Katika uzinduzi wa Maktaba mpya ya kisasa jijini Dar Es Salaam,Rais Magufuli amesema maktaba hiyo ni nyumba ya maarifa hivyo itasaidia kuinua kiwango cha elimu Katika uzinduzi wa Maktaba mpya ya kisasa jijini Dar Es Salaam,Rais Magufuli amesema maktaba hiyo ni nyumba ya maarifa hivyo itasaidia kuinua kiwango cha elimu  

Tanzania:maktaba kubwa zaidi Afrika Mashariki imezinduliwa!

Rais John Magufuli amezindua maktaba ya kisasa ya mfumo wa teknolojia ya mawasiliano na ambayo inaelezwa kuwa kubwa zaidi Afrika mashariki. Uzinduzi huo ulifanyika tarehe 27 Novemba 2018 katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Tanzania

Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Maktaba ya kisasa inayotumia mfumo wa teknolojia ya mawasiliano ambayo inaelezwa ndio kubwa zaidi katika eneo la Afrika Mashariki pamoja kusini mwa Afrika, imefunguliwa tarehe 27 Novemba katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais John Magufuli wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Katika hotuba yake  kwenye ufunguzi wa maktaba hiyo iliyojengwa kwa ufadhili wa nchi ya China, Rais Magufuli amesema maktaba hiyo ni nyumba ya maarifa hivyo itasaidia kuinua kiwango cha elimu pamoja na maendeleo katika sekta nyingine kupitia utafiti.

Hata hivyo mapema, makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa  William Anangisye ameelezea uwezo wa maktaba hiyo katika kuwahudumia wanafunzi. Na pia wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wamekiri kufurahishwa na ujenzi wa maktaba hiyo.

Kwa mujibu wa balozi wa China nchini Tanzania, Daktari Wang Ke, amethibitisha kuwa nchi yake imetumia kiasi cha dola za kimarekani million 41 kujenga maktaba hiyo ya kisasa pamoja na kituo cha kufundishia lugha ya kichina. Ujenzi wa maktaba hiyo ni mradi wa pili mkubwa kufadhiliwa na China nchini Tanzania, baada ya ule wa reli ya Tazara, kutoka Tanzania hadi Zambia, iliofunguliwa kunako mwaka 1975.

Katika tukio lisilotegemewa, Rais  Magufuli alimpongeza hata Waziri Mkuu  wa zamani Edward Lowassa ambaye alikuwa ni mmoja wa wageni katika hafla hiyo kwa kumtaja kuwa ni mwanasiasa aliyekomaa lakini akitoa onyo kwa wanasiasa wanaovunja sheria. Pamoja na hayo hata Bwana Lowasa  ameipongeza juhudi zinazofanywa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na serikali kwa ujumla  katika kuimarisha elimu.

 

29 November 2018, 14:39