asilimia 95 ya watu wanaougua kisukari ambao hulazimika kukatwa viungo ni wavutaji wa sigara.

Zitambue dalili za ugonjwa wa kisukari

Kunywa maji mengi kuliko kawaida na kusikia kiu kila wakati. Kwenda haja ndogo mara kwa mara. Watoto kukojoa kitandani. Kuwa dhaifu, kukosa nguvu na kujisikia mchovu kila wakati. Kupungua uzito au kukonda licha ya kula vizuri. Kusikia njaa kila wakati na kula sana. Wanawake kuwashwa ukeni. Kutoona vizuri. Kupungua nguvu za kiume au hamu ya kujamiiana kwa wanawake. Ganzi, kuchomwachomwa au kutohisi unapoguswa sehemu za miguu, viganja na vidole. Miguu kuoza na hata kupata gangrini. Kukaukwa na ngozi na pia kupata aina ya ngazi katika miguu. Vidonda au majeraha sehemu yoyote ya mwili kutopona haraka. Majipu mwilini. Kutokana na hilo, wenye dalili hizi wanashauriwa kupima sukari ili kubaini kama wana kisukari.

 

 

 

 

14 November 2018, 15:48